05 Oktoba 2014

Halima Mdee akamatwa Dar

Dar es Salaam. Mbunge wa Kawe na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee ametiwa nguvuni na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa madai ya kuongoza maandamano ya baraza hilo kwenda Ikulu.

Habari zilizotufikia wakati tukienda mitamboni, zilisema Mdee baada ya kuachiwa kwa dhamana, aliitisha mkutano wa hadhara jimboni kwake Kawe, lakini polisi walimkamata tena kwa mara ya pili.

Katika tukio la kwanza wengine waliokamatwa na Mdee walikuwemo Diwani wa Viti Maalumu wa chama hicho, Rose Moshi, Mratibu wa Uhamasishaji wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Edward Simbeye na wanachama wengine sita walikamatwa katika maandamano hayo yaliyokuwa na lengo la kwenda kuonana na Rais Jakaya Kikwete kumshinikiza kutoipokea Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Wengine waliokutwa katika kadhia hiyo ni Martha Charles, Beauty Mmari, Anna Linjewele, Sofia Phanuel, Remina Peter na Mwanne Kassim. Hata hivyo wote waliachiwa jana jioni kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camilius Wambura alithibitisha kuwashikilia wafuasi hao ingawa hakueleza hatua zinazoendelea baada ya kuwatia nguvuni.

Juzi jioni, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliyapiga marufuku maandamano hayo kwa kuwa hawakuwa na sababu ya msingi ya kuandamana kwenda kuonana na Rais Kikwete.

Mara baada ya kukamatwa na kupakiwa katika gari la polisi lililokuwa limesheheni askari wenye silaha na mabomu ya machozi na lingine likiwa nyuma likisindikiza, yalikwenda katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay.

Aidha, katika hatua nyingine, polisi wa kituo hicho waliendeleza ubabe kwa waandishi wa habari kwa kuwazuia kupata fursa ya kupata habari hasa baada ya Mdee kufikishwa kituoni hapo.

“Nasema ondokeni, hatutaki mtu hapa,” alisema askari mmoja aliyejulikana kwa jina la EM Tille ambaye muda wote alikuwa akiwazonga waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari.

Jana asubuhi maandalizi ya maandamano hayo yalianza saa mbili kwa wahusika kuanza kukusanyika katika ofisi za Bawacha zilizopo Mtaa wa Togo, Kinondoni jijini humo karibu na Kituo Kidogo cha Polisi Kinondoni.

Wakati wakiendelea kukusanyika, polisi nao walikuwa wakifanya doria kwenye mitaa inayozunguka ofisi hiyo, wakiwa katika magari manne yaliyosheheni askari polisi na silaha mbalimbali pamoja na gari la maji ya kuwasha.



Saa 3.58 asubuhi, Mdee alifika katika ofisi hizo ambapo shangwe zilianza kutawala viunga hivyo kwa kuimba nyimbo za kuhamasishana, huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali hasa kulaani mchakato mzima wa Bunge Maalumu la Katiba.

Mabango hayo yalisomeka: ‘Katiba sio mali ya CCM’, ‘Rais usipochukua hatua, wananchi tutakulazimisha uchukue hatua’, ‘Bilioni 20 ndani ya siku 50 wakati wamama wanakufa hospitali’, ‘Katiba ya CCM hatuitaki’, ‘Chenge wa vijisenti kapata wapi uzalendo’ na ‘Ardhi, wakulima, wavuvi, afya nk hayo ni ya Tanganyika hatutaki unyonyaji- haki itawale’.

Msafara wa kuelekea Ikulu ulianza saa 4.18 asubuhi kwa Mdee kusema utapita Umoja wa Mataifa kwenda kuingia Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na kundi la pili litaanzia Mnazi Mmoja lililokuwa liongozwe na Mbunge wa Viti Maalumu Ester Matiko kabla ya kutofanyika kutokana na kukamatwa kwa Mdee.

Wakati maandamano hayo yakielekea Ikulu kuanzia zilipo ofisi za baraza hilo Mtaa wa Togo, magari manne ya polisi yaliyosheheni polisi wenye silaha na gari la kuwasha yalikuwa yamefunga mtaa huo hivyo kuwalazimu waandamanaji hao wakiongozwa na Mdee kupita Mtaa wa Ufipa karibu na Makao Makuu ya Chadema.

Wakati wakikata kona kuingia Mtaa wa Ufipa, mita 100 kutoka yalipo makao makuu ya Chadema, gari la maji ya kuwasha lilianza kumwaga maji hayo saa 4.23 ambapo waandamanaji hao waliingia katika kibanda kimoja na askari wa kiume waliingia kuwakamata.

Wakati askari hao wakielekeza nguvu kumkamata Mdee, mmoja wa waandamanaji hao Sofia alitumia nguvu nyingi kumsaidia ili asipate kipigo kutoka kwa polisi, lakini ilishindikana.

Walipokuwa wakimwingiza katika gari askari hao walikuwa wakimpiga Mdee kwa mateke, makofi na askari mwingine alitumia fimbo yake kumchapa sanjari na wanachama wengine waliofikwa na mkasa huo.

Tukio hilo lilipokuwa likiendelea umati wa watu ulikusanyika katika mtaa huo kushuhudia kilichokuwa kikiendelea wakati wa maandamano hayo yaliyokuwa na watu kati ya 50 hadi 80.

Mara baada ya kukamatwa kwa Mdee na kupelekwa Oysterbay, polisi wa kituo hicho waliimarisha ulinzi kwa kutoruhusu mtu au gari lolote kuingia bali walitakiwa kuishia ng’ambo ya barabara.

Katika kituo hicho, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kinondoni, Henry Kileo na Mkurugenzi wa Oganaizesheni wa Mafunzo ya Kanda wa chama hicho, Singo Kigaila na wafuasi wengine walitumia dakika 30 kubishana kutokana na kuzuiliwa kwenda kujua hatima ya wanachama wenzao.

“Unatuzuia kama nani’...Acheni kutumika na CCM’, zilisikika sauti za wanachama hao huku Polisi waliokuwa na silaha wakisema “Ondokeni hapa, nendeni kule ng’ambo na haturuhusu mtu yeyote kusogea hapa,” alisema askari mmoja huku wakifunga riboni karibu na Barabara ya Ali Hassan Mwingi na kuwataka kutouvuka.

Wanachama hao hawakuondoka eneo hilo na kubaki wakiimba nyimbo mbalimbali za kuwasifu wanachama waliokamatwa kwa ujasiri waliouonyesha. Hadi mwandishi wa gazeti hili anaondoka hapo saa 10 jioni wafuasi hao walikuwapo eneo hilo.

Awali Mdee asubuhi akizungumza na waandishi wa habari alisema; “Mmeona polisi walivyotanda, tutaandamana na hatujui kitakachotokea ila lengo letu ni kufikisha ujumbe kwa Rais Kikwete kuwa Rasimu iliyopitishwa haitamkomboa mwananchi.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU
KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU

TANGAZO LA KAZI -Commited youth agricultural organisation CYAO is looking for a person who is specialised in agriculture

POSITION DESRIPTION;

Agricultural Technician

Qualifications

Diploma in agriculture

Mode of application applicant must send an updated Cv,birth cirtificate,one recent passport size, an accademic cirtificate, age limit 20 to 35

apply to Project cordinator,Commited youth agriculture organisation,P.O.Box 78438 Dar es salaam or you can call through +255657990920/+255754823728