Miezi michache tu baada ya mkongwe wa Muziki wa Afro Pop Bongo, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ kumtambulisha ‘baby’ wake mpya, raia wa
Nigeria aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Spicy, fununu zinadai kuwa penzi la wawili hao limefikia tamati. Chanzo chetu kilicho karibu na msanii huyo aliyefanikiwa kubaki juu kwenye chati kwa miaka mingi, kililiambia Risasi Mchanganyiko kuwa Jide amekorofishana na mpenzi wake huyo, lakini sababu hasa za kutokea kwa jambo hilo hazifahamiki.
“Mimi ninamfahamu kwa miaka mingi Jide, ni msiri sana, lakini uzuri wake ni mtu wa mafumbo, huwa anaongea kwa mafumbo, sasa umeona alichokiandika Twitter? Nenda kasome ndiyo utaelewa nini ninamaanisha,” kilisema chanzo hicho.
Risasi Mchanganyiko lilipoifuata akaunti ya Twitter ya mwimbaji huyo anayetarajia kuzindua albamu yake ya saba mwishoni mwa mwezi huu, lilikutana na maandiko yaliyosomeka; “Ni kweli niliamua kuondoka, nikidhani nitapendwa niendako HAKUNA, Nilidhani nitakuta tofauti yoyote mpaka sasa sijaona.” Chini ya maandishi hayo, mashabiki mbalimbali wa mwimbaji huyo walikuwa na maoni tofauti, wengine wakisema inaashiria kuwa mwisho wa penzi hilo, huku wengine wakisema huenda ni mambo yao ya muziki.
“Jide siyo mtu wa kusemasema mambo yake kirahisi, ana moyo wa peke yake, ni mtu anayeweza kukaa na kitu moyoni na watu wasijue, unapomuona anaanza kutupa vijembe kama hivi, ujue kuna jambo, mimi nadhani siku si nyingi zijazo, kuna mshindo mkubwa utatokea ,” alisema shabiki mmoja.
Mtumwingine aliyechangia katika akaunti hiyo, alimtaka mwimbaji huyo kuweka wazi juu ya kilichotokea au kinachokuja, kuliko kuanza mafumbo yanayoweza kuwafanya watu wakazungumza vitu ambavyo kimsingi havipo kabisa.
“Dada funguka, kama shemela kazingua tuambie, halafu wala usikonde, siku hazigandi,” alisomeka msomaji huyo.
Lakini ili kupataukweli wa tukio hilo, Risasi Mchanganyiko lilifanya jitihada za makusudi za kumfikia Lady Jaydee, ambaye hata hivyo, simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa. Meneja wa mwimbaji huyo, Seven Mosha alipatikana kupitia simu yake ya mkononi na
alipoelezwa kusudi la kupigiwa, aliguna na kuomba muda ili awasiliane na msanii wake, akiahidi kurejea kwa mwandishi ili kumpa kilichopo.
Dakika kadhaa baadaye, Seven, ambaye pia anamsimamia mkali mwingine wa Bongo Fleva, Ali Kiba alipiga simu; “Nimeongea na Jide, kwanza amekiri kweli kile kilichopo Twitter ni chake, yaani aliandika yeye, lakini kuhusu kama ameachana na Spicy au la, amesema hilo hawezi kuliongelea kwa sasa, muda muafaka ukifika atazungumza.
Swali: Lakini mashabiki wanasema Jide ni msiri sana na kwa vyovyote kuna kitu, kwa nini usigusie walau hata kama kuna mzozo, maana haya ni mambo ya kawaida kwa wapenzi.
Seven: Ninasema kile ninachokijua na nilichoambiwa na Jide mwenyewe. Mimi sijaona kama kuna tofauti yoyote kati yao na isitoshe haya ni mambo binafsi ambayo mimi siyasimamii, lakini msanii mwenyewe ameniambia muda muafaka utafika atalizungumzia, naomba unielewe hivyo. Mwishoni mwa mwaka jana, wakati wa onyesho maalum la Tuzo za East Africa Radio, zilizofanyika Mlimani City, Jide aliyeshinda mojawapo ya tuzo hizo, alimtambulisha Spicy, raia wa Nigeria kuwa ndiye mpenzi wake mpya. Katika uhusiano wao, wamesharekodi wimbo mmoja uitwao Together ambao bado unafanya vizuri katika redio za Tanzania na Nigeria.
16 Machi 2017
HALI TETE KWA LADY JAYDEE NA MNIGERIA
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni