Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imesisitiza kuwa fedha zilizochukuliwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow Sh306 bilioni ni za umma na waliohusika katika sakata hilo wachukuliwe hatua kali na za kinidhamu.
Akihitimisha mjadala huo uliochangiwa na wabunge 35 na wawili kwa njia ya maandishi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe alisema fedha hizo ni mali ya umma na hilo limethibitishwa na ofisi nyeti za Serikali.
Zitto alizitaja ofisi hizo kuwa ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“CAG, Takukuru na TRA kwa viapo ambavyo hawatahojiwa sehemu yoyote, walikubali kwamba fedha hizo ni za wananchi, sasa anayesimama na kupinga anatoa wapi mamlaka hayo.”
“Lakini huyu Profesa Muhongo alipoingia katika wizara hii, alikuta Tanesco wanapata hasara ya Sh43 bilioni kwa mwaka, lakini Desemba 2012 walipata hasara ya Sh117 bilioni na mwaka 2013 walipata hasara Sh467 bilioni, hii inaonyesha miaka mitatu imepata hasara mara nne zaidi na huyu ndiyo Profesa Muhongo,” alisema Zitto.
Filikunjombe
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema swali la kwanza ambalo CAG aliulizwa na kamati hiyo kuwa fedha hizo ni za nani?
“Ndiyo maana sisi tulimuuliza na CAG hakupindisha na alikuwa msafi kwa hili kuwa fedha ni za umma. “CAG, Takukuru, TRA wote hawa ni watendaji wa Serikali na wamekiri kuwa ni fedha za umma, sasa nashangaa hapa mtu anasimama na kupinga,” alisema Filikunjombe ambaye pia ni Mbunge wa Ludewa (CCM).
Alisema kwa miaka 11 Tanesco walikuwa wakisema fedha ni za kwao, lakini mwaka wa 12 kikao kimoja pekee wakasema fedha siyo za kwao, hapo hakuna ukweli wowote.
“Kamati ya PAC siyo ya Zitto, siyo kamati ya upinzani ni kamati yetu sote... tumewaonea watu wengi sana na mimi nikipitapita huko magari ya Tanesco yote yana namba SU sasa sijui fedha zao ni mali ya nani,” alihoji Filikunjombe.
Dk Kigwangalla
Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamisi Kigwangalla alisema ukubwa wa Bunge katika Bunge hilo wakati tunafanya uamuzi, CCM watatawala na kila kitu kutokana na wingi lakini hilo tutalifikia endapo tutaweka mbele na kuthamini ukubwa wa Bunge hili.
Huku akitumia hadithi, Dk Kigwangalla alisema, “Unakuwa na watu wakisafiri katika ziwa au bahari halafu wanapofika katikati ya safari, mtu mmoja anaanza kutoboa boti kitu watakachokifanya hawa watamchukua huyo anayetoboa na kumtupia majini ili kama anapenda kuchezea maji akachezee.”
“Kama tutamwacha huyu atoboe na tuzame kweli itanibidi nitafakari sana uanachama wangu ndani ya CCM,” alisema.
Dk Kigwangalla akitumia hadithi hiyo alisema, “Mapendekezo tuliyoyafikisha mbele yafanyiwe kazi...ripoti yote ya Muhongo ni uongo na amedhihirisha hilo kwa nyakati tofauti tofauti ndani ya Bunge hili, sijawahi kuona Profesa muongo kama huyu na hawa ndiyo viongozi wetu.”
Mpina
Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhanga Mpina alisema, “Tuna Profesa (Mhongo) ambaye ni muongo kupita kiasa na ukiwa na kiongozi muongo namna hii katika taasisi hii nyeti ni hatari sana.”
“Tumefika hatua hadi taifa linapoteza mwelekeo hadi taifa linapoteza Sh321 bilioni, ni hatari na dunia nzima kuona tutashughulikiaje suala hili na tutakavyofanya,” alisema Mpina.
Kuhusu michango ya wabunge wa CCM katika mjadala huo alisema, “Mimi nilichaguliwa na ofisi ya Spika kwenda kuongeza nguvu lakini jana (juzi) nilianza kuchanganyikiwa baada ya wabunge wa CCM walivyokuwa wakichangia, nilisikitika.”
“Fedha zilizoibiwa ni nyingi sana lakini toka lini mwanasheria mkuu wa Serikali akawa mkusanya kodi? Hii haikubaliki na waliohusika lazima wachukuliwe hatua kama mapendekezo ya kamati yalivyowasilishwa mbele ya Bunge,” alisema Mpina.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni