Dar/ Singida. Jeshi la Polisi mkoani Singida, linamshikilia Nawaridi Saidi (45), mkazi wa Dar es Salaam kwa tuhuma za kumtupa mjukuu wake Mayasa Meshack (6) kutoka ndani ya gari wakati akisafiri kwenda Kigoma akitokea Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka alisema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 18, saa 2 usiku katika Kijiji cha Igugumo, wilayani Iramba ambapo mama huyo akiwa kwenye basi aina ya Scania, alifungua dirisha kutoka katika kiti alichokaa na kumtupa Mayasa wakati basi likiwa katika mwendo.
“Mama alikuwa anaenda mkoani Kigoma kwa ajili ya Sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya, aliambatana na mtoto wake mwingine ambaye jina bado halijafahamika,” alisema Kamanda Sedoyeka.
Aliongeza: “Baada ya kumtupa mtoto huyo, abiria wenzake walianza kupiga kelele, zilizomuamuru dereva kusimamisha basi na kulirudisha nyuma ili kwenda kumwokota mtoto huyo ambaye alikuwa bado hai.”
Alisema kuwa baada ya kuokotwa, mtoto huyo alipelekwa moja kwa moja katika Hospitali ya Mkoa Singida na kupokewa na Dk Adam Hussein ambaye alianza kumtibia kwa kuanza kumtoa uchafu kwenye mfumo wa kupumulia.
“Dk Hussein alimwongezea damu na kumshona majeraha, hata hivyo saa 2 asubuhi ya Desemba 19, Mayasa alifariki dunia,” alisema Kamanda Sedoyeka.
Alibainisha kuwa walimpeleka hospitali mama aliyetupa mtoto huyo kwa ajili ya kumpima akili baada ya kufanya mahojiano ya awali na baadaye atafikishwa mahakamani.
Kamanda huyo alisema kwamba katika maelezo yake, mama huyo alisema ana tatizo la kuumwa kichwa na kupoteza kumbukumbu mara kwa mara, hivyo hakumbuki kama alitenda kosa la kumtupa mtoto huyo, lakini alishtuka baada ya kupigwa na abiria waliokuwamo kwenye basi hilo.
Awali, mmoja wa abiria waliokuwamo kwenye basi hilo, Ebenezer Hans alilieleza gazeti hili kwamba mama huyo akiwa miongoni mwa abiria, alikuwa na mtoto wake mwenye umri unaokadiriwa miaka 14 na wajukuu wawili, ambao alikuwa akisafiri pamoja nao.
Alisema abiria waliokuwa jirani naye walishtuka kufuatia mmoja wa abiria kupiga kelele, baada ya kushuhudia mama huyo akifungua kioo cha dirisha taratibu na kumtupa mtoto huyo kimyakimya, wakati gari likiwa kwenye mwendo wa kasi katika eneo hilo lenye mapori mengi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni