Dar es Salaam. Siku moja baada ya Ikulu kueleza kuwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na kupokea ripoti kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow hawezi kuwachukulia hatua wahusika mpaka uchunguzi kuhusu suala hilo utakapokamilika, ofisi hiyo ya Rais sasa imesema atafanyia kazi uamuzi wa ripoti hiyo katika wiki moja ijayo.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alikaririwa na vyombo vya habari jana akisema: “Rais lazima aagize vyombo vya uchunguzi kufanya kazi yake na baada ya hapo ndipo atapata mahali pa kuanzia,” alisema.
Hata hivyo, taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, ilisema Rais Kikwete ambaye alianza kazi rasmi juzi, baada ya upasuaji aliofanyiwa mwezi uliopita, amekwishaanza kusoma Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Umma (PAC) na Maazimio ya Bunge kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow na atayatolea uamuzi ndani ya wiki moja ijayo.
“Katika wiki moja ijayo atazitolea uamuzi kwa maana ya kwamba yale mambo yanayomhusu yeye moja kwa moja atayatolea uamuzi yeye, yale yanayohusu Serikali atayatolea maagizo na maelekezo ya namna ya kuyashughulikia,” ilisema taarifa hiyo kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete ameelekeza kuwa Ripoti ya CAG iwekwe hadharani kwa ajili ya umma kuisoma na kujua nini hasa kimesemwa na kupendekezwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Rais Kikwete ameelekeza kuwa ripoti hiyo itangazwe kwenye magazeti yanayosomwa na watu wengi na kwenye mitandao ya kijamii, ili iweze kupatikana kwa Watanzania wengi.
Mbali na taarifa ya CAG, Bunge lilijadili na kutoa maazimio manane yaliyotokana na majadiliano ya PAC kuhusu uchunguzi huo wa CAG na ule wa Takukuru.
Maazimio ya Bunge
Baada ya mjadala wa Tegeta Escrow, Bunge liliazimia kwamba:
1. Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, watu wote waliotajwa na taarifa maalumu ya kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya akaunti ya escrow na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea.
2. Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
3. Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa 18 wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati husika za kudumu za Bunge.
4. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya kijaji ya uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania
5. Serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
6. Mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi, ziitaje Stanbic Bank (Tanzania) Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika, kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
7. Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.
8. Serikali itekeleze Azimio la Bunge la kuitaka iwasilishe mikataba husika bungeni au kwenye Kamati zake kwa lengo la kuliwezesha kutekeleza vyema wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri Serikali mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile, kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali.
Azindua jengo Ikulu
Jana, Rais Kikwete alifungua jengo la shughuli mbalimbali (multipurpose hall) la Ikulu katika moja ya shughuli zake za kwanza baada ya kuanza kazi rasmi juzi.
Sherehe ya ufunguzi wa jengo hilo lililoko upande wa kushoto wa bustani za Ikulu upande wa lango kuu, zilihudhuriwa na mawaziri, makatibu makuu na viongozi waandamizi wa Serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Baada ya kufungua jengo hilo lenye vyumba 53, Rais Kikwete alitembezwa kuona shughuli zitakazofanyika. Lina ukumbi wenye uwezo wa kubeba watu kati ya 500 na 1,000 kwa wakati mmoja.
Balozi Sefue aliyekuwa msimamizi mkuu wa ujenzi huo, alisema ukumbi huo unaweza pia kugawanywa na kuwa tatu kubwa na zote kutumika kwa wakati mmoja.
Jengo hilo ambalo gharama zake hazikutajwa, limejengwa kwa maelekezo ya Rais Kikwete aliyoyatoa Dodoma Agosti 21, 2009, wakati alipoelekeza lijengwe kwa nia ya kuongeza nafasi ya kufanyia shughuli mbalimbali Ikulu kwa kutilia maanani kuwa nafasi imekuwa finyu kwenye jengo la sasa lililojengwa mwaka 1902.
Rais alitaka uwepo ukumbi mkubwa ili kuondokana na gharama za kukodi wakati wa mikutano ya Ikulu ikiwamo ya viongozi wa nchi za nje.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni