Shinyanga. Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Shinyanga (Shirecu), kimeiomba Serikali kupitia chama hicho, inunue tani 5,100 za pamba ambayo bado iko kwenye maghala ya wakulima kutokana na kukosa soko.
Akitoa taarifa ya kufungwa kwa msimu wa ununuzi ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, Meneja Mkuu wa Shirecu, Joseph Mihangwa alisema wamenunua kilo milioni 5.1 zenye thamani ya Sh3.825 bilioni.
Mihangwa alisema lengo lilikuwa ni kununua kilo milioni 7.5 lakini hawakufikia kutokana na wakulima kugoma kuiuza wakidai bei iko chini.
Meneja huyo alisema wakulima wengi wa pamba wanaonekana kukata tamaa kuendelea kulima zao hilo kutokana na mkanganyiko wa bei unaojitokeza kila mwaka pia na aina ya mbegu inayopaswa kutumika baada ya isiyo na manyoya kuwaingizia hasara kubwa.
“Pamba imeanza kufifia maeneo tuliyokuwa tunayategemea kwa mikoa yote ya Shinyanga, Simiyu na Geita… msimu uliopita pamba nyingi tumeipata wilaya za Kishapu, Meatu, Bariadi na Maswa pekee. Bukombe na Mbogwe hatukupata pamba ya kutosha, wakulima wameshakata tamaa hawataki kulima tena,” alisema Mihangwa.
Alisema upungufu wa pamba ulitokana na mgogoro wa mbegu baada ya Serikali kutoa waraka kutaka mbegu za Quton zisizo na manyoya zitumike. “Tumeanza kusambaza mbegu za pamba yenye manyoya kwa wakulima kwa bei ya Sh500 kwa kilo kama tulivyoelekezwa na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) badala ya Sh350, ingawa wakulima wanalalamika na kudai ni kubwa na wengine wanasusa kulilima zao hili,” alisema Mihangwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni