29 Novemba 2014

'Waliochukua fedha za Escrow wachukuliwe hatua’

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema kuwa fedha zote zilizopotea kutokana na ukwepaji wa kodi zaidi ya Sh26 bilioni kwenye sakata la escrow zitarudishwa na waliohusika watachukuliwa hatua.
Pia, amemtaka kila mtu aliyepata mgawa wa fedha hizo kuhakikisha analipa kodi ya mapato ya kiasi alichopokea kabla ya Desemba 31, 2014 huku akipendekeza mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), aliyekosea kuandika kodi sahihi kufukuzwa kazi.
Akichangia taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kutokana na matokeo ya ukaguzi maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) bungeni jana, Mwigulu alisema kuwa iwapo kodi hizo zingekatwa kwenye chanzo kilichotakiwa mambo yasingefika yalipo sasa.
Mwigulu alisema kuwa baada ya kugundua kwamba kuna kodi ya wananchi haijakusanywa, TRA ilichukua hatua na kupata Sh4.12 bilioni na kwamba fedha hizo zimeshalipwa.
“TRA inaendelea na utaratibu kuhakikisha kuwa hela hiyo inalipwa na mimi niwahakikishie kuwa hela hiyo italipwa. Kodi iliyosalia lazima italipwa. Hatuwezi tukawa na mahitaji mengi namna hii, halafu ikatokea tukaacha kukusanya kodi,” alisema Mwigulu.
Alisema Serikali haiwezi kuacha kodi kubwa namna hiyo kwa tajiri, halafu ikakimbizana na mama mjane anayeuza mchicha barabarani na kwamba kila anayehusika ajiandae kisaikolojia.
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, alisema kwamba taifa litalipwa kodi iliyopotea kutokana na kukosewa kwa hesabu na kwamba tayari TRA imeshachukua hatua za kuhakikisha fedha hizo zinarudishwa serikalini.
“Kuna mtu alipewa kazi yake, badala ya kuandika Dola za Marekani 6 milioni, msomi aliyesoma kwa kodi za Watanzania waliojinyima yeye akaenda shule akaandika Sh6 milioni.
Ili kuandika Dola za Marekani 20 milioni, msomi aliyesoma kwa kodi za Watanzania akaandika Sh20 milioni,” alisema naibu waziri huyo, huku akishangiliwa na wabunge:
“Namwagiza Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, kwanza achukue hatua za kinidhamu za ndani kwa waliohusika na kwenye hili hakuna uchunguzi juu ya uchunguzi.
Uchunguzi umeshafanyika, ameandika Sh20 milioni badala ya Dola za Marekani 20 milioni, Tanzania imekosa kodi… Hii huwezi kusema amekosea; ni makusudi. Naagiza wafuate taratibu za ndani za TRA, lakini na yeye atafute kazi nyingine,” alielekeza.
Mwigulu alisema kuwa kwa kukosekana kodi hiyo kuna watu waliopoteza maisha kwa kukosekana dawa hospitalini na watoto wa maskini waliokuwa wamefaulu kukosa mkopo wa kwenda vyuo vikuu.
Hata hivyo, Mwigulu alisema kwamba haitoshi kwa wahusika kuachishwa kazi pekee yake kwa kuwa kufanya hivyo ni kuwapa likizo ya kwenda kuzitumia fedha walizoiba.
Kuhusu watu waliotajwa kupata mgawo wa fedha hizo, Mwigulu aliitaka TRA kuwachukulia hatua iwapo watashindwa kulipa kodi ya fedha hizo hadi mwishoni mwa Desemba.
“Huu ni utaratibu wa kawaida wa kisheria, siyo mimi niliyetunga. Nipo hapa kuzitekeleza, Mamlaka ya Mapato kama mtu hajalipa hadi Desemba 31, wamfuatilie alipe,” alisema.
Kuhusu kubeba fedha kwenye magunia
Mwigulu alisema fedha zilichukuliwa kwenye benki kwa kufuata utaratibu, lakini akawataka wakurugenzi watendaji wa benki zilizotajwa kutoa taarifa kuhusu tukio hilo.
“Utaratibu wa kibenki, mtu haruhusiwi kubeba kwenye magunia, nataka wakurugenzi watendaji watoe matamko leo (jana), walitoa fedha kwa magunia au kwa namna ya taratibu za kawaida? Na Gavana wa Benki Kuu alisimamie hilo,” alisema.
Wakati Mwigulu akitoa maelekezo hayo, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisimama na kulitaarifa Bunge kuwa mfanyakazi wa Benki ya Stanbic aliyefungua akaunti ya PAP iliyopokea fedha za escrow, amefukuzwa kazi na kurudishwa kwao nchini Uganda.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU
KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU

TANGAZO LA KAZI -Commited youth agricultural organisation CYAO is looking for a person who is specialised in agriculture

POSITION DESRIPTION;

Agricultural Technician

Qualifications

Diploma in agriculture

Mode of application applicant must send an updated Cv,birth cirtificate,one recent passport size, an accademic cirtificate, age limit 20 to 35

apply to Project cordinator,Commited youth agriculture organisation,P.O.Box 78438 Dar es salaam or you can call through +255657990920/+255754823728