Moja ya mambo ninayoyaona mara kwa mara ninapokuwa safarini, ni wakulima wakiwa barabarani wakibembeleza wapita njia, hasa wanaoendesha magari, kusimama kununua bidhaa zao.
Ni ishara kuwa kuna tatizo la kutojua soko liko wapi, maana pale walipo bidhaa hizo hazina wateja.
Pia, ni jambo la kawaida kuona bidhaa, hasa za mazao ya kilimo, zikiwa zimepangwa juani kwa muda mrefu, zikiwa hazina vifungashio vyovyote. Ni wazi kuwa hawa ni wakulima wasio na mafunzo yoyote ya uandaaji wa bidhaa za kibiashara.
Nyakati za mavuno ya mahindi, kwa mfano, ni jambo la kawaida katika maeneo ya Kabuku hadi Mkata, mkoani Tanga kuwaona vijana na vifurushi va mahindi wakisimama katikati ya barabara kuwapungia waendesha magari kusimama na kununua.
Hilo ni jambo la kawaida pia, kwa mfano, eneo la Mikumi hadi Ruaha. Vijana wanasimama na vifuko katikati ya barabara kutaka wapita njia kununua nyanya, vitunguu na bidhaa nyingine.
Najua hakuna jibu na mbinu rahisi, lakini tunapozungumzia vijana kujiingiza katika shughuli za uzalishaji za kilimo na kuwa kwa njia hiyo tutawarudisha kutoka kukimbilia mjini, ni lazima kujenga mkakati wa soko ambao wao ndio wapange bei, na siyo wao wawabembeleze wanunuzi wapandishe bei ili wapate faida japo kidogo. Hii inakuwa ni jambo lisiloweza kuwavuta wengi katika kilimo.
Inavyoonekana ni kuwa Serikali, katika ngazi mbalimbali hazijipangi mapema kufanya tafiti za masoko ya bidhaa za wakulima.
Tunawezaje kuwa na afisa biashara katika ngazi ya wilaya ambaye kazi yake ni kusubiri kukatisha leseni za biashara na kufuatilia hilo huku hana ushauri wowote kwa Serikali na wadau mbalimbali kuhusu biashara ya mazao ya wakulima.
Hivi tunahitaji tena mshauri mwingine wa halmashauri wa kutusaidia ushauri kuhusu nini tulime na namna gani tuuze bidhaa za wakulima.
Kwa nini hatujengi mfumo mchangamano ambapo wataalamu wa ngazi ya halmashauri wanakuwa watoa ushauri kitaalamu wa namna ya kuboresha mfumo wa masoko ya wakulima.
Kuna kampuni zinazosindika bidhaa za mashambani, mananasi, machungwa na kadhalika. Ningetegemea watendaji wa halmashauri wangeenda kuongea na wasindikizaji hao juu ya uwezekano wa wakulima wao kupata soko.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni