JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linamshikilia raia wa Kuwait, Hussein Mansour (34), baada ya kukamatwa Uwanja wa Ndenge wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) usiku wa kuamkia jana akijaribu kusafirisha kenge hai 149.
Kenge hao wana thamani ya Sh milioni 6.3.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Kamishina Msaidizi, Hamis Seleman, alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akijiandaa kusafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kuwait kwenda nchini Dubai.
Alisema polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa baada ya kufika eneo la ukaguzi, ambako alionekana akihaha namna ya kusogeza mizigo yake.
“Baada ya kufika eneo la ukaguzi wa mizigo, wataalamu wetu walimtilia shaka baada kuona kwenye begi lake kuna kitu ambacho si cha kawaida.
“Polisi kwa kushirikina na wafanyakazi wa mamlaka ya viwanja vya ndege, walimweka chini ya ulinzi kwa ajili ya kujiridhisha,” alisema Seleman.
Alisema baada ya upekuzi ndipo walikuta kenge hao, ambao wote walikuwa hai.
Kamanda Seleman alisema mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa akisubiri taratibu za kisheria ili afikishwe mahakamani.
Alisema kenge hao wamekabidhiwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kuwahifadhi.
Kamanda Seleman, alitoa wito kwa wananchi kuwa wazalendo na nchi yao kwa kuacha tabia ya kuuza rasilimali kwa raia wa kigeni.
“Huyu raia wa kigeni amekuja nchini juzi, leo (jana) kama angefanikiwa kuondoka fedha zote na rasilimali hizi angekwenda nazo, tena kibaya hana kibali kinachoonyesha uhalali wa kumiliki kenge.
“Hii ni hasara kwa Serikali, lakini pia kwa taifa letu kwa sababu kenge watapungua kwa kiasi kikubwa kama wataendelea kuibwa hivi,” alisema.
09 Januari 2015
Raia wa Kuwait akamatwa na kenge 149
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni