Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete jana alikagua gwaride la Uhuru la vikosi vya ulinzi na usalama ambavyo baadaye vilipita mbele yake kutoa heshima ikiwa ni maadhimisho ya miaka 53 ya Uhuru wa Tanganyika.
Ikiwa hakutakuwa na mabadiliko yoyote, kiongozi huyo wa awamu ya nne wa Tanzania, anatazamiwa kustaafu kikatiba mwakani kabla ya sherehe nyingine za Uhuru Desemba 9, 2015.
Kwa kawaida uchaguzi mkuu hufanyika wikiendi ya mwisho ya Oktoba na matokeo hutangazwa siku chache baadaye. Kwa maana hiyo, hilo lilikuwa gwaride la mwisho la sherehe za Uhuru kwake akiwa mkuu wa nchi.
Mbali na hilo, wakati Rais Kikwete akifanya shughuli hiyo, macho ya Watanzania yalikuwa yameelekezwa kwake kuona jinsi anavyotekeleza jukumu hilo siku ya pili tu baada ya kutoka katika mapumziko ya upasuaji wa saratani ya tezi dume huko Marekani Novemba 8.
Kabla ya tukio hilo lililofanyika Uwanja wa Uhuru, juzi Rais Kikwete alionekana katika picha akifanya mazoezi mepesi siku 10 tu baada kurejea nchini akitokea Hospitali ya Johns Hopkins, Baltimore alikotibiwa.
Jana, Rais Kikwete alidhihirisha kuimarika kiafya baada ya kumudu kukagua gwaride hilo na baadaye mchana akasimama kwa muda mrefu akitoa nishani za heshima kwa watu mbalimbali waliolitumikia Taifa.Rais, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu alitembea kwa mwendo wa ukakamavu akiwa ameongozana na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange kukagua gwaride hilo.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi walisikika wakimshukuru Mungu kwa jinsi alivyosaidia afya ya Rais kuimarika.
“Jamani kweli Rais Kikwete sasa yupo poa anatembea kwa mwendo wa ushupavu haswaa,” alisema mkazi wa Kinondoni Juma Ramadhani.
Rais Kikwete pia alisimama kwa muda mrefu kupokea salamu za kijeshi kutoka kwa gwaride hilo.
Sherehe zafana
Rais Kikwete aliingia kwenye Uwanja wa Uhuru saa 5.08 asubuhi akiwa katika gari la wazi huku akiwa ameambatana na Jenerali Mwamunyange.
Wakati akiingia, Kikwete alikuwa akitabasamu na kuwapungia mikono wananchi waliofika kwenye uwanja huo ambao walijibu kwa kumshangilia.
Akiwa amevalia suti nyeusi, shati jeupe na tai nyekundu, Rais Kikwete alikagua gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama ambavyo ni, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Magereza, Polisi, Wanamaji, FFU na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Baada ya ukaguzi huo, vikosi hivyo vilipita kwa mwendo wa pole na wa haraka kutoa heshima kwake. Kivutio kikubwa kilikuwa kwa kikosi cha FFU ambacho askari wake walionyesha ukakamavu wa hali ya juu walipokuwa wakipita kutoa heshima zao kwa Rais na kuibua shangwe na hoihoi kutoka wa wananchi waliokuwa wamefurika uwanjani hapo.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Ali Mohamed Shein, makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Shariff Hamad, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Makamu wa Pili wa SMZ, Balozi Seif Ali Idd.
Wengine waliohudhuria ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa, Cleopa Msuya na Frederick Sumaye.
Sherehe hizo zenye kaulimbiu; “Miaka 53 ya Uhuru; ingia katika historia ya nchi yetu jitokeze kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa,” ilitumbuizwa na halaiki ya watoto 1,500 wa shule za msingi ambao walionyesha maumbo mbalimbali, kucheza sarakasi na kuimba.
Mbali na maonyesho mengine, watoto hao walipeperusha njiwa 25 angani ikiwa ni ishara ya kuonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya amani.
Pia vikundi vya ngoma za asili kutoka Kasulu, Kigoma na Kyela, Mbeya vilitumbuza.
Viongozi wakosekana
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal alikuwa miongoni mwa baadhi ya viongozi walikosekana katika sherehe hizo, wengine wakiwa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa na mawaziri wakuu wastaafu, Jaji Joseph Warioba, Salim Ahmed Salim na John Malecela.
Pia viongozi wa vyama vya siasa akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema hawakuhudhuria.
Alipoulizwa, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni alijibu kwa kifupi kwamba yuko Ujerumani na angetaka apigiwe simu baadaye. Simu za Mbatia na Lipumba ziliita bila kupokewa huku Mrema akiwa hapatikani kwenye simu yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni