Dar/Mikoani.
Jeshi la Polisi jana liliendelea kumwaga askari wake mitaani katika mikoa mbalimbali kudhibiti maandamano ya Chadema yaliyokuwa yametangazwa kufanyika nchi nzima.
Pamoja na kwamba juzi chama hicho kilisisitiza kufanya maandamano hayo, polisi waliyadhibiti maeneo yote yaliyotajwa na hadi jana jioni hakukuwa na dalili kuwa wafuasi hao wa Chadema wangejitokeza kuandamana kupinga kile walichoeleza ni kuendelea kwa vikao vya Bunge la Katiba baada ya kukubaliana visitishwe.
Tangu wiki iliyopita, polisi walijipanga kuzuia maandamano hayo ambayo tayari walikuwa wameyapiga marufuku tangu yalipotangazwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika hivi karibuni.
Dodoma Polisi waliimarisha ulinzi katika barabara zote zinazoingia na kutoka kwenye majengo ya Bunge huku Barabara ya Dodoma - Dar inayopita nje ya Bunge ikifungwa kwa muda kama ilivyokuwa Alhamisi iliyopita.
Wanachama na wafuasi wa Chadema wa Mjini Dodoma walitarajiwa kuandamana kuelekea bungeni.
Polisi walitanda barabara zote zinazoingia maeneo ya Bunge ikiwamo ile inayoanzia Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) hadi Hoteli ya Fifty Six ambako kila aliyepita katika barabara hiyo alihojiwa.
Polisi walimwagwa pia katika barabara inayoelekea Chuo cha Ufundi (Veta) na ile inayopita lango la kuingilia bungeni kwa viongozi wakuu wa Serikali akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Barabara ya Dodoma - Dar es Salaam inayopita nje ya Bunge, ilifungwa saa 3:00 asubuhi hadi Bunge lilipoahirishwa saa 6:00 mchana ndipo magari yaliporuhusiwa kupita.
Hata hivyo, ulinzi huo haukuwa mkali kulinganisha na ule uliokuwapo Septemba 18 na 19 ambako askari wa kikosi cha mbwa na farasi nao walishiriki katika ulinzi huo.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Dodoma, Jella Mambo alipoulizwa jana kuhusu maandamano hayo alisema hawakuwa wamepanga kuandamana jana, bali walikuwa wanaendelea na vikao vya kimkakati.
23 Septemba 2014
Chadema wakacha kuandamana, Polisi watanda
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni