05 Oktoba 2014

PINDA AMPINGA KIKWETE

SIKU chache baada ya Bunge Maalum la Katiba kupitisha kwa mbinde katiba inayopendekezwa, Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwapo kwa mpasuko mpya ndani ya Chama. Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali.

Mpasuko huo umewagawa makada wa CCM katika makundi mawili, moja likitaka kura ya maoni juu ya Katiba ifanywe kabla ya uchaguzi mkuu ujao huku jingine likitaka ifanyike baada ya Uchaguzi Mkuu.

Kundi linalopinga linataka kuheshimiwa kwa mazungumzo kati ya Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) waliokubaliana kura za maoni zifanyike mwaka 2016.

Katika kikao hicho kilichofanyika mwezi uliopita, Rais Kikwete na wapinzani walikubaliana Bunge la Katiba liishie Oktoba 4 mwaka huu, na Rasimu ya Katiba isipelekwe kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni.

Ilipendekezwa kwenye kikao hicho yafanyike marekebisho katika katiba ya sasa ili kuingiza vipengele vya tume huru ya uchaguzi, mgombea binafsi, matokeo ya Rais kupingwa mahakamani na mshindi wa urais kupata kura zaidi ya asilimia 50.

Kwa makubaliano hayo, mchakato wa kura ya maoni kama utakuwepo, utaamriwa na rais ajaye ikiwa atataka kuanzia pale mchakato huo ulipoishia au kuanzia pale ilipoishia Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Uamuzi huo ulikuwa pigo kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, aliyetutumua kuwa Oktoba 31 mwaka huu wangemkabidhi Rais Kikwete katiba inayopendekezwa.

Hata hivyo, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa baadhi ya vigogo wa CCM akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anayetajwa kutaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani, wanataka kura za maoni zifanyike chini ya utawala wa sasa.

Inadaiwa kundi hilo linataka jambo hilo lifanyike sasa ili rais ajaye asibebeshwe mzigo ambao hakuuanzisha.

Kauli kama hiyo ilitolewa na Pinda siku ya kuvunjwa Bunge akisema angependa mchakato wa kura za maoni ufanywe pamoja na uchaguzi mkuu wa mwakani.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wamelidokezwa Tanzania Daima Jumapili kuwa kauli ya Pinda ni sawa na kumshauri Rais Kikwete, atupilie mbali makubaliano yake na vyama vya siasa

Ushauri huo umezua maswali mengi kuhusu ajenda iliyo nyuma yake, na kwamba utamuathiri zaidi Rais Kikwete iwapo ataukubali.

Inaelezwa kama Rais Kikwete akiukubali ataonekana ataonekana ni asiye na msimamo katika mambo ya msingi, anayeweza kubadilika kwa ushauri kinzani wa wasaidizi wake.

Katika hatua ya kushangaza, katika salamu zake kwa wajumbe muda mfupi kabla Bunge halijavunjwa, Pinda alisema angependa kuona mchakato huo unakamilika kabla Rais Kikwete hajaondoka.

“Maana unaweza kuachia jambo hili kwa nia njema tu lakini wengine wakafikiri umeliacha ili kuendeleza vurugu. Tujitahidi kuona kama hili jambo litakwenda hadi mwisho.

“Nashauri hata kama ikiwezekana kwenda kwenye uchaguzi mkuu mwaka kesho tukiwa na kura mbili za kumtafuta Rais na ile ya maoni ya katiba bora tulimalize,” alisema Pinda.

Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa ndani ya CCM kuna makundi mawili ambayo yanasigana kuhusu mchakato huo ama umalizwe na Kikwete mwenyewe au ungoje Rais ajaye.

Duru za kisiasa zinasema kuwa kwa jinsi mchakato huo ulivyovurugwa hasa na Bunge Maalumu chini ya Sitta, hakuna Rais ajaye anayeweza kukubali katiba inayopendekezwa iende kwa wananchi kupigiwa kura wakati inaonekana dhahiri imetawaliwa na mizengwe na imekataliwa tangu ikiwa bungeni.

“Hoja hii ya Pinda ndio mtazamo wa wagombea urais wengi ndani ya CCM wanavyotaka Rais Kikwete abebe msalaba wake kwa kumaliza mchakato wake aliyouasisi kuliko kuja kumbebesha mrithi wake,”kilisema chanzo chetu.

Kundi linalounga mkono kura za maoni kufanyika mwaka 2016, lina imani Rais ajaye atakuwa amepata fundisho kubwa kupitia mchakato wa sasa na hivyo atataka kwanza yafanyike maridhiano ya kuamua suala la muundo wa muungano.

Msigiano wa pande hizo mbili umezua mpasuko mpya unaonekana kulenga urais wa mwaka 2015.




Takwimu zaleta utata

Takwimu za kukinzana zilizotolewa na Sitta kuhusu idadi ya wajumbe wa Bunge hilo waliotakiwa kupiga kura ya kupitisha rasimu ya katiba inayopendekezwa, zimevuruga ukokotoaji wa theluthi mbili na hivyo kuibua tuhuma za uchakachuaji.

Muda mfupi kabla ya upigaji kura kuanza, Sitta alilieleza Bunge kuwa idadi ya wajumbe ilikuwa 630 lakini baada ya kifo cha mjumbe, Shida Salum, wamebaki 629 ambapo kati yao 130 ni wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliosusia.

Kwa mujibu wa Sitta, katika idadi hiyo wajumbe wa Bara ni 419 na Zanzibar ni 210, na kwamba ili kupata theluthi mbili ya kura za Bara lazima wawe na wajumbe 280 wanaunga mkono wakati kwa Zanzibar wanatakiwa wajumbe 140.

Hizi ndizo takwimu walizokuwa wakitumia wajumbe wa Ukawa kukokotoa theluthi mbili ya Zanzibar na kujiridhisha kwamba kwa idadi ya wajumbe 67 walionao Zanzibar, rasimu ya katiba inayopendekezwa isingepitishwa.

Wajumbe 67 wa Ukawa kutoka Zanzibar wakijumlishwa na wajumbe saba wa kundi la 201 kutoka Zanzibar waliopiga kura ya ‘hapana’ wanafikia 74 na ukiongeza wajumbe watatu yaani Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Abdallah Abas na Ali Omar Juma waliopiga kura za hapana katika ibara nyingi kura za hapana zingefika 77.

Kwa maana hiyo, Ukawa walichukua 210 wakatoa 74 wakapata 136, idadi ambayo haikidhi akidi au 133 ukitoa kwa wajumbe 77, na hivyo wakajihalalishia ushindi bila kutegemea majaaliwa ya wajumbe waliopiga kura za siri kama kungetokea ambao wangepiga ‘hapana’.

Lakini katika hatua ya kushangaza, siku ya kutangaza matokeo takwimu hizo zilibadilika, ambapo, Naibu Katibu wa Bunge Maalum, Dk. Thomas Kashililah, alisema idadi ya wajumbe ni 630, wajumbe 219 ni kutoka Zanzibar na Bara ni 411.

Kwamba kati ya hao, waliopiga kura kwa upande wa Zanzibar ni 154 na ili kupata theluthi mbili ya huko zilihitajika kura za wajumbe 146 wakati theluthi mbili kwa upande wa Bara ilitakiwa kuwa wajumbe 274.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, tayari hesabu ya Ukawa ilikuwa imevurugika kwani taarifa za Bunge zilisema kuwa wajumbe wote 31 wa Zanzibar waliopiga kura ya siri, walipiga ‘ndiyo’.

Dk. Kashililah alisema kuwa theluthi mbili ya Zanzibar ilipatikana kwa ibara zote 289 ambapo ilikuwa ikibadilika kati ya 146, 147 na 148 wakati kwa upande wa Bara theluthi mbili ilikuwa ikibadilika kuanzia 332, 333 na 334 kutegemeana na ibara.

“Kwa upande wa Zanzibar, wajumbe waliopiga kura za ndiyo za wazi ni kati ya 106 hadi 108, wajumbe kati ya 7 hadi 8 walipiga kura za hapana za wazi wakati kura za siri zilikuwa kati ya 38 hadi 40 ambazo zote zilikuwa za ndiyo isipokuwa moja tu ilikuwa ya hapana katika baadhi ya ibara,” alisema.

Kwa Bara, kura za ndiyo za wazi zilikuwa kati ya 301 na 304, kura ya wazi ya hapana ilikuwa kati ya moja na tatu. Kura za siri za ndiyo zilikuwa kati ya 29 na 31 wakati kura za siri za hapana zilikuwa kati ya moja na mbili.

Hali hiyo ndiyo imeacha maswali mengi kuhusiana na upatikanaji wa theluthi mbili ya Zanzibar hasa baada ya baadhi ya wajumbe kudai kurubuniwa kwa fedha ili wapige kura ya ndiyo.

Sitta aliongeza utata pale alipolitangazia Bunge wakati kura zikiendelea kuhesabiwa kuwa wajumbe wawili wa Ukawa kutoka Zanzibar walikubali kupiga kura ya ndiyo wakati awali alishasema kuwa kura za Ukawa zingehesabika kama za hapana kwasababu hawakushiriki mchakato huo.

Uamuzi wa Sitta uliwashtua hata wajumbe wa CCM ambao baadhi walihoji inawezekanaje mjumbe ambaye hakushiriki mijadala kwa makusudi aruhusiwe kupiga kura, tena akiwa nje ya Bunge.

Sitta alitamba akisema kuwa, “baada ya tangazo langu kwamba wale wote walioko nje watapiga kura, wajumbe wawili ambao walikuwa kwenye ule mgomo wa kile kiukundi cha Ukawa wameisoma katiba inayopendekezwa wakaona ni kitu cha kizalendo kuipigia kura.”

Sitta alisema kuwa wajumbe hao ambao ni kutoka Zanzibar, na mmoja wao yuko radhi kufukuzwa hata uanachama wa chama chake baada ya kupiga kura, ingawa hawakuwa katika orodha ya wale waliotangazwa kuwa walipata ruhusa ya mwenyekiti kupiga kura wakiwa nje ya Bunge kwa sababu maalumu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU
KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU

TANGAZO LA KAZI -Commited youth agricultural organisation CYAO is looking for a person who is specialised in agriculture

POSITION DESRIPTION;

Agricultural Technician

Qualifications

Diploma in agriculture

Mode of application applicant must send an updated Cv,birth cirtificate,one recent passport size, an accademic cirtificate, age limit 20 to 35

apply to Project cordinator,Commited youth agriculture organisation,P.O.Box 78438 Dar es salaam or you can call through +255657990920/+255754823728