KIMENUKA, mzaha mzaha siku zote hutumbua usaha! Hali imeshakuwa mbaya kwa nyota mtukutu wa Liverpool, Mario Balotelli, baada ya taarifa za ndani ya klabu yake kusema kuwa mchezaji huyo atawekwa sokoni Januari.
Imeelezwa kwamba viongozi wa klabu hiyo hawatajali hasara ya kumnasa mchezaji huyo kwa Pauni 16 milioni katika dirisha la usajili lililopita.
Balotelli ambaye alihamia Liverpool akitokea AC Milan alishindwa kutamba kwenye timu yake ya awali, lakini kocha Brendan Rodgers alitegemea nyota huyo angebadilika.
Hata hivyo sikio la kufa halisikii dawa, ubovu wa Balotelli umejionyesha wazi. Tangu msimu huu ulipoanza, nyota huyo amefunga bao moja tu jambo ambalo si sahihi kwa mshambuliaji wa kati.
Katika kupigilia msumari wa moto, nyota wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher, amesema kuwa haoni sababu yoyote ya kuendelea kumfuga mchezaji huyo ambaye haonyeshi ushindani.
Carragher alisema kuwa anatarajia kuona klabu hiyo ikimtimua Balotelli kabla ya kuanza msimu ujao. Carragher ambaye hakufurahishwa na kasi ndogo ya nyota huyo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid juzi Jumatano usiku ambapo Liverpool ilichapwa mabao 3-0, alisema: “Mario hawezi kubadilika, yeye ni mtukutu, labda alivumiliwa akiwa Machester City kwa sababu alikuwa akifunga mabao.
“Lakini hawezi kuvumiliwa sehemu ambayo hafungi mabao na kibaya zaidi ni kuwa anafanya utukutu.”
Katika mechi hiyo ya juzi, mchezaji huyo alibadilishana jezi na Pepe wakati wa mapumziko. Carragher alisema: “Nadhani wakati umefika kwa kocha wa Liverpool, Rodgers kukubali kuwa amemsajili Balotelli akiwa na kiwango hafifu sana na hana sababu ya kumbakiza kwenye timu yake.”
Carragher aliongeza kuwa haoni uwezekano wa nyota huyo ambaye alisajiliwa kuchukua nafasi ya Luis Suarez kama atafikia hata robo ya uwezo wa Suarez.
“Mwaka jana mabao ya Luis Suarez na Daniel Sturridge yaliwafikisha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, hayo ni mafanikio. Ilikuwa si jambo rahisi kwa timu hiyo kufunga zaidi ya mabao 100, lakini iliwezekana. Ni lazima kocha amsajili mtu mwingine kama anataka kikosi kisonge mbele,” aliongeza Carragher.
Kocha Rodgers hakufurahishwa na kitendo cha Balotelli cha kubadilishana jezi na Pepe wakati wa mapumziko, lakini hakutaka kuzungumza mengi juu ya tukio hilo.
Katika hatua nyingine, kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, amesema kuwa hakuna sababu ya kumtupia lawama Balotelli kwa kuwa si yeye peke yake aliyecheza vibaya. Alisema wachezaji kadhaa wa Liverpool walicheza chini ya kiwango.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni