17 Novemba 2014
Meno ya tembo yawatupa wawili jela miaka 20
Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya Sh5 milioni kila mmoja watu wawili baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na meno ya tembo kinyume cha sheria.
Waliohukumiwa kifungo hicho ni Nicolaus Daud na Salum Mohammed ambao walishtakiwa baada ya kukutwa na nyara hizo za Serikali.
Washtakiwa hao watatumikia kifungo hicho baada ya Mahakama kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na mashahidi dhidi yao.
Akitoa hukumu hiyo mwishoni mwa wiki, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Hassan Juma alisema: “Mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne dhidi ya washtakiwa hawa na hivyo mahakama yangu imewatia hatiani na watatumikia kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya Sh 5 milioni,” alisema Hakimu Juma.
Alisema iwapo washitakiwa hawajaridhika na adhabu iliyotolewa mahakamani hapo wanaweza kukata rufani ya kuipinga adhabu.
Kabla ya hukumu kutolewa, washitakiwa waliiomba mahakama iwapunguzie adhabu ombi ambalo lilitupiliwa mbali.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa walitenda kosa hilo Desemba 13, mwaka 2009, katika maeneo ya Bombom wilayani Ilala walikokutwa na vipande vitano vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh1.3 milioni mali ya Serikali.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni