Mahenge. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba wamewaomba viongozi wa dini kuwasamehe viongozi wa Serikali waliokwaruzana nao wakati wa mchakato wa Katiba na kuliombea Taifa lipate viongozi wenye hekima na uwezo katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Viongozi hao walisema hayo jana katika maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mahenge. Makamba ameshatangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi huo na Lowassa, licha ya kwamba hajatangaza nia hiyo, amekuwa akihusishwa na kinyang’anyiro hicho.
Lowassa
Akihutubia katika sherehe hizo, Lowassa aliliomba Kanisa, kusamehe sintofahamu iliyojitokeza kati yake na baadhi ya viongozi wa Serikali akisema lina mchango mkubwa katika kudumisha amani na mshikamano nchini.
“Najua hivi karibuni tuliwaudhi, lakini mimi naomba mtusamehe bure tu... kama vile mzazi anavyomsamehe mtoto wake anapokosea, tunaomba radhi sana,” alisema Lowassa na kuongeza kuwa anafanya hivyo kwa kuwa kanisa hilo ni muhimu katika maendeleo ya nchi.
Pamoja na kutotaja majina, wakati wa utungaji wa Katiba Inayopendekezwa, Mwenyekiti wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta aliingia katika mgogoro na baadhi ya viongozi Kikristo baada ya kuuponda waraka waliokuwa wameusambaza makanisani kupinga mchakato huo kwamba ni wa kipuuzi.
Kwa upande mwingine, Lowassa alimpongeza Mbunge wa Ulanga Mashariki, Celina Kombani kwa kuiletea maendeleo wilaya yake ya Mahenge. “Kwa kazi kubwa aliyoifanya Kombani, nina hakika atapita bila kupingwa,” alisema na kushangiliwa.
Makamba
Makamba aliliomba kanisa hilo kusaidia kuiombea nchi katika Uchaguzi Mkuu ujayo ili ipate viongozi wenye hekima na uwezo wa kuwatumikia wananchi bila kubagua.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), alitangaza kuisaidia Shule ya Sekondari ya Kwiro kompyuta 10 pamoja na mashine moja ya kudurufu. Hiyo ilikuja baada ya Lowassa kutangaza kuizawadia kwaya ya kanisa hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni