Arusha. Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) hakitarejesha serikalini viwanja vyote vya soka nchini kinavyosimamia badala amewataka wanaoleta hoja hiyo kujenga viwanja vyao.
Nkamia alisema hayo wakati akihojiwa na waandishi wa habari katika ziara yake ya kikazi jijini Arusha, ambapo aliulizwa kuhusu uchakavu wa viwanja nchini vinavyosimamiwa na CCM na kwa nini visirudishwe serikalini.
Akijibu swali hilo Nkamia alisema kamwe CCM haiwezi kuvirudisha viwanja hivyo mikononi mwa serikali na endapo vyama vya siasa vya upinzani vina hoja hiyo basi vijenge viwanja vyao.
“Wapinzani kama wanaona viwanja vya CCM havifai basi wajenge vya kwao ,CCM haiwezi kurudisha viwanja hivyo mikononi mwa Serikali, ”alisema Nkamia Nkamia alisema Serikali imeanza kuweka mikakati ya kuviboresha viwanja hivyo huku akivitaja baadhi kuwa ni Uwanja wa Sokoine uliopo jijini Mbeya, Mkwakwani uliopo Tanga, CCM Kirumba Mwanza, Kambarage Shinyanga na Sheikh Amri Abeid uliopo Arusha.
Wakati huo huo, Nkamia alizungumzia mvutano uliopo ndani ya chama cha riadha nchini na kusema kuwa endapo maji yakizidi unga wao kama wasimamizi wa vyama vyote watalazimika kuingilia kati.
Naibu waziri huyo alidai kwamba wao kama Serikali hawajapokea malalamiko rasmi kuhusu mvutano huo zaidi ya kusikia kupitia vyombo vya habari.
23 Septemba 2014
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni