Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Marekani ikisema haitatoa fedha za Changamoto za Milenia (MCC) hadi utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu ufisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow wa Sh306 bilioni utakapofanyiwa kazi, Ikulu imesema, Rais Jakaya Kikwete hatatekeleza agizo hilo kwa shinikizo la msaada huo.
MCC ni taasisi ya Serikali ya Marekani inayotoa misaada kwa nchi zinazoendelea. Shughuli za MCC zinajengwa katika msingi kwamba msaada utaleta ufanisi na matokeo makubwa zaidi pale tu unapoimarisha utawala bora, uhuru wa kiuchumi na uwekezaji katika watu ambao unakuza uchumi na kuondoa umaskini.
Taarifa hiyo ilisema Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la MCC kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa jana na Ubalozi wa Marekani nchini ilisema, katika mkutano wa bodi hiyo uliokutana Desemba 10 mwaka huu nchini Marekani, ulielezea hofu na masikitiko kuhusu hali ya rushwa inavyoendelea Tanzania.
Fedha ambazo Tanzania ilipaswa kupata kupitia mradi huo wa MCC awamu ya pili ni Dola 450 milioni ambazo ni sawa na Sh765 bilioni.
“Japokuwa bodi ilipiga kura ya kuiruhusu Tanzania iendelee na maandalizi kwa ajili ya mkataba wa pili kwa dhati kabisa, inaihimiza serikali ya Tanzania kuchukua hatua thabiti na mahsusi za kukabiliana na rushwa kama sharti la msingi kwa bodi hiyo kufanya uamuzi wa mwisho wa kuidhinisha mkataba huo.
“Bodi ilieleza kutambua umuhimu wa kusubiri na kuona utekelezaji kamilifu wa tamko lililotolewa na Ikulu ya Tanzania hapo Desemba 9 mwaka huu kwamba itachukua hatua za haraka na kutoa uamuzi dhahiri na thabiti kuhusu maazimio ya Bunge juu la suala la IPTL,” ilieleza taarifa hiyo.
Katika tamko hilo kwa umma, Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress alisema “Kupigwa hatua katika mapambano dhidi ya rushwa ni muhimu sana kwa mkataba mpya kati ya MCC na Tanzania na katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara Tanzania.”
Aliongeza: “Tunatoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kuhusu suala hili hasa kutokana na uzito wake katika masuala muhimu kadhaa ya maendeleo,” ilisema taarifa hiyo.
Hali kadhalika, Bodi iligusia makubaliano kadhaa yaliyofanyika na Tanzania iliahidi kufanya mageuzi ya kisera, kimuundo na kitaasisi ili kuongeza ufanisi na uwazi katika taasisi zake na katika sekta ya nishati.
Balozi Childress aliendelea kusema, “Tunafurahi kwamba mchakato wa majadiliano ya maandalizi ya mkataba wa pili utaendelea kwa miezi kadhaa ijayo. Tunapenda kusisitiza kuwa ni lazima ahadi hizi zitekelezwe kabla Marekani haijafanya uamuzi wa mwisho kuhusu mkataba wowote mpya na Tanzania.”
Katika mkutano huo, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 10 zilizojadiliwa na Bodi ya MCC iliyokutana kuangalia kama nchi hizi zimekidhi vigezo vya kuendelea na mchakato wa kuandaa mikataba mipya.
Iwapo mkataba huo utapitishwa, utakuwa wa pili wa MCC kwa Tanzania kati ya mwaka 2008 na 2013 ambao ulitekeleza mkataba wa uwekezaji wenye thamani ya Dola za milioni 698 sawa na Sh1.18 trilioni ambao uliowezesha utekelezaji wa miradi ya maji, barabara na nishati ya umeme nchini kote Tanzania.
Chini ya mkataba huo, mtandao wa nyaya za umeme wenye zaidi ya kilomita 3,000 ulijengwa, jumla ya kilomita 450 za barabara pia zilijengwa, kadhalika mitambo mikubwa miwili ya usafishaji maji na njia ya kurukia ndege katika kiwanja kimoja cha ndege ilijengwa.
Kauli ya Ikulu
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema hilo ni jambo la kawaida kwani ili uweze kupata msaada huo ni lazima uwe umetimiza masharti na vigezo ambavyo miongoni ni masuala ya utawala bora na rushwa.
“Kabla ya kutia saini wanaangalia masuala ya utawala bora na rushwa na kama walivyosema wanasubiri kuona utekelezaji wake ni jambo la kawaida duniani kutokea.”
Kuhusu Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua za haraka dhidi ya waliohusika na sakata hilo, Balozi Sefue alisema, “MCC ipo au haipo Rais (Kikwete) anachukulia suala hili kwa umakini na atachukua uamuzi kwa misingi ya ushahidi uliotolewa.”
EIL yakazia
Wakala wa Uchunguzi wa Mazingira (EIA) wameitaka MCC kutokubali kuidhinisha mkabata huo na Tanzania wa dola 450 milioni hadi Rais Kikwete atakapochukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya rushwa viliyotawala kwenye sakata la ujangili na usafirishwaji wa pembe za ndovu kwenda nje ya nchi hususani China.
Taasisi hiyo inayojihusisha na masuala ya mazingira ilitoa wito huo jana kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry na Mwenyekiti ambaye pia ni Mkurugenzi wa MCC, Diana Hyde kwamba wasitishe hatua hiyo kwa Tanzania.
Kutokana na hilo, EIA imeomba MCC ambayo imekuwa ikifadhili miradi ya maendeleo nchini kusitisha hatua hiyo kwanza hadi Rais Kikwete atakapolivalia njuga suala hilo.
Novemba mwaka huu, EIA ilitoa ripoti ya utafiti wa ujangili uliyoanika madudu dhidi ya mauaji ya tembo na namna meno yanavyotoroshwa nchini.
Mvutano bungeni
Katiba Bunge la 16/17 lililomalizika mjini Dodoma mwishoni mwa mwezi uliopita, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya walivutana kuhusu ufadhili huo wa MCC uliokwama kutokana na ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow.
Wakati wabunge wakiomba kiti cha Spika kiruhusu kujadiliwa bungeni kwa ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow, Mnyika alisimama na kusema, “kama ripoti hii haitajadiliwa basi fedha zinazotolewa na MCC tutazikosa.”
Baada ya kauli hiyo, Mkuya alisimama na kusema, “Si kweli kwamba tutazikosa fedha hizo kwani taratibu zinaendelea vizuri na mkataba utasainiwa Desemba mwaka huu na fedha hizo zitatoka Desemba.”
Kafulila
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila akizungumzia uamuzi huo wa bodi ya MCC alisema, “taarifa hiyo imekuja wakati mwafaka...imenivisha nguo baada ya kuwa nimevuliwa bungeni na kuitwa mimi mwongo.”
Alisema, “Nilisema bungeni kwamba hasara tunayoipata kutokana na ufisadi huo wa Escrow ni zaidi kwani misaada tuliyokuwa tunaisubiri ya Sh900 bilioni kutoka Ulaya, Marekani Dola milioni 700 na ukijumuisha Sh306 bilioni ni zaidi ya Sh2 trilioni.”
Kafulila alisema fedha hizo zilikuwa zitoke tangu Septemba mwaka huu kama ambavyo Ghana imezipata lakini kutokana na uzembe wa Serikali ya Tanzania, imepoteza kiasi hicho cha fedha.
“Waziri wa fedha (Saada Mkuya) na Profesa Muhongo (Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo) walikana bungeni kwamba ninasema uwongo sasa ukweli umejulikana nani ni mkweli na nani ni mwongo,” alisema Kafulila jana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni