20 Novemba 2014

Licha ya kupata mwekezaji; Usafirishaji mizigo waporomoka kutoka tani 1.4 milioni hadi 200,000

Baada ya Sekta Binafsi kuendesha sekta ya reli pasi na mafanikio ya kuridhisha, mwaka 2011, Serikali iliamua kutengua rasmi mkataba wake na Kampuni ya Reli ya India ya Rites.
Rites, iliyokuwa imefanya biashara kwa takriban miaka minne, haikuwa na jipya baada kushindwa kuongeza ufanisi wa Shirika la Reli nchini badala yake kuchangia kushusha kiwango cha usafirishaji mizigo kutoka tani milioni 1.4 hadi tani 200,000 mwaka 2012.
Hatua ya awali ya Serikali kuipa Rites usimamizi wa reli hiyo ya kati ilitokana na msukumo wa kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji kwa kubinafsisha huduma ya reli na wengi wakiwa na matumaini. Katika ubinafsishaji huo ulioanzisha Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Serikali ilikuwa na umiliki wa hisa asilimia 49. Baada ya Rites kushindwa kazi, Serikali iliamua kuirudisha kampuni hiyo chini yake na kuiwekea mikakati madhubuti ya kuiimarisha ikiwamo kuiweka sekta hiyo katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Miaka mitatu baadaye, sekta binafsi nchini inaamka na kutaka kushirikishwa tena kikamilifu. Safari hii kukiwa na maonyo mbalimbali ya kutaka rushwa isitawale katika harakati za kutafuta wabia wa kushirikiana na Serikali katika uendeshaji wa reli.
Kwa sasa, TRL bado inachechemea licha ya kwamba mikakati ya kuiinua imeanza ikiwamo ya kuongeza mabehewa na vichwa vya treni vya abiria na mizigo. Kwa mujibu wa mtalaamu wa kampuni hiyo, Mhandisi Richard Lawuo hadi ifikapo mwaka 2015 wamekadiria kusafirisha mizigo ya tani milioni 3.
Lawuo, ambaye pia kaimu mkuu wa mipango na usimamizi wa TRL, anasema kati ya mzigo huo, tani milioni 1.7 zinatarajiwa kuwa mizigo itokanayo na sekta ya madini na tani 1.3 ni bidhaa zisizo za madini kama mafuta, magari na mingineyo.
“Kupitia BRN tunatarajia kuongeza hadi kasi ya treni zetu kutoka mwendo wa kasi wa sasa wa kilomita 7.4 kwa saa hadi mwendo wa kilomita 20 kwa saa.
“Tumeshaunda upya vichwa nane vya treni na vingine 13 vinatarajia kuingizwa nchini mwanzo mwa mwaka 2015. Tunatarajia ufanisi kuongezeka mara dufu,” anasema Lawuo. Licha ya jitihada za kuboresha sekta hiyo, Serikali bado inaonekana kusuasua kufanya ubia na sekta binafsi kikamilifu.
Hali hiyo huenda inatokana na historia ya ‘kuumwa na nyoka’ baada ya sakata la Rites, hivyo msukumo wa sekta binafsi ni jambo jingine linaloigusa na kuigofya.
“Serikali ilifanya makosa makubwa wakati wa kumchagua mwekezaji wa Kihindi,” anasema Godfrey Simbeye, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF);
“Chaguo la mwekezaji lilikuwa baya na mchakato ule ulitawaliwa na mizengwe na rushwa… Ndiyo maana yale yalitokea. Kwa sasa tunahitaji mchakato wa wazi na wa ushindani kuwapata wabia katika sekta ya reli.”
Simbeye anasema umefika wakati wa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika usafirishaji wa kutumia reli, na hata kuwekeza kujenga reli ya kisasa.
“Sisi tunajua mahali pa kutafuta pesa kupitia masoko ya fedha…wao wanazunguka dunia nzima kutafuta kiasi cha kuwekeza…Wakati mambo yanawezekana kufanywa na sekta binasfi hapa hapa nchini,” anaongeza Simbeye.
Ufanisi na utendaji bora wa ubia baina ya serikali na sekta binafsi katika sekta ya reli utabaki imara iwapo mwekezaji husika anatambua vizuri asili na mazingira ya kufanyia biashara kama anavyobainisha Wamuka Mwamuka, mtendaji wa biashara wa kampuni ya reli ya Afrika Kusini ya Grindrod.
Anasema kabla ya kuruhusu kampuni yoyote binafsi kutia fedha zake kwa ajili ya uwekezaji ni lazima ichunguzwe kama ina uwezo mzuri na inafahamu mazingira ya kufanyia biashara ya Afrika.
Mwamuka anabainisha kuwa wana uzoefu wa kufanya ubia na nchi nyingi barani Afrika na kwamba sekta binafsi nchini inatakiwa ijitose haraka katika kuendesha reli ili kukuza uchumi baadala ya kusubiria Serikali ifanye kila kitu.
Japo wadau wa sekta binafsi wanaweka ushawishi mkubwa kupatiwa sehemu ya majukumu ya kuendeleza sekta ya reli, wataalamu wa uchumi na biashara wanaonya kuwa lazima ufanyike upembuzi wa kutosha kabla ya kushirikisha sekta binafsi.
“Kwa bahati mbaya kila tulipojaribu kushirikisha sekta binafsi, hasa katika sekta za uchukuzi za reli na ndege, hatukufanikiwa sana,” anasema Profesa Humphrey Moshi wa Idara ya Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM),
“Lazima tuwe makini katika uwekezaji wa aina hii kwa sababu karibu dunia nzima uendeshaji wa sekta ya reli ni nyeti sana. Haitakiwi kukurupuka kuishirikisha sekta binafsi… Kuna baadhi ya nchi kubwa kama Uingereza nao walishindwa kubinafsisha sekta nzima.”
Profesa Moshi anasema Serikali iendelee kushikilia sehemu muhimu ya miundombinu na kampuni binafsi zinunue tu mabehewa na vichwa. Hii ni kwa sababu ya bahati mbaya iliyotokea hapo awali inayohusiana pia na udhaifu katika mchakato wa kuingia mikataba.
Kuhusu muda gani serikali inahitaji kutibu vidonda vya kushindwa kwa sekta binafsi kwenye baadhi ya sekta nchini, ikiwamo reli, profesa huyo anasema hilo siyo suala la muda bali ni kujipanga. “Tunaweza kukodisha wataalamu wa sheria, uchumi na masuala ya reli ambao wanaweza kusaidiana na serikali katika kuandaa mikataba yenye maslahi makubwa kwa taifa na kuimarisha ubia na sekta binafsi nchini,” anaongeza Profesa Moshi.
Hata hivyo, mkurugenzi wa mipango wa Wizara ya Uchukuzi, Gabriel Migire anasema Serikali haina kinyongo na sekta binafsi kushiriki katika uendelezaji wa reli na ndiyo maana inaandaa miundombinu ya kutosha.
“Tunazidi kuwekeza zaidi kwenye reli ili tupunguze gharama za uwekezaji. Tunaendelea kununua vichwa na mabehewa ili kuhakikisha tunaongeza idadi ya tani tunazosafirisha kwa mwaka,” anasema Migire.
Kuonyesha kuwa sekta binafsi inahusishwa sana katika sekta hiyo, Migire anasema hadi sasa kuna kampuni kama Bakhresa Group ambayo inamiliki mabehewa yake yanayosafirisha mizigo kwa njia ya reli. Pia, Wiki iliyopita Waziri wa uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe aliainisha bungeni ununuzi mbalimbali wa vichwa na mabehewa ya treni na alisema wamenunua mabehewa mapya ya mizigo ambayo yanaanza kuwasili nchini mwezi huu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU
KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU

TANGAZO LA KAZI -Commited youth agricultural organisation CYAO is looking for a person who is specialised in agriculture

POSITION DESRIPTION;

Agricultural Technician

Qualifications

Diploma in agriculture

Mode of application applicant must send an updated Cv,birth cirtificate,one recent passport size, an accademic cirtificate, age limit 20 to 35

apply to Project cordinator,Commited youth agriculture organisation,P.O.Box 78438 Dar es salaam or you can call through +255657990920/+255754823728