Ardhi ni mali na watu wanajipatia ardhi kwa njia mbalimbali. Leo tutaangalia njia mbadala ambazo watu hujipatia ardhi hapa nchini.
Leo tutajikita katika zile njia zinazotambulika kisheria na zinazokubalika katika jamii, maana wengine wanapata ardhi kwa kuvamia au kudhurumu, hizo siyo njia sahihi.
Njia ninazozizungumzia leo ni zile za kupewa na Serikali, kununua, kwa kupewa zawadi au kurithishwa na kwa kusafisha sehemu ambayo ni poli na kukaa zaidi ya miaka 12 bila kubugudhiwa.
Mfululizo wa makala hii utachambua njia moja mpaka nyingine, leo nitaanza na ardhi ambayo mtu amemilikishwa na Serikali.
Njia hii inaeleweka kwa wengi na imeanza tangu kipindi cha ukoloni. Kwa sasa mara nyingi haya maeneo yanagawiwa kwa wananchi kwa bei nafuu, na hiyo inatokana na kuwa ardhi ni mali ya wananchi, lakini sheria imemteua Rais kuwa ndiye msimamizi mkuu.
Katika hali ya kushangaza, maeneo yanayotakiwa kugawiwa kwa wananchi kwa bei nafuu, unakuta yanatawaliwa na rushwa na upendeleo wa hali ya juu. Au wanapewa watu ambao wana maeneo tayari bila kufanya uchunguzi wa kina na kutambua nani ana haki ya kupata ardhi katika maeneo hayo.
Tangu mwaka 2008, ule utaratibu wa kupata ofa kwanza ulifutwa na kimsingi, mtu mwenye ardhi kwa njia ya kupewa na Serikali anauwezo wa kuomba ili apewe hati ya eneo husika kwa mujibu wa Kifungu cha 25 cha Sheria ya Ardhi sura ya 113.
Kimsingi, utaratibu uliopo ni kuwa Serikali ikishatangaza maeneo ya kugawa ardhi , wananchi wanapaswa kupeleka maombi kwa kujaza fomu maalumu ili waweze kupewa ardhi hiyo kwa mujibu wa sheria.
Lakini tatizo kubwa la ardhi inayopatikana kwa njia hii ni ya kupewa eneo moja hati tofauti. Unakuta kila mtu ana hati ya umiliki wa eneo lakini eneo ni moja. Hii mara nyingi husababishwa na rushwa na uongozi na usimamizi mbovu wa kumbukumbu za maeneo.
Katika shauri moja, Simon Byamuma v. H.E Haday (Kesi ya Ardhi na. 27/2014) Mahakama ilionya juu ya kugawa eneo kwa watu wawili tofauti, Mahakama kwa kuangalia kesi ya mdai ya kupata hati, ikaonekana ni kasi isiyo ya kawaida, pia mahakama ikaeleza kama wasajili wangekuwa makini wasingetoa hati kwa watu wawili tofauti.
Mpaka sasa sheria iko wazi kama kuna tukio kama hilo wataangalia nani alipewa kwanza kabla ya mtu kugawiwa hilo eneo.
Kimsingi, Mahakama itaangalia nani wa kwanza kusajili ndiye atakuwa na haki, lakini anayesajili awe amepata kihalali.
Village Chairman KCU Mateka v. Anthony Hyera (1988) TLR 188, Kijiji kiligawa ardhi ambayo inamilikiwa na mtu mwingine, Mahakama Kuu ya Tanzania ikiwa Songea, walieleza kuwa Serikali ya kijiji inaweza kugawa ardhi ambayo haimilikiwa na mtu.
Serikali inagawa ardhi kwa kupitia kamati za ugawaji ardhi ambazo zimeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 Kifungu cha 12 na Kanuni za kamati za ugawaji wa ardhi za mwaka 2001 zilizotolewa na Tangazo la Serikali na 72 lililotolewa 4/5/2001.
Kamati za ugawaji wa ardhi zinapaswa kuzingatia yafuatayo katika ugawaji wa ardhi; kuangalia uhitaji wa mtu, umri, je mtu huyo ana ardhi nyingine, ulemavu na makundi yanayo hitaji, asiyeridhika na uamuzi wa kamati anaweza kukata rufani katika baraza la ardhi na nyumba la wilaya.
Mwandishi wa Makala hii ni Jebra Kambole Wakili wa Kujitegemea kutoka Kampuni ya Law Guards Advocates wa jijini Dar es Salaam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni