31 Desemba 2014

Kwa heri mwaka 2014 ulionogeshwa na filamu ya Katiba na Escrow

Hatmaye miezi 12 imekamilika leo ikiashiria kumalizika kwa mwaka 2014 utakaokumbukwa na wengi kwa kuwa na matukio motomoto.
Matukio ya kukumbukwa ni mengi, hata hivyo jarida la Ndani ya Habari leo linahitimisha mwaka kwa kuangazia baadhi ya matukio muhimu yalivyoibua mijadala ya kitaifa na kuvuta hisia za watu wengi.
Tanzania Kinara wa ujangili
Februari 10, 2014, ikiwa ni siku chache kabla ya Rais Jakaya Kikwete kuhudhuria mkutano jijini London, Uingereza, uliohusu ajenda ya kuokoa viumbe vilivyo hatarini kutoweka duniani, tatizo la ujangili lilibua kashfa nzito nchini.
Taarifa ya gazeti la The Mail on Sunday la Uingereza la Februari 8, mwaka huu liliitaja Tanzania kama kinara wa ujangili kwa kuua zaidi ya tembo 11,000 kwa mwaka, huku Rais wake (Jakaya Kikwete) akielezwa kuwa anafumbia macho tatizo hilo.
Sehemu ya taarifa hiyo ilinukuliwa ikisema: “Utawala wa Rais Kikwete umetawaliwa na mauaji ya tembo yaliyovunja rekodi katika historia ya nchi yake. Kibaya zaidi, wahifadhi wanasisitiza kuwa ndani ya Serikali kuna viongozi wanaoshiriki biashara hiyo.”
Hata hivyo, Serikali iliagiza kufanya uchunguzi wa kujiridhisha na taarifa hizo, lakini mpaka mwaka unakatika hakuna taarifa zozote zilizotolewa kuhusu tuhuma hizo.
Mfumo mpya wa madaraja ya ufaulu kuibua mjadala
Februari 22, mwaka huu, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), lilitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa 2013, huku ufaulu ukiongezeka kwa asilimia 15.17 kupitia mfumo mpya wa upangaji ambao ulipanua wigo wa alama na madaraja ya ufaulu.
Upangaji mpya wa alama hizo ulikuwa ni A: 75-100, B+:60-74, B:50-59, C:40-49, D:30-39, E:20-29 na F:0-19. Kabla ya mabadiliko hayo, alama zilizokuwa zikitumiwa kupanga matokeo ya kidato cha nne zilikuwa ni A:80-100, B:65-79, C:50-64, D:35-49 na F: 0-34.
Wadau wengi waliokosoa mfumo huo ambao mbali ya kuongeza wigo wa watu kufaulu hata kama hawana sifa, walisema ulikuwa ni mpango maalumu wenye utashi wa kisiasa uliolenga kuwaridhisha wananchi
Ajira Uhamiaji
Ajira imeendelea kuwa wimbo wa kwa vijana wengi hasa wahitimu. Takwimu kutoka Wizara ya Kazi na Ajira zinazoenysha kuwa taifa lina uwezo wa kukidhi mahitaji ya ajira 80,000 mpaka 100,000 kwa mwaka ukilinganisha na mzigo wa vijana 400,000 mpaka milioni moja wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.
Katika kudhihirisha hilo, Juni 13 kulitokea tukio la aina yake katika historia ya nchi baada ya zaidi ya watu 10,000 waliomba kazi ya wakaguzi wasaidizi wa uhamiaji kuitwa na kufanyiwa usaili kwenye Uwanja wa Taifa.
Kilichoshtua wengi katika tukio hili ni idadi kubwa ya wasailiwa hali iliyolazimu wahusika kutumia uwanja wa mpira kufanya usaili wa maandishi.
Hata hivyo, siku chache baadaye, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nachi ilitoa taarifa ikisema wingi wa wasailiwa ni matokeo ya kidemokrasia ya kutoa nafasi kwa kila raia kushindania nafasi za ajira zinazotolewa nchini ili mradi awe na sifa.
‘Filamu’ ya Bunge la Katiba
Bunge la Maalumu la Katiba lilikuwa ni moja kati ya habari zilizoteka vyombo vya habari na hisia za Watanzania wengi kutokana na mijadala mikali, na hata vurugu. Kikubwa katika mchakato wa Bunge la Katiba ilikuwa ni kuwekwa kando kwa hoja ya muundo wa Muungano wa serikali tatu, jambo lilowafanya wajumbe kutoka vyama vya upinzani kuungana na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), na baadaye kususia vikao vya chombo hicho cha kuandika Katiba.
Bunge la Katiba lilianza Aprili 2 likitakiwa kuwa na wajumbe 629 huku matarajio ya wengi yakiwa wajumbe wangetumia nafasi hiyo kujadili mapendekezo ya Rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kwa mshangao wa wengi, bunge hilo lililotawaliwa na hisia na itikadi za CCM kwa kiasi kikubwa liliyapa kisogo mapendekezo ya tume na hatimaye kumalizika kwa kuingiza mapendekezo mapya kwenye Katiba Inayopendekezwa iliyokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete Oktoba 9.
Kashfa ziara ya Rais wa China
Novemba 7, mwaka huu, ziara ya Rais Xi Jinping wa China aliyoifanya nchini Machi mwaka jana, ilizua kizaazaa na kuitia doa sifa ya Tanzania kimataifa, baada ya maofisa waliokuwa wameambatana naye kutuhumniwa kuhusika na biashara haramu ya meno ya tembo.
Ripoti iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya Uingereza Environmental Investigation Agency(IEA), inayojihusisha na uchunguzi wa masuala ya mazingira, inadai kuwa maofisa hao walinunua kiasi kikubwa cha bidhaa hizo katika soko la Mwenge, Dar es Salaam kisha kuzisafirisha kidiplomasia kwa ndege ya rais huyo.
Baada ya kulipotiwa taarifa hizo Watanzania walishtushwa na taarifa hiyo huku serikali ikikanusha vikali madai hayo kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kabla ya kuunda jopo la uchunguzi wa kujiridhisha na ukweli huo.
Hata hivyo, mpaka sasa hakuna taarifa zozote juu ya kamati ya uchunguzi kuhusu kashfa hiyo.
Sakata la Ecrow
Sakata la utata wa kuchotwa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow kwenda IPTL, lilichukua nafasi kubwa ya mjadala kwa mwaka 2014. Lilinogesha ajenda za viongozi wa dini, wanaharakati na jamii huku vituo vya daladala za Tegeta zikipewa majina ya escrow.
Sakata hilo lilikuwa na sura mbalimbali kama vile umiliki wa hisa za Kampuni ya Pan Africa Power Solution Tanzania Limited (PAP), nani mmiliki halali wa fedha za akaunti hiyo, ukwepaji wa kodi, tuhuma za rushwa kwa viongozi na miamala ya malipo iliyotokea katika benki kadhaa.
Ni sakata lililoibuliwa na gazeti la The Citizen ambalo ni gazeti dada na Mwananchi na hatimaye kujadiliwa bungeni na kutolewa maazimio nane, yakiwamo kuwajibishwa baadhi ya watendaji wakuu serikalini, na kupitia upya mikataba yote ya Tanesco na kampuni za umeme.
Baada ya maazimio ya Bunge macho na masikio yalielekezwa kwa Rais Jakaya Kikwete kufanyia kazi mapendekezo. Hatimaye Desemba 22 Rais alikutana na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam na kuelezea kwa kina sakata la Escrow na maazimio ya Bunge.
Ukiondoa kuteungua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kwa jumla mazungumzo ya Rais hayakukidhi matarajio ya wananchi hasa kwa kuyafanyia kazi maazimio ya Bunge.
Hata hivyo, Ikulu ilitangaza kumsimamisha katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi akisubiri uchunguzi. Awali aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Frederic Werema aliandika barua ya kujiuzulu akieleza kuwa ushauri wake haukueleweka na ulizua tafrani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU
KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU

TANGAZO LA KAZI -Commited youth agricultural organisation CYAO is looking for a person who is specialised in agriculture

POSITION DESRIPTION;

Agricultural Technician

Qualifications

Diploma in agriculture

Mode of application applicant must send an updated Cv,birth cirtificate,one recent passport size, an accademic cirtificate, age limit 20 to 35

apply to Project cordinator,Commited youth agriculture organisation,P.O.Box 78438 Dar es salaam or you can call through +255657990920/+255754823728