Dar es Salaam. Wakati vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vikitafakari jina la mgombea urais, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila tayari anaye mtu anayefaa; anamtaka Dk Willbrod Slaa.
Kwa maoni yake, si kwamba viongozi au wanachama wa vyama vingine vinavyounda Ukawa hawana sifa za kuwania nafasi hiyo ya juu katika siasa nchini, bali Dk Slaa ana sifa ya ziada; ana mvuto.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Kafulila, ambaye alikuwa mwanachama wa Chadema kabla ya kuondoka na kujiunga na NCCR-Mageuzi mwaka 2010, alisema Dk Slaa ana nafasi kubwa kuliko viongozi wa vyama vingine vya siasa vinavyounda umoja huo ambavyo ni Chadema, NCCR, NLD na CUF kwa sababu katibu huyo mkuu wa Chadema anakubalika zaidi katika jamii kulinganisha na wengine.
Vyama hivyo vinne vilitia saini ya makubaliano ya ushirikiano Oktoba 27, hasa ya kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi zote, kuanzia wa Serikali za Mitaa mwaka huu na madiwani, wabunge na rais mwaka 2015.
Hata hivyo, bado kamati maalumu inatafakari jinsi ya kutekeleza makubaliano hayo ili kuzuia uwezekano wa mpango huo kuvurugika kama ilivyowahi kutokea kwenye chaguzi zilizopita.
Miongoni mwa watu wanaopewa nafasi ya kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa ni pamoja na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Dk Slaa.
“Kwa maoni yangu bado namwona Dk Slaa kuwa ni mtu ambaye ana nafasi kubwa kuliko wenzake. Kwa vyovyote itakavyokuwa yeye ndiye anawazidi wenzake kwa kukubalika,” alisema Kafulila (32) alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa na kuongeza: “Siyo kama wengine hawawezi, hapana, ila si kila mwenye mvuto anaweza kuongoza na wala si kila mwenye sifa anayeweza kuwa na mvuto. Pia si kila anayekubalika anaweza na si kila anayeweza anakubalika. Ni adimu kukuta mtu anaweza na anakubalika pia.”
Katika matokeo ya utafiti wa taasisi ya Twaweza, Dk Slaa alishika nafasi ya tatu nyuma ya waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na wa sasa, Mizengo Pinda akipewa asilimia 11 ya ushindi kulinganisha na Pinda (asilimia 12) na Lowassa (asilimia 13).
Lipumba amegombea urais mara nne, akiwa ameshika nafasi ya pili mwaka 2000 na 2005 kabla ya kushuka mwaka 2010 wakati Dk Slaa alipopata asilimia 26 za kura katika uchaguzi ambao mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete aliposhuka kwa takriban asilimia 20 ya kura alizopata mwaka 2005.
Mbowe aligombea urais mwaka 2005 na kushika nafasi ya tatu wakati James Mbatia hajawahi kugombea urais na katika siku za karibuni ameonekana kuelekeza nguvu kugombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, ambako kuna uwezekano mkubwa akapambana vikali na mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema.
Alipoulizwa kama kuna uwezekano wa mgombea wa umoja huo kuibuka na ushindi, Kafulila alisema: “Ni mapema mno kusema Ukawa inaweza kushinda. Hiyo itategemea tunajipangaje, tukifanya makosa tutashindwa vibaya. Makosa ya CCM na Ukawa yanategemeana kwenye kuamua nani agombee.”
Akizungumzia vigogo wa CCM wanaotajwa kuutaka urais kama wana uwezo wa kuchuana na Dk Slaa, Kafulila alisema mpaka sasa hajaona hata mtu mmoja mwenye uwezo na sifa za kuwa rais wa Tanzania.
“Kwenye nchi maskini kama Tanzania ambayo inakosa taasisi na mifumo imara, inatakiwa kuwa na rais mwenye sifa tatu ambazo ni weledi, uadilifu na dhamira. Nasema hivi kwa sababu katika nchi yetu sera, sheria na mifumo haijatosha kubana sehemu zote, hivyo maamuzi ya siku hadi siku ambayo rais anayafanya ndiyo yanaendesha nchi,” alisema.
Alisema rais mwenye weledi ataweza kuchambua kila ushauri anaopewa na kwamba kama nchi itakuwa na rais asiye na weledi, ni rahisi kupokea ushauri mbaya kutoka wa watu tofauti na kusisitiza kuwa hilo ndilo tatizo linalozikabili nchi nyingi barani Afrika.
“Rais mwenye weledi ataijua vyema historia ya nchi yake pamoja na majirani zake na kujua mambo ya kijamii,” alisema.
Kuhusu uadilifu alisema: “Nchi ikikosa rais mwadilifu ni sawa na kazi bure maana akiwa Ikulu anaweza kutengeneza ‘dili’ zake za kujiingizia fedha tu. Ndiyo maana nikagusia suala la mifumo yetu mibovu. Jambo hili haliwezi kutokea katika nchi zilizoendelea kwa sababu mifumo yao imebana na rais akijaribu kupiga ‘dili’ lazima atabainika”.
Kuhusu dhamira, Kafulila alisema hilo ndilo jambo la msingi zaidi kuliko uadilifu na weledi kwa maelezo kuwa rais asiye na dhamira hawezi kuleta mabadiliko yoyote.
“Katika hili mnaweza kuwa na rais ambaye si mwizi ila hasimamii mambo. Kifupi ni kuwa na rais ambaye si mwizi na ana akili nzuri tu, lakini hachukui hatua. Tunatakiwa kuwa na rais anayejua anatakiwa kufanya nini,” alisema.
Alisema sifa hiyo inakosekana kwa wagombea wa CCM na kusisitiza kuwa ni vigumu kujua wanataka nini... “Binafsi nashindwa kuwalinganisha wagombea wengine wa CCM kwa sababu wengi wanakosa vigezo vya kuwapima.”
Alisema rais bora ni yule anayejua anataka kutengeneza wananchi wa aina gani, huku akimtolea mfano Mwalimu Julius Nyerere alivyoweza kuwatengeneza Watanzania katika misingi ya uadilifu na uhusiano mzuri wa kijamii na kuwafanya kuwa tofauti na wananchi wa nchi nyingine.
“Bado tunachagua rais kwa kubahatisha kwa sababu wagombea wengi wana sifa za kubahatisha. Bado tunabahatisha katika kuchagua viongozi wetu,” alisema na kuongeza:
“Nipo Ukawa na ninatamani CCM waweke mgombea dhaifu ili Ukawa tushinde, lakini mimi pia ni Mtanzania ninatamani tupate rais mwenye uwezo wa kufanya Tanzania ifikie matamanio yake. Ikiwa lazima atoke CCM kama ulivyoniuliza, siwezi kukubali aje mwenye uwezo duni. Sijaona wa kutoka CCM.”
Akizungumzia mgogoro ulioibuka katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kutishia ushirikiano wa Ukawa kutokana na baadhi ya wagombea wa vyama vinavyounda umoja huo kujiondoa katika msingi wa makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja, Kafulila alisema katika urais jambo hilo haliwezi kutokea.
“Kwenye kugombea urais ni rahisi zaidi Ukawa kushirikiana kuliko uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa sababu serikali za vijiji ni nyingi na zina changamoto zaidi kuliko katika ngazi ya urais,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni