Dodoma. Bunge la jamuhuri ya muungano wa Tanzania limeongeza muda wake na kusitisha vikao vyake mara mbili ili kutafuta muafaka juu ya andikaji wa maazimio yatakayotumiwa kuwawajibisha wale wote waliohusika na kashfa ya Escrow.
Hali hiyo ilijitokeza wakati spika wa bunge, Anne Makinda alipositisha bunge muda wa saa tatu asubuhi hadi saa tano asubuhi, lakini upande wa chama cha mapinduzi na serikali yake, ukaomba kuongezewa muda wa kushauriana na upande wa upinzani.
Kufuatia kuwepo kwa misiguano hiyo, spika wa bunge akapendekeza kusitisha tena kikao hicho cha bunge hadi saa 10 jioni, huku kila upande ukiteua viongozi wao, watakaotafuta muafaka, kwa lengo kufanikisha kazi iliyokuwa mbele yao ya kuandika maazimio ya bunge.
Kufikiwa kwa maamuzi hayo kunatokana mvutano mkali uliojitokeza jana usiku majira ya saa tano kasoro, baada ya kiongozi wa upinzani bungeni, Bw. Freeman Mbowe kudai kuwepo kwa njama za kuwalinda viongozi waliotuhumiwa na kashfa hiyo ya Escrow.
Kutolewa kwa kauli hizo za kukinzana, kukaleta rabsha ndani ya bunge, wabunge wa upinzani wakasimama na kuanza kuimba, na hivyo kukawa hapana budi kwa spika kulazimika kuliahirisha bunge, baada ya kutokea mpasuko katika hoja ya bunge lenyewe.
Ikumbukwe kuwa ratiba ya bunge iliyotolewa wakati wa kuanza mkutano huu wa 16 na 17 wa bunge, ilionyesha bunge lingemaliza shuguli zake Novemba 28, lakini kutokana na hoja Escrow, bunge hilo limelazimika kuendelea na vikao vyake hadi Novemba 29, mwaka huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni