Mwanasiasa huyo kijana pia amemtetea aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman kwa kukataa vipengele 22 kwenye Katiba Inayopendekezwa, akisema alitoa maoni yake binafsi kama alivyofanya Rais Jakaya Kikwete wakati akizindua Bunge la Katiba mwezi Machi.
Dar es Salaam. Ikiwa ni takriban majuma mawili sasa tangu Bunge la Maalumu la Katiba likamilishe kazi ya kuandika Katiba Inayopendekezwa, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi amesema anajuta kumchagua Samuel Sitta kuwa mwenyekiti wa chombo hicho, akidai kuwa amesaliti ahadi yake kwa wapinzani wakati akiomba kura.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Mbilinyi alimtuhumu Sitta kuwa aliwageuka wapinzani baada ya kuchaguliwa kuongoza chombo hicho cha kihistoria kwa kuweka mbele masilahi yake binafsi na Chama cha Mapinduzi (CCM) badala ya wananchi wote, kama alivyoahidi wakati akiomba kura za kuwa mwenyekiti wa Bunge la Katiba.
Sitta, ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Bunge la Tisa, alionekana anakubalika na pande zote, CCM na wapinzani, na hivyo chama hicho kumpitisha kuwania uenyekiti wa Bunge la Katiba ambao alishinda kwa kupata asilimia 86.5 dhidi ya mpinzani wake, Hashim Rungwe Sipunda aliyepata asilimia 12.3. “Najuta kumfanyia Sitta kampeni,” alisema Mbilinyi, msanii wa muziki wa rap ambaye mashairi ya baadhi ya nyimbo zilizompatia umaarufu yalikuwa yamejaa utetezi wa haki.
“Wakati wa kampeni, Sitta alinifuata kwa upole akiniomba nimpigie debe ili akishinda, atekeleze pamoja na mambo mengine, madai ya serikali tatu yaliyotolewa na wajumbe wa upinzani,” alisema Mbilinyi ambaye jina lake maarufu la kisanii ni Sugu.
“Sitta alikuja kwangu na kuniambia ‘Sugu unajua kuwa una kura zangu 100 za wajumbe kutokana na ushawishi wako kwa vijana na hata wajumbe wa CCM?’
“Mimi nilimuuliza ‘kwa nini nikupe kura 100?’ Sitta huyu huyu akanijibu ‘unajua mkimchagua (Andrew) Chenge ana msimamo wa serikali mbili, lakini wananchi wanataka serikali tatu. Mkinichagua mimi nitasimamia hilo,” alidai Sugu.
Hata hivyo, Chenge hakuingia kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya vikao vya ndani vya CCM kumpitisha Sitta. Badala yake, Chenge aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi.
Julai mwaka jana, Sitta alikaririwa akiunga mkono serikali tatu, lakini akapinga nchi kuongozwa na marais watatu akisema wakuu wa Zanzibar na Bara wawe na hadhi nyingine badala ya urais, huku akipendekeza kuwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania libadilishwe na kuwa Shirikisho la Nchi za Tanzania.
Hata hivyo, Mbilinyi anaona huo ulikuwa ujanja. “Sitta alitumia ujanja ujanja kufika pale ili afanye ya kwake binafsi kufikisha maoni yake na ninashukuru kuwa amejidhihirishia kuwa ameanguka katika harakati za urais mwakani na hatakuwapo katika mchakato huo,” alisema Mbilinyi.
“Ninajuta kumpa kura yangu na ninajuta kwa wajumbe wa 201 kumpa kura Sitta kwani ameshindwa kusimamia kile alichokiahidi.”
Sitta, mbunge wa Urambo Mashariki na ambaye anatajwa kuwania urais mwakani kwa tiketi ya CCM, alianza kusakamwa kutokana na kumruhusu Rais Jakaya Kikwete kuzindua Bunge la Katiba baada ya mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kusoma hotuba yake na kuwasilisha Rasimu ya Katiba, kitendo kilichomruhusu mkuu huyo wa nchi kuchambua baadhi ya vipengele na kutoa maoni yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni