Zikiwa zimesalia siku 42 kufika tarehe 1 Machi 2015, tarehe ambayo kwa mujibu wa kifungu cha 5 cha Sheria ya Kura ya Maoni ndiyo siku ambayo Asasi za Kiraia baada ya kupewa ruhusa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi zitaanza kutoa elimu ya uraia juu ya Katiba Inayopendekezwa.
Kwa kawaida Elimu ya Mpiga Kura hutolewa kila panapokuwapo uchaguzi ama wa kitaifa kwa maana ya uchaguzi wa Rais au katika ngazi ya jimbo kwa maana ya uchaguzi wa ubunge na halkadharika katika ngazi ya kata kwa maana ya uchaguzi wa udiwani. Elimu ya mpiga kura lengo lake hasa ni kumuandaa mpiga kura kwa kumpa maarifa juu ya faida za kupiga kura kama raia, namna ya kuwabaini viongozi wazuri ambao anaweza kuwapa dhamana kwa kutumia kura yake, lakini pia elimu ya mpiga kura hugusa mambo mengine muhimu kama vile utaratibu wa kupiga kura, makatazo na jumla ni hamasa ya kujitokeza siku ya upigaji kura.
Kwa upande wa Tanzania Bara kipindi hiki na kama kweli bado Aprili 30 iko pale pale basi Watanzania wanaoishi upande huu watapata fursa ya kushiriki pamoja na Watanzania wanaoishi Tanzania Zanzibar katika zoezi adhimu, adimu na la kihistoria la Kura ya Maoni. Kura ya Maoni ndiyo itakuwa hatua ya mwisho katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya, siku hiyo raia wa Tanzania hasa wale walioandikishwa katika daftari la kudumu la mpiga kura watafanya uamuzi wa kuipitisha au kutoipitisha Katiba Inayopendekezwa.
Kwa msomaji ambaye anasoma makala hii kwa mara ya kwanza ni vyema akaelewa hatua hii ya Kura ya Maoni imetanguliwa na hatua tatu muhimu ambazo kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 ni Wananchi kote nchini kutoa Maoni yao (Hatua ya kwanza), Wananchi kote nchini kupitia mabaraza ya Katiba takribani 179 na kuleta Watanzania 18,000 yale yaliyosimamiwa na Tume ya Katiba na yale yaliyoendeshwa na Taasisi mbalimbali zaidi ya 600 na kuleta Watanzania zaidi ya milioni nane (Hatua ya Pili), na Bunge Maalumu la Katiba, ambalo pia lilileta pamoja wajumbe zaidi ya 600 wakijumuisha wabunge wote wa Bunge la Jamhuri, wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi na wajumbe wengine 201 kutoa Taasisi na asasi mbalimbali (Hatua ya Tatu).
Matarajio yangu ni kwamba zoezi kama hili muhimu kabisa lapaswa kupewa uzito linaoustahili. Kule Uingereza mwaka jana (2014) walipiga kura ya maoni na tangazo la siku ya kupiga kura lilitolewa mwaka mmoja kabla yaani 2013. Hapa kwetu tangazo la kupiga kura ya maoni limetolewa Mwezi Oktoba Mwaka jana (2014) ikiwa ni miezi saba kabla ya tarehe ya Kura ya Maoni. Najaribu kulinganisha nchi hizi mbili kwa maana kwamba kule Uingereza ambako wenzetu wametangulia mbele karibu kwa kila sekta ilionekana notisi ya mwaka mmoja ingewatosha kwa wananchi wao kujua zoezi lililo mbele yao, wawe na mjadala mpana na wajiandae kisaikolojia na matokeo ya uamuzi wao.
Waingereza wale hasa kule Uskochi waliona mwaka mmoja kwa mazingira yao ungetosha, na ninaposema mazingira yao nazungumzia miundo mbinu kama barabara za kufika huku na huko kufanikisha zoezi la Kura ya Maoni, ninazungumzia mawasiliano ya kila namna, redio, televisheni, magazeti ya kuchapa na ya mtandaoni, matangazo mbalimbali na pamoja na kuandaa utaratibu mzima wa kuendesha kura ya maoni. Kwa hakika mwaka mmoja uliwatosha na sisi tu mashuhuda kwamba kura ile ya maoni kule Uskochi ilikwenda kwa mafanikio makubwa, kwanza walioandikishwa walikuwa wengi kifani tofauti na matarajio ya wengi hasa hasa wale ambao walikuwa wanapiga kura ya mara ya kwanza, kundi la vijana na matineja.
Wananchi kule waliandikishwa kwa wingi na kwa wakati, kisha kukawa na elimu ambayo ilikuwa motomoto ambayo ilifuatiwa na kampeni ya kukata na shoka kutoka kambi mbili kubwa zilizojitanabaisha kama “Ndio kwa Uskochi” au kwa Kiingereza “Yes Scotland” wakitaka Uskochi Huru nje ya Umoja wa Ufalme wa Uingereza (UK) na kambi ile ya “Bora Kuwa Pamoja” au kwa Kiingereza “Better Together” waliotaka Uskochi iendelee kuwa sehemu ya Umoja wa Ufalme wa Uingereza (UK).
Utaona natoa mfano huu wa Uskochi nikifananisha na hapa kwetu, sina nia ya kuiga kwasababu naheshimu sana ule usemi niliojifunza kitambo kutoka kwa mshauri wangu mmoja nadhani ni Dokta Maselle Nzingula Maziku usemao “a leader does not compare his or her success by comparing with others but by the set goals prior set” yaani “Kiongozi hapimi mafanikio yake kwa kujilinganisha na wengine bali kwa malengo aliyokwisha jiwekea awali”. Naheshimu pia ule usemi usemao “tunajifunza kwa wengine”, hivyo basi mfano wangu wa Uskochi utufundishe kuona kama wenzetu walitenda vile basi hata sisi kwa mazingira yetu twaweza tenda kwa namna yetu pasina kusahau uhalisia ni uleule.
Sasa tukirudi hapa nyumbani najiuliza na nikitizama mazingira yetu, barabara zetu, ukubwa wa nchi yetu yenye kilometa za mraba zaidi ya 945,000 na mtawanyiko wa wananchi wetu hasa wale wenye sifa za kushiriki kupiga Kura ya Maoni. Maandalizi ya teknolojia itakayotumika ile ya “biometric Voter Registration” (BVR) ambayo ni ngeni kabisa, teknolojia hii itatumika kuwaandikisha wapiga kura kielektroniki, zoezi hili si lelemama. Wananchi wetu wanapaswa kuandaliwa kimaarifa juu ya mfumo huu mpya utakaotumika kuwaandikisha yasije tokea yale ya Malawi, wao walipoanza ilileta shida kidogo, watu wenye hila huwa hawakosekani katika jamii yoyote ile. Hapa nazungumzia wale wenye tabia za kujiandisha sehemu mbili au wengine wajanja kwa hila watajiandikisha hata sehemu tano, sijui wana uwezo gani, sijui huwa wanapaa kutoka kituo kimoja kwenda kingine au sijui ni uwezo mkubwa wa bodaboda kwenda haraka, hata sijui.
Wajanja hawa wenye hila kwenye “BVR” ndiyo mwisho wao. Kuna jamaa mmoja mwingi wa porojo akaniambia wako wajanja-hila wengine huvuka hata na majahazi kwenda Zanzibar “kusaidia” kupiga kura licha ya kwamba wao ni wakazi miaka nenda rudi wa huku bara, wajanja-hila kama hawa wanaweza kujikuta ni wakazi wa Bara lakini wakapata kitambulisho cha kupiga kura kutoka Zanzibar sasa unaweza “ukasaidia” kura za maoni kule Zanzibar lakini kadri siku zinavyokwenda utagundua haki zako za kushiriki uchaguzi huku bara au eneo lingine lolote halisi ukaikosa, kabla ya kuwa mamluki naomba utafakari.
Sasa msomaji wetu, nakuuliza, ndani ya siku 42 zilizobaki kabla ya elimu kuanza, je, tunaweza kuwaandikisha wapiga kura wote takribani Milioni 20? Je, vile vifaa vya “BVR” ambavyo baada ya majaribio vitakuwa vimeshafanyiwa maboresho kule kiwandani, vikarudishwa tena hapa Tanzania kwa majaribio ya mwisho ili sasa kiwanda kifyatue vifaa vyote zaidi ya 7000 ili zoezi liende bila Changamoto tulizozibaini awali? Je, tuna muda wa kutosha kutoa elimu ya namna ya kujiandikisha hasa kwa kutumia huu utaratibu na mfumo mpya wa uandikishwaji wa “BVR”? Je, siku 42 tunaweza zaidi kwa mazingira yetu na kupata mafanikio makubwa kama yale ya wenzetu Uskochi? Najua kwa wengine maswali yangu ni ya kipuuzi lakini nikuhakikishie ni katika upuuzi dunia yetu imepiga hatua, ni katika mawazo madogo madogo tu, dunia ilibadilishwa na kuwa ilivyo leo yenye tija, ugunduzi, ubunifu na maendeleo tofauti na zama za mawe.
Natamani kweli mwanasiasa fulani ajitokeze na ayaseme haya waziwazi maana ni kwa maslahi ya Taifa, mwanasiasa huyo atakuwa ameamua kusimama upande wa wananchi katika kulinda Uhuru na Umoja wa Taifa letu, natamani kumwona mwanasiasa huyo. Ndugu Wananchi kama akikosekana basi, simameni wenyewe na muwasaidie wanasiasa kujua kuna maslahi ya nchi kwanza kisha maslahi binafsi hufuata baadaye.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni