NYOTA ya Mwanamuziki wa kizazi kipya nchini, Nassib Abdul ‘Diamond’, imezidi kung’aa baada ya kutwaa tuzo ya Msanii Bora wa mwezi huu wa Kituo cha Televisheni cha Mtv-Base cha Afrika Kusini.
Mbali na kutwaa tuzo hiyo, Diamond pia anawania tuzo ya All African Music (Afrima) inayofanyika nchini Nigeria pamoja na wasanii wenzake Peter Msechu na Vanessa Mdee.
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa televisheni hiyo, zilieleza kwamba kila mwezi wanakuwa na tuzo hiyo ambapo inatokana na vipindi vyao mbalimbali kama Mixtape na 10 Bora.
Ilieleza mashabiki hupiga kura kupitia mitandao ya kijamii ambapo huulizwa na nyimbo zipi ambazo zinapigwa kwa mwezi husika na mwisho wa siku hupata mshindi.
Katika tuzo hizo za Afrima, Vanessa anawania vipengele viwili vikiwemo vya Msanii Bora Afrika Mashariki pamoja na Msanii Bora Afrika wa miondoko ya R&B Soul.
Diamond na Msechu wametajwa kuwania tuzo ya Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki pamoja na Wimbo Bora wa kushirikiana.
Wasanii waliotajwa kuwania tuzo hizo, watawasilisha kazi zao kwa jopo la majaji wa Afrima kwa nyimbo zao walizotoa kati ya Mei 15, mwaka jana hadi Julai 21, mwaka huu na kwamba jumla ya kazi 2,025 zilipokelewa kufanyiwa kazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni