Wanawake nchini Korea Kusini watakuwa wa kwanza duniani kuwa na umri wa kuishi wa zaidi ya miaka 90, utafiti unaonesha.
Utafiti
huo uliofanywa na Chuo cha Imperial cha London na Shirika la Afya
Duniani uliangazia umri wa kuishi katika mataifa 35 yaliyostawi
kiviwanda.Utafiti huo unaonesha watu watakuwa wakishi miaka mingi kuliko sasa kufikia mwaka 2030 na pengo kati ya wanaume na wanawake litaanza
kufutika katika mataifa mengi.
Watafiti hao wanasema matokeo ya utafiti wao ni changamoto kwa hazina za malipo ya uzeeni na vituo vinavyowatunza wazee.
"Korea Kusini imefanya mambo mengi kwa njia ifaayo," Prof Majid Ezzati aliambia BBC.
"Wanaonekana kuwa na mazingira yenye usawa na mambo yao mengi yamewafaa watu kwa juma - elimu, lishe - watu wengi wamenufaika.
"Na kufikia sasa, wanafanya vyema katika kukabiliana na shinikizo la damu na wana viwango vya chini zaidi vya unene duniani."
Takwimu hizo pia zinakadiria kwamba Japan, ambayo zamani ilifahamika kwa raia wake kuishi maisha marefu, inaendelea kushuka.
Kwa sasa, ina kiwango cha juu zaidi cha umri ambao wanawake huishi, lakini itapitwa hivi karibuni na KOrea Kusini na Ufaransa, utafiti huo unadokeza.
Umri wa wanaume kuishi Japan nao utashuka kutoka kuwa wa nne miongoni mwa nchi zilizochunguzwa hadi nambari 11.
Marekani yabaki nyuma
Marekani pia haijafanya vyema kwa mujibu wa utafiti huo na huenda ikawa na kiwango cha chini zaidi cha umri wa kuishi miongoni mwa mataifa tajiri kufikia 2030.Utafiti huo unabashiri kwamba kiwango cha wastani cha umri wa wanaume kuishi Marekani kitakuwa miaka 80 kwa wanaume na 83 kwa wanawake, karibu sawa na Mexico na Croatia wakati huo.
Marekani pia itakuwa imepitwa na Chile, ambapo wanawake watakaozaliwa 2030 watatarajia kuishi miaka 87 na wanaume 81.
Kati ya 2015 na 2030, umri wa kuishi Uingereza utapanda kutoka 79 hadi 82 kwa wanaume na 83 hadi 85 kwa wanawake.
Wanaume wanapanda
Utafiti huo, ambao matokeo yake yamechapishwa katika jarida la Lancet, unaonesha pengo kati ya umri wa kuishi kati ya wanawake na wanaume linapungua.Prof Ezzati alisema: "Wanaume kawaida waliishi maisha yasiyo ya afya, na hawaishi muda mrefu ukilinganisha na wanawake. Walikunywa pombe na kuvuta sigara zaidi, na waliuawa sana nyumbani au kufa kwenye ajali barabarani. Hata hivyo, mtindo wa maisha kati ya wanaume na wanawake sasa unakaribia kufanana. Hivyo, umri wa wanaume kuishi unaonekana kuongezeka."
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni