04 Novemba 2014

Yaone haya katika siasa yetu Tanzania

Dar/mikoani. Rais Jakaya Kikwete amesema anaomba yasimkute ya Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliyeshambuliwa katika mdahalo wa katiba uliofanyika Dar es Salaam, juzi.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo Mwanza jana katika mkutano wa 12 wa Shirikisho la Taasisi za Kupambana na Rushwa (Safac) unaojumuisha nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc).
“Naamini Katiba Inayopendekezwa itapitishwa, nina matumaini hayo. Nadhani na mimi nitakavyokuwa napiga kampeni hayatatokea yale ya jana(juzi), maana mie sioni haya kuipigia kampeni kama wale wenzetu ambao wanataka isipite,” alisema Rais Kikwete kwa ufupi.
Juzi, Jaji Warioba alishambuliwa na kundi dogo la watu walioingia katika mdahalo ulioitishwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kutolewa chini ya ulinzi.
Vurugu hizo zilitokea wakati Jaji Warioba alipokuwa akihitimisha hotuba yake kwa kuhoji watu wanaotumia vibaya jina la Mwalimu Julius Nyerere kupitisha hoja zao katika misingi isiyokubalika.
Miongoni mwa wanaotuhumiwa kumshambulia Jaji Warioba ni Katibu wa Hamasa wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM), Paul Makonda ambaye hata hivyo, jana alikana kufanya kitendo hicho.

Tukio lakemewa kila kona
Wasomi, wanasiasa na wananchi wa kada mbalimbali nchini wamelaani vurugu zilizotokea katika mdahalo huo na zaidi, kitendo cha Jaji Warioba kuvamiwa na kupigwa.
Mbali na kulaani, mjumbe wa iliyokuwa Tume hiyo, Profesa Mwesiga Baregu alimtaka Rais Kikwete kutoa tamko, huku wanaharakati na wasomi wakitaka ulinzi uimarishwe kwa viongozi wa kitaifa wakiwamo wastaafu.
Profesa Baregu alisema ni vizuri kwa Rais akatoa tamko kuhusu tukio hilo ili kunusuru mchakato mzima wa Katiba Mpya.
“Nashangaa mpaka sasa Serikali imekaa kimya licha ya kutokea kwa tukio hili la aibu kwa Taifa, ambalo unaweza ukahisi lilipangwa ili kuhatarisha usalama wa wananchi,” alisema na kuongeza:
“Jaji Warioba kwa wadhifa wake, anatakiwa kupatiwa ulinzi wa kutosha kama walivyo viongozi wengine wastaafu, lakini cha kushangaza jana (juzi) mpaka tunaanza mdahalo hakukuwa na askari hata mmoja ndani ya ukumbi, badala yake walikuwa nje ya jengo lile.”
Alisema kwa mwenendo uliopo sasa, itakuwa vigumu kupatikana Katiba Mpya kwani wananchi wanakoseshwa haki zao za msingi ikiwamo usalama.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee alilaani kitendo hicho na kuitaka Serikali kuwachukulia hatua kali waliohusika.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Nyalikungu Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Mdee alimtuhumu Makonda na wenzake kuwa wamefanya tukio ambalo limeidhalilisha nchi.
“Tunalaani vikali kilichomtokea Warioba ...nani asiyefahamu uadilifu wa Warioba? Eti wanampiga, hili hatuwezi kukubali litokee tena. Serikali iwachukulie hatua kali kwani waliofanya wanajulikana kwa nini kuwaficha au kosa la Warioba ni lipi?”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema viongozi wa kitaifa wanatakiwa kupewa ulinzi wa kutosha na kitendo kilichotokea juzi ni aibu kwa Taifa zima.
Mwenyekiti wa PPT - Maendeleo, Peter Mziray alisema viongozi wastaafu wasijihusishe kabisa na masuala ya kisiasa badala yake wapumzike kama alivyoamua Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikataa kuzungumzia lolote akisema yupo nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba la Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema vurugu hizo ni maafa na uhuni wa kutisha unaostahili kulaaniwa.
“Sitaki kuamini kuwa wale vijana wahuni walitumwa na CCM, sitaki kuamini hata kidogo… hali ile ni maafa. Ulinzi na usalama umekwisha kabisa,” alisema na kuongeza: “Hii hali ya kusubiri mpaka maafa yatokee haifai. Warioba ana mlinzi mmoja na sisi jana tulikuwapo pale ilifikia kipindi hadi walinzi wa Jukata waliingia kumsaidia Warioba, ni aibu kubwa.”
Mtafiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Patience Mlowe alisema vurugu hizo zimemshangaza kila mpenda amani na demokrasia.
“Ni fedheha kwa Taifa. Warioba ni Makamu wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, halafu vijana wanashindwa kumheshimu… hili ni janga kwa Taifa,” alisema Mlowe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU
KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU

TANGAZO LA KAZI -Commited youth agricultural organisation CYAO is looking for a person who is specialised in agriculture

POSITION DESRIPTION;

Agricultural Technician

Qualifications

Diploma in agriculture

Mode of application applicant must send an updated Cv,birth cirtificate,one recent passport size, an accademic cirtificate, age limit 20 to 35

apply to Project cordinator,Commited youth agriculture organisation,P.O.Box 78438 Dar es salaam or you can call through +255657990920/+255754823728