25 Oktoba 2014
Kura ya Maoni mkorogano
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema, “Tangu mwanzo niliupinga mchakato wa Katiba na matokeo yake imezaliwa Katiba Inayopendekezwa isiyokuwa na maoni muhimu ya Watanzania. Sikubaliani na mchakato wa kura ya maoni.”Profesa Mpangala alisema mchakato wa kupata Katiba Mpya unatakiwa kurudiwa mwaka 2016 kwa maelezo kuwa Katiba itakayopatikana haitakuwa na ridhaa kwa Watanzania.
Dar es Salaam. Kitendo cha Serikali kutoa kauli tatu tofauti ndani ya wiki moja kuhusu tarehe ya Kura ya Maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa, kimeelezwa na watu wa kada mbalimbali nchini kuwa ni matokeo ya viongozi wa Serikali kukosa uongozi wa pamoja.
Wakizungumza na Mwananchi Jumamosi, wasomi, wanaharakati, viongozi wa dini na wanasiasa wamesema kauli hizo zinawachanganya Watanzania, kwamba mpaka sasa hakuna anayejua tarahe rasmi ya kufanyika Kura ya Maoni.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alilieleza gazeti hili kuwa kura hiyo ingefanyika Machi 30 mwakani na kwamba upigaji kura utatanguliwa na kampeni ambazo zitafanyika kwa siku 30, kuanzia mwanzoni mwa Machi ili kushawishi Katiba Inayopendekezwa iungwe mkono au kinyume chake kwa makundi yanayoipinga.
Siku moja baadaye, Rais Kikwete alipokutana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Jamhuri ya Watu wa China alisema endapo mipango yote itakwenda kama inavyoandaliwa, Watanzania wataipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa Aprili mwakani.
Kauli ya Jaji Werema pia ilipingwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva na kufafanua kuwa kura ya maoni haiwezi kufanyika Machi 30 mwakani kwa sababu kazi ya uandikishaji wa Daftari la Wapigakura haitakuwa imekamilika.
Utata umezidi kuongezeka baada ya jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, Jaji Lubuva kusema kuwa Daftari la Kudumu la Wapigakura litakamilika Aprili 18 mwakani, huku taratibu zikieleza kwamba kura ya maoni itafanyika baada ya elimu kutolewa kwa wananchi na hutolewa kati ya miezi mitatu hadi sita.
Awali Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwahi kukaririwa akisema kuwa Kura ya Maoni ifanyike kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015, huku Rais Kikwete akikubaliana na viongozi wa vyama vya siasa kuwa kura ya maoni itafanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti Mwalimu wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Faraja Christoms alisema, “Hayo ni matokeo ya kukosekana kwa uwajibikaji wa pamoja. Sina hakika kama AG ndiye alipaswa kutaja tarehe ya kura ya maoni, yeye ni mshauri tu.”
Alisema kitendo cha kauli ya AG kutofautiana na iliyotolewa na rais ambaye amemteua ni ishara mbaya katika utendaji kazi wa Serikali.
“Wakati mwingine kauli kama hizi zinaweza kuwavunja moyo walioteuliwa. Nakumbuka Waziri Mkuu Pinda aliwahi kutoa kauli ya kupinga maelezo ya Waziri wa Ujenzi, Magufuli (John). Tafsiri ya kilichotokea ni kukosekana kwa uwajibikaji wa pamoja,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dk Leonard Mtaita alisema kazi iliyobaki ni kuwahamasisha wananchi wakati wa kupiga kura ya maoni utakapofika kwa maelezo kuwa kila mtu atapiga kura kutokana na anachokiamini.
Dk Mtaita alisisitiza pia kuboreshwa kwa Daftari la Wapigakura, akisema kuwa hilo ndilo litakuwa jambo la msingi ili kuwafanya Watanzania wote wenye sifa waweze kupiga kura, huku akiiomba Serikali kuhakikisha inasambaza nakala za kutosha za Katiba Inayopendekezwa.
Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St Augustine, Dk Charles Kitima alisema, Serikali kupuuza mawazo na malalamiko ya watu ni ishara mbaya, kufafanua kwamba Katiba Inayopendekezwa ina uhalali wa kisheria lakini inakosa uhalali wa kisiasa na ili kuokoa mvutano, maridhiano ni jambo la msingi.
“Wananchi wanaulalamikia mchakato wa Katiba, pamoja na mvutano unaoendelea, haya malalamiko ya wananchi si ya kufurahia hata kidogo. Jambo hili linatakiwa kupatiwa ufumbuzi,” alisema.
Aliongeza, “Rais ndiye anayetakiwa kutueleza msimamo wake ni nini juu ya suala hili. Je, na yeye atafuata masilahi ya CCM au atazungumza kama Rais. Kama maridhiano yatakosekana na Katiba hiyo ikapitishwa, haitadumu muda mrefu kwa sababu watawala wengine watakaokabidhiwa kijiti wataibadili Katiba hiyo.”
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala ya kijamii, Fordia, Bubelwa Kaiza alisema tofauti za kauli za viongozi zinaonyesha kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya uliendeshwa katika taratibu zisizo sahihi, ndio maana hakuna kauli moja kuhusu siku ya kupiga kura ya maoni.
“Hayo ni majibu kwamba ndani ya serikali kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu suala zima la Katiba Mpya. Hakuna msemaji sahihi, kila mtu anazungumza lake. Ndio maana hata katika Bunge Maalumu kila mtu alifanya lake, sheria zilibadilishwa bila kufuatwa kwa utaratibu,” alisema.
Alifafanua kuwa ni ngumu kwa kila jambo linalohusu Katiba kwenda vizuri kwa sasa kwa sababu mchakato uliharibika baada ya kuanza vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema elimu ya uraia inatakiwa kutolewa miezi mitatu hadi sita kabla ya kufanyika Kura ya Maoni, si siku 30 alizozitaja Jaji Werema.
“Huwezi kutoa elimu ya uraia kwa siku 30, mfano Zimbabwe walitumia miezi sita kutoa elimu ya uraia. Mchakato huu umeingiliwa na wajanja, si riziki tena, ni kama mtu aliyejifungua mtoto aliyekufa,” alisema.
Kibamba alisema Nec ilieleza kuwa kufikia Mei ndiyo itakuwa imemaliza kazi ya kuboresha Daftari la Wapigakura, kwamba kitendo cha Jaji Werema kueleza kuwa Kura ya Maoni itafanyika Machi mwakani, ni ishara ya ‘ukambale’.
“Waziri Mkuu (Pinda) alisema Katiba ipatikane kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015, Rais Kikwete akakubaliana na TCD kuwa ni 2016, jana (juzi) Jaji Werema anatueleza kuwa ni Machi mwakani, tumsikilize nani?”
Alisema tarehe ya kura ya maoni kwa mujibu wa sheria inatakiwa kutangazwa na Rais si Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kibamba alisisitiza kuwa Serikali bora ni ile inayojiendesha kwa uwajibikaji wa pamoja.
Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Felix Kibodya alisema, “Tamko la Serikali kwa jambo kama hilo huwa ni moja na si kila kiongozi kutoa tamko lake. Ndiyo maana tarehe ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ilitolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, si mtu mwingine.
Alisema huenda mkanganyiko ulioibuka juu ya tarehe rasmi ya kura ya maoni unatokana na nchi kutowahi kuendesha zoezi la upigaji wa kura hiyo.
“Sheria inaeleza wazi kuwa rais atatangaza tarehe rasmi siku 84 baada ya kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa. Ili muda usogezwe mbele ni lazima sheria ibadilishwe, nadhani hilo linaweza kufanyika katika kikao kijacho cha Bunge,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severini Niwemugizi alisema mchakato wa Katiba ni suala la kisheria na kisiasa, hivyo kama Rais alikutana na wanasiasa na kukubaliana, ingekuwa jambo jema kama makubaliano hayo yangezingatiwa.
“Kama ni suala la sheria, sheria husika inabadilishwa lakini kama ni suala la makubaliano ya wanasiasa, pia lilitakiwa kuzingatiwa. Kwa sasa kuna mvutano mkali, sijui nini kitatokea,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbrod Slaa alisema jambo hilo linatokana na viongozi wa Serikali kugawanyika huku akitolea mfano kauli ya Rais Kikwete kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ungefanyika Februari mwakani, lakini baadaye Waziri Pinda akatangaza kuwa utafanyika Desemba 14 mwaka huu.
“Nchi inayokuwa na viongozi ambao kila mmoja anatoa kauli yake haiwezi kuwa na mshikamano. Wao hawana umoja halafu wanataka Watanzania kuwa na umoja, hilo litawezekana kweli?” alihoji Dk Slaa.
Aliongeza, “Hata kura ya maoni ikifanyika leo haina maana tena kwa sababu Katiba Inayopendekezwa imeondolewa mambo ya msingi yaliyotokana na maoni ya wananchi. Wanasema Katiba hii ni bora barani Afrika, sijui nani kawadanganya.”
Dk Slaa alisisitiza kuwa ili hali iwe shwari ni lazima kura ya maoni ifanyike wakati ambao Nec itakuwa imeliboresha Daftari la Wapigakura. “Watambue kuwa safari ya kudai Katiba Mpya ndiyo inaanza sasa kwa sababu Katiba Inayopendekezwa ni mali ya CCM, si Watanzania.”
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka alisema, “Kama tunaamini kuwa Katiba Inayopendekezwa siyo nzuri, umefikia wakati wa kuwaachia wananchi wapige kura. Kama ni nzuri wataipitisha na kama hawaikubali wataikataa.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema, “Tangu mwanzo niliupinga mchakato wa Katiba na matokeo yake imezaliwa Katiba Inayopendekezwa isiyokuwa na maoni muhimu ya Watanzania. Sikubaliani na mchakato wa kura ya maoni.”
Profesa Mpangala alisema mchakato wa kupata Katiba Mpya unatakiwa kurudiwa mwaka 2016 kwa maelezo kuwa Katiba itakayopatikana haitakuwa na ridhaa kwa Watanzania.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe alisema, “Hayo ni matokeo ya nchi kuwa na sheria mbovu. Katiba yetu pamoja na sheria za nchi hii hazieleweki. Rais amepewa madaraka makubwa kiasi kwamba wengine wakitoa kauli hata kama wanaweza kufanya hivyo, kauli zao zinaonekana si kitu mbele ya kauli ya Rais.”
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni