Dar es Salaam. Kiwango cha juu kilichoonyeshwa na mshambuliaji Genilson Santos ‘Jaja’ kimefanya uongozi wa Yanga, kutupilia mbali wazo la kumshitaki Emmanuel Okwi kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa( Fifa).
Tangu aliposajiliwa na Yanga, Jaja ameonyesha kiwango cha juu cha ufungaji mabao akiwa amefunga mabao manne katika mechi sita alizocheza hadi sasa katika michuano mbalimbali.
Jaja aliwasahaulisha Wanayanga kabisa habari za Okwi wakati alipofunga mabao mawili ya ufundi wa hali ya juu katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam walioshinda 3-0.
Kwa mujibu wa taarifa ilizolifikia gazeti hili, zinasema kikao kilichofanyika wiki iliyopita kati ya wanasheria na baadhi ya wanachama wa Yanga wamemshauri mwenyekiti wao Yusuf Manji kuachana na jambo hilo kwa sasa.
“Ni ukweli ulio wazi hakuna mwanachama yeyote wa Yanga anayetaka Okwi arudi; kutaka kwenda Fifa ni kupoteza muda na fedha nyingi ambazo zingeweza kufanya vitu vingine vya maana. Okwi mwenyewe amekwisha, hizo Dola 60,000 alizochukua ni sadaka tumempa,” alisema mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye hakupenda kutajwa jina.
Wakili wa Yanga, Sam Mapande alipoulizwa kuhusiaana na suala hilo alisema “Ni kama limeisha siwezi kulizungumza kwa undani Katibu Mkuu Beno Njovu ndiyo mwenye mamlaka ya kufanya hivyo.”
Naye Benno Njovu alipotafutwa kuhisana na suala hilo alisema “Unajua haya mambo ni ya kimahakama sasa kama kitu kipo mahakamani siwezi kukizungumzia.”
Alipoulizwa iwapo wameacha kwenda Fifa na badala yake wamekimbilia mahakamani, Njovu alisema, “Hata huko Fifa ni mtindo wa mahakama, nisingependa kuongelea kitu kilichopo mahakamani.”
Mwanzoni mwa mwezi huu, TFF kupitia kwa Kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji chini ya Richard Sinamtwa ilimuidhinisha Okwi kuwa ni mchezaji huru na ana uwezo wa kujiunga na timu yoyote baada ya kubaini Yanga ilikiuka makubaliano ya mkataba na ilikuwa na lengo ya kumkomoa mchezaji.
Yanga iliingia kwenye mgogoro na mshambualiji huyo baada ya kushindwa kumtimizia mahitaji yake ya kimkataba ikiwa ni kummalizia deni lake la Dola 50,000 za usajili, nyumba na bima.
24 Septemba 2014
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni