Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kurejea nchini Jumamosi, Novemba 29 baada ya taratibu za matibabu yake nchini Marekani kukamilika.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilisema jana kuwa taratibu hizo zilikamilika saa 12 asubuhi jana, baada ya madaktari bingwa katika Hospitali ya Johns Hopkins kumfanyia hatua ya mwisho ya tiba.
Hata hivyo, Rais Kikwete ataendelea kupumzika na kuangaliwa kwenye Hoteli Maalumu inayohusiana na Hospitali ya Johns Hopkins kwa siku mbili hadi tatu kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani.
Rais Kikwete aliondoka nchini Alhamisi ya Novemba 6, 2014, kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya yake lakini madaktari katika Hospitali ya Johns Hopkins waliamua kumfanyia upasuaji wa tezi dume Jumamosi ya Novemba 8, 2014.
Taarifa hiyo ilisema Rais Kikwete anaendelea kuwashukuru Watanzania kwa sala na maombi yao ya kumtakia heri ya kupona haraka na kurejesha afya njema katika kipindi chote cha ugonjwa wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni