JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limeendelea na kamatakamata ya vijana wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha na uporaji, walio maarufu kwa jina la Panya Road.
Watuhumiwa 329 zaidi wametiwa mbaroni jana katika operesheni iliyofanyika katika mikoa miwili ya kipolisi, Temeke na Ilala na kufanya idadi yao kufikia 953.
Operesheni hiyo inatokana na tukio la Januari 2, mwaka huu katika eneo la Magomeni Kagera ambapo vijana hao walipambana na polisi, ambapo 36 walikamatwa.
Akizungumzia operesheni hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki, alisema imefanyika maeneo mbalimbali ya mkoa wake.
Alisema maeneo ambayo vijana wengi wamekamatwa ni kwenye vijiwe vya wanaojihusisha na uvutaji bangi, dawa za kulevya na unywaji wa pombe haramu ya gongo.
“Vijana hawa hawana dhamana kwa sababu ndio chimbuko la kundi la Panya Road, wanaohatarisha amani kwa wananchi ambao wanashindwa kufanya kazi zao kwa uhuru na amani,” alisema Kamanda Nzuki.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya Kihenya, alisema uchunguzi wa baadhi ya wahalifu waliokamatwa umekamilika na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Alisema wahalifu 68 kati ya 168, uchunguzi wao umekamilika na watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
“Wapo wengine tuliwakamata kwa bahati mbaya tumewaachia, lakini 68 uchunguzi wao umekamilika tutawafikisha mahakamani wakati waliosalia wanaendelea kuchunguzwa,” alifafanua Kamanda Kihenya.
Kutokana na kuongezeka kwa idadi kubwa ya vijana wanaofanya uhalifu huo, MTANZANIA ilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleimani Kova, kwa lengo la kujua watuhumiwa hao wamehifadhiwa wapi.
Kamanda Kova, alisema idadi ya vijana waliokamatwa ni kubwa, lakini baadhi yao uchunguzi umeshakamilika na wameshafikishwa mahakamani, wengine wanaendelea kuwahoji na taarifa nyingine ataitoa leo.
09 Januari 2015
Panya Road wafurika mahabusu Dar
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni