ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Balozi Adadi Rajabu, ametaka makamanda na
maofisa wa Jeshi la Polisi kuwadhibiti viongozi wao wa mikoa na wilaya katika masuala ya kisheria; kabla mambo hayajawaharibikia watendaji hao wa serikali.
Balozi Rajabu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, alitoa ushauri huo jana katika kikao cha kazi cha mwaka cha maofisa waandamizi wa polisi, makamanda wa mikoa na vikosi, kilichofanyika hapa Dodoma.
“Nyinyi mnatakiwa kuwashauri viongozi wenu wa mikoa na wilaya,” alisema Balozi Rajabu kwa sababu “viongozi wa kisiasa sisi tunajua mambo ya siasa tu.
“Mambo ya sheria na taratibu mbalimbali ni muhimu nyinyi mkawashauri viongozi wenu.”
Alisema pindi maofisa waandamizi wa polisi, makamanda wa mikoa na vikosi wanapoona kiongozi wa mkoa wake anakwenda kinyume cha sheria, amzuie na kumwambia huo sio utaratibu.
“Sasa wewe unapoona kiongozi wako wa mkoa anakwenda kinyume mtonye (mshitue), mwambie huo sio utaratibu, utaratibu ni huu basi mambo yatakwenda vizuri," alisema Balozi Rajabu.
“Usingoje (mpaka) mambo yameharibika.”
Katika hotuba yake hiyo Balozi Rajabu hakutoa mifano, lakini Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ni moja ya watendaji ambao wamelaumiwa katika siku za karibuni kwa kukiuka sheria.
Katika awamu mpya ya vita dhidi ya dawa za kulevya aliyoanzisha mwanzoni mwa mwezi uliopita, Makonda litaja hadharani majina ya washukiwa, wakiwamo wasanii, wafanyabiashara wakubwa, wanasiasa na kiongozi mmoja wa dini.
Hatua hiyo ililalamikiwa vikali, ikiwamo Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kufungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu, akipinga kitendo cha Makonda kumtangaza mtuhumiwa wa biashara ya mihadarati.
TUME YA MADAWA
Tangu hapo, vita dhidi ya mihadarati nchini inaongozwa na Tume ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya, chini ya Kamishna James Sianga ambaye anaendesha shughuli zake kimya kimya.
Balozi Adadi alisema kusawazisha kitu ambacho kimeharibika ni ngumu sana kuliko kuzuia kitu ambacho kinataka kufanyika.
Aidha, Balozi Adadi ambaye ni Mbunge wa Muheza (CCM), alisema serikali inategemea sana Jeshi la Polisi na kwamba kamati yake itaendelea kuibana ili lipate bajeti nzuri itakayowawezesha kufanya kazi ambazo zinatakiwa.
“Sisi kazi yetu ni kutunga sheria, lakini utekelezaji wa sheria mbalimbali ni nyie Jeshi la Polisi," alisema Balozi Rajabu.
"Zipo idara nyingine ambazo pia zinatekeleza mambo mengi ya sheria zinazotungwa na Bunge, lakini kwa ujumla wake utakuta kwamba Jeshi la Polisi lina uwezo wa kuingia katika kila idara.”
Alisema jeshi hilo lina mamlaka ya kukamata dawa za kulevya, rushwa na hata rasilimali za misitu ingawa kuna idara zake.
Kuhusu vita ya dawa za kulevya, Balozi Rajabu alipongeza jitihada zilizopo katika kukabiliana na janga hilo huku akisema ni vyema kesi zisimamiwe kadri inavyowezekana kwa kuwa wananchi wanataka kujua matokeo ya watu waliokamatwa.
Akifungua kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba aliwataka maofisa hao kutotumia taarifa ya watu wanaohasimiana katika kufungua mashtaka.
Alisema ni vyema wakazitumia taarifa hizo kama chanzo katika kufanya uchunguzi kwa kutumia weledi kwa kupeleleza na kufanyanyia kazi.
Aidha, Mwigulu alisema uhalifu kwa mwaka 2016 uliongezeka kwa makosa makubwa kufikia 75,487 ukilinganisha na 68,814 ya mwaka 2015.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu alisema askari yeyote atakayekwenda kinyume na maadili atakuwa hafai kuendelea katika jeshi hilo na kamwe hawatawavumilia.
28 Machi 2017
DCI ataka Polisi iwadhibiti ma-RC
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni