IKIWA imebaki miezi 10 kufikia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Askofu Mkuu
wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,
amewataka Watanzania walio masikini kuungana ili kuwang’oa madarakani
viongozi matajiri wasiojali maslahi ya taifa.
Alisema kwa muda mrefu Watanzania wanafikiria ulimwengu utabadilishwa na
watu wenye mabilioni na walio na fedha za Escrow jambo ambalo si
sahihi.
Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam juzi alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari baada ya ibada ya sherehe za kutimiza miaka 70 ya
kuzaliwa kwake iliyofanyika katika Kanisa la St. Joseph ambapo alisema
kwa hali ya sasa ya Tanzania, mabadiliko lazima yatokee.
“Kwa muda mrefu sana Watanzania na labda siyo Watanzania ila kwa dunia
kwa ujumla, tunafikiria ulimwengu utabadilishwa na watu wenye mabilioni,
walio na fedha za Escrow, sijui na vitu gani, kwamba hao ndio
watakaoleta mabadiliko. Hapo tunadanganyana sana,” alisema Kardinali
Pengo na kuongeza:
“Wewe fikiria sisi Watanzania wengi tulio masikini, tungesema tumechoka
na hali hii ya nchi, hao wenye madaraka hata wangekuja na mabomu,
bunduki au fedha, sisi tukakubaliana kwamba hatuhongwi na mtu yeyote
mwenye hela, mnaonaje, si tungeleta mabadiliko? Hivi ndivyo Mungu
aliwaambia wachungaji.”
Huku akitoa mfano wa maandiko ya Biblia, Kardinali Pengo alisema
Watanzania kwa sasa ni sawa na wachungaji wa mifugo wa wakati ule wa
kuzaliwa Yesu, ambao waliletewa taarifa na malaika.
“Wakati ule malaika alipeleka habari njema kwa watu duni kabisa, wale
wachungaji walikuwa ni watu ambao hakuna anayewahesabu wakati ule. Sasa
malaika akawaambia nawaletea habari njema, amezaliwa Masiha. Katika
kuwapa habari njema aliwapa ili wakawaambie watu wengine.
“Msiseme sisi wachungaji hawatatusikiliza, ni mimi au ni sisi kama
tungekubaliana wenye fedha wangetuchangia na wakatupatia ingekuwa
rahisi, lakini isingekuwa rahisi kwa ulimwengu huu. Walioneemeka wenye
kipato kizuri, daima walikuwa na tabia ya kutunza kipato chao wabaki
vilevile huku sisi wengi masikini tubaki hivyo hivyo,” alisema Kardinali
Pengo.
Kiongozi huyo wa juu wa Kanisa Katoliki nchini, alishangazwa na jinsi
Watanzania wengi walio katika hali ya umasikini lakini hawashtuki, huku
akiahidi kuendelea kupaza sauti yake hadi waelewe.
“Kama Yohana Mbatizaji, nitapiga kelele nyikani, hata watu
wasiponisikiliza, hata mawe yatanisikiliza na hayo yataleta mabadiliko…
Najua Tanzania tuna wakati mgumu sana, lakini asiwepo hata mtu mmoja
anayesema anakata tamaa kwa sababu mwingine amefanya hivi. Kila mmoja
wetu atekeleze jukumu lake,” alisema.
Alisema katika nchi ni lazima yatokee mabadiliko ili kuleta utengamano
kati ya masikini na matajiri na alisisitiza kuwa mabadiliko hayo
yatakuja kama masikini na matajiri watakapokubaliana.
“Pengo la kipato kwa walionacho na wasionacho linakuja kutokana na wenye
kipato kikubwa kuzidi kujilimbikizia… utajiri wa dunia una kikomo,
tukiwa wengi wenye kipato, kwa kadiri kinavyozidi kuwa kikubwa ndiyo
minofu inazidi kuwa mikubwa halafu tembo anamalizikia. Lakini mkiwa watu
100 na nyama ya tembo vipande vinakuwa vidogo, wale wenye njaa kama ya
simba hawawezi kuridhika,” alisema Kardinali Pengo.
Alisema pamoja na siasa kuwa ni moja ya njia zinazotumika ili kukuza
nafasi ya mtu, jina na mapato ndiyo inayotengeneza mazingira
yanayonusuru uchumi na jamii, ambapo siasa za Tanzania zinawasaidia
wachache.
“ Ni lazima tuunganike na tusianze kutofautiana, utakuta masikini
wanatofautiana, wewe sijui ni Mwislamu, wewe Mkristo, wewe sijui Mngoni
wewe nani, unakuta tena umasikini unatutenganisha badala ya
kutuunganisha. Hata mtakapoingia kwenye familia mtasema, huyu mrefu huyu
sijui Mungu amemuumbaje, tofauti hazitatuunganisha,” alisisitiza.
Akizungumza katika ibada hiyo, Kardinali Pengo alisema anamshukuru Mungu
kwa kufikia umri huo akisema ni upendeleo aliopewa na Mungu.
Kauli hiyo ya kiongozi huyo wa juu wa Kanisa Katoliki nchini imekuja
siku chache tangu Rais Jakaya Kikwete amfute kazi aliyekuwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka Desemba 22,
mwaka huu alipokuwa akihutubia taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es
Salaam.
Uamuzi huo wa Rais Kikwete ulikuja baada ya Bunge kupitia maazimio
manane kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wa waziri huyo,
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Jaji Fredereck Werema ambaye alijizulu na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi ambaye tayari amesimamishwa
kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake.
Awali akieleza lengo la ibada hiyo, Askofu Mkuu msaidizi wa Jimbo Kuu la
Dar es Salaam, Titus Mdoe, alisema Kardinali Pengo alitimiza umri wa
miaka 70 Agosti 5, mwaka huu, lakini hali yake ya afya haikuwa nzuri
ndiyo maana sherehe hizo zikaahirishwa hadi juzi.
“Kardinali amepewa zawadi ya miaka 70 iliyopita, anaifanyia kazi. Kuna
kitu kimefanyika kwake yeye kama wakili na mtumishi wake. Anapojiweka
mbele za Bwana ana kitu cha kusema,” alisema Askofu Mdoe.
Licha ya kusherehekea miaka hiyo, Askofu Mdoe alisema Kardinali Pengo
anaadhimisha miaka 30 ya uaskofu wake na miaka 43 tangu alipopewa daraja
la upadre.
“Miaka 30 ya uaskofu siyo michache… basi Mungu yumo ndani alimkabidhi
mtu mwingine kuwa askofu wa jimbo kule Nachingwea. 1994 kuwa askofu siyo
Dar es Salaam tu, bali majimbo yote. Mwaka 1998 akawa kardinali, kuwa
mkuu siyo Tanzania tu bali Afrika na Madagascar na pia awe msaidizi wa
Papa,” alisema Askofu Mdoe.
30 Desemba 2014
Pengo aonya ufujaji wa Escrow
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni