Wakizungumza na wanahabari kituoni hapo, wagonjwa hao walidai kuwa Mganga Mkuu wa kituo hicho, Fred Nyangosie aliwapiga wagonjwa na jamaa zao akiwataka wafanye usafi, huku wengine wakiwa ni wagonjwa wasiojiweza.
Mmoja wa wagonjwa hao, Ester Bonifasi aliyekuwa akipata matibabu katika kituo hicho, alisema kituoni hapo kuna utaratibu wa kuzuia wagonjwa kulia chakula wodini, hivyo walipokutwa wakikiuka utaratibu huo walianza kupigwa na mganga huyo.
Alisema mganga na wafanyakazi walianza kuwaburuta waliokuwa ndani ya wodi za wagonjwa na kuamriwa kufanya usafi, huku waliokuwa wakizubaa kutafuta zana za kufanyia usafi huo, walikuwa wakipigwa na watu kukimbia ovyo.
Aidha kijana Samweli Gwassa alisema yeye alikamatwa na mganga huyo na kumfungia kwenye chumba maalumu kilichojulikana kuwa ni mahabusu alipokuwa akiegesha baiskeli yake pembeni ili akachukue kwanja.
Mganga Mkuu wa kituo hicho, Fred Nyangosie hakutaka kutoa maelezo ya chanzo cha kuwapiga wagonjwa na jamaa zao bali alidai kuwa ili aweze kuongea lazima awe na kibali kutoka kwa mwajiri wake.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Colnery Ngudungi alisema Kamati ya Afya ya Wilaya itakaa na kujadili changamoto za kituo hicho na uamuzi utakaotolewa atawajulisha wananchi na utoaji huduma unaendelea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni