Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete leo atalihutubia taifa la nchi hiyo ambapo anatarajiwa kuyatolea ufafanuzi masuala nyeti yanayoligusa taifa hilo.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa na kijamii wanatabiri huenda hatua atakazozichukua dhidi mawaziri na maafisa wa serikali waliohusika na ufisadi wa mamilioni ya fedha katika akaunti ya Escrow itakuwa ni moja kati ya agenda muhimu atakayoitolea ufafanuzi.
Hotuba hiyo inakuja wakati kukiwa na shinikizo kutoka kwa baadhi ya raia na wapinzani wakitaka hatua zaidi zichukuliwe kutekeleza azimio la bunge ambalo linatataka mawaziri na maafisa wa serikali waliohusika na sakata hilo la ufisadi wawajibishwe ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.
Sakata la Akaunti ya Escrow liliibuliwa bungeni na mmoja wa wabunge wa bunge la Tanzania, David Kafulila na kusababisha mjadala mkali na kuamua Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kupewa jukumu la kuchunguza kashfa hiyo.
Baada ya uchunguzi kuwasilishwa katika mkutano wa bunge uliomalizika mwishoni mwa mwezi Novemba, kamati hiyo ilikuja na maazimio manane kuhusu taarifa ya ukaguzi maalum kuhusiana na miamala iliyofanyika katika akaunti ya Escrow ya Tegeta pamoja na umiliki wa kampuni ya IPTL.
Miongoni mwa maazimio ya bunge yaliwataja baadhi ya wanasiasa, mwanasheria mkuu, maafisa waandamizi wa serikali, majaji, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi kuhusika katika kashfa hii na hivyo kuagiza mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua za kisheria wahusika na wengine kuondolewa katika nyadhifa zao za kuteuliwa,tayari Mwanasheria mkuu wa serikali amekwisha jiuzulu na rais kukubali uamuzi huo.
Akaunti ya Escrow ilianzishwa katika Benki Kuu ya Tanzania ili kuhifadhi fedha, baada ya kuibuka kwa mvutano kati ya Shirika la Umeme la Tanzania, Tanesco na kampuni ya kufua umeme ya IPTL kuhusu ongezeko la mtaji wa uwekezaji, huku TANESCO ikilalamika kuwa gharama za kununua umeme kutoka kampuni ya IPTL zilikuwa za juu mno. Fedha hizo zingeendelea kutunzwa katika Akaunti hayo hadi wakati ambapo suluhisho la mvutano wa wabia hao wawili lingepatikana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni