Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova amesema ulinzi utaimarishwa kabla, wakati na baada ya mdahalo maalumu wa Katiba ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam mzungumzaji mkuu akiwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Hatua ya Kova imekuja baada ya kuibuka kwa vurugu zilizosababisha kuvunjika mdahalo wa kwanza uliofanyika Novemba 2, kwenye Hoteli ya Blue Pearl Ubungo, Dar es Salaam.
Kova alisema polisi imejiandaa kwa ulinzi ili kudhibiti vurugu zozote zitakazotokea pamoja na kuhakikisha usalama wa washiriki na eneo zima kwa ujumla.
“Mdahalo ule wa kwanza uliovurugwa, hatukuwa na taarifa nao, lakini huu waandaaji wametupa taarifa hivyo tumejiandaa kuimarisha ulinzi, ili kuhakikisha amani inatawala katika eneo hilo,” alisema.
Juzi, Mwenyekiti wa MNF, Joseph Butiku alisema ofisi yake inaamini kwamba mdahalo huo wa wazi kwa ajili ya Watanzania wenye mapenzi mema utakuwa wa amani. Alisema uhakika wa usalama katika mdahalo huo unatokana na kwamba wameshatoa taarifa kwa vyombo vya usalama.
Alisema mdahalo wa leo ni sehemu tu ya ushiriki wa mijadala ya umma kuhusu Katiba Inayopendekezwa, ambayo kwa sasa inaendelea katika maeneo yote ya nchi, ikifanywa na viongozi wa kisiasa, mashirika ya kijamii na hata watu binafsi katika vyombo mbalimbali vya habari.
Alisema japokuwa kwa sasa wamepata ukumbi mdogo unaoweza kuingiza watu 350, watatoa fursa kwa watu kuuliza maswali na kupata majibu kuhusu vifungu na vipengele mbalimbali vyenye utata vinavyoyahusu makundi yote ya kijamii ambayo yamepata uwakilishi katika mapendekezo hayo ya Katiba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni