Kiongozi wa zamani wa Waserbia wa Bosnia, Radovan Karadzic, amehukumiwa
kifungo cha miaka 40 gerezani, baada ya Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya
Uhalifu wa Kivita-ICTY, kumkuta na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji kiongozi katika kesi hiyo, inayosikilizwa
kwenye mahakama hiyo ya ICTY iliyoko The Hague, O-Gon Kwon amesema Karadzic akiwa kama kiongozi wa kisiasa na kamanda wa majeshi wa vikosi vya Serbia nchini Bosnia, ambavyo vinatuhumiwa kufanya mauaji, amepatikana na hatia ya kuizingira Sarajevo na uhalifu dhidi ya ubinaadamu kwenye miji na vijiji vingine wakati wa vita vya Bosnia katika miaka ya 1990.
Mahakama ya ICTY imesema Karadzic amepatikana na hatia ya mauaji, kuwashambulia raia na ugaidi kutokana na vitisho alivyotoa wakati alipouzingira mji mkuu wa Bosnia, Sarajevo kwa miezi 44, wakati wa vita nchini humo. Kiongozi huyo pia amepatikana na hatia ya makosa mengine tisa, ikiwemo mauaji na mateso.
''Mtuhumiwa alikuwa anashtakiwa kwa makosa 11: mawili ya uhalifu wa kimbari, matano ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu, hasa mauaji, mateso na kuwahamisha watu kwa lazima. Na mashtaka manne ya ukiukaji wa sheria za vita,'' alisema Jaji Kwon.
Hata hivyo, Karadzic amefutiwa moja ya mashtaka yaliyokuwa yanamkabili ya mauaji ya kimbari, baada ya kukosekana kwa ushahidi unaomuonyesha kiongozi huyo wa zamani kuhusika na mauaji hayo wakati wa vita vya Bosnia kuanzia mwaka 1992 hadi 1995.
Uhalifu haukuwa mkubwa sawa na mauaji ya kimbari
Jaji Kwon amesema uhalifu mkubwa ulifanywa na vikosi vya Waserbia wa Bosnia dhidi ya kampeni ya kuwatimua Waislamu wa Bosnia na Wakroatia wa Bosnia katika vijiji vya Bosnia vilivyotekwa na kusababisha mauaji ya watu 100,000, lakini uhalifu huo haukuwa mkubwa sawa na mauaji ya kimbari.
Karadzic mwenye umri wa miaka 70, na ambaye baada ya kuwasili katika chumba cha mahakama inaposomwa hukumu yake, aliwasalimia majaji na kuitambulisha timu yake ya washauri wa kisheria. Aidha, kiongozi huyo amesisitiza kwamba hana hatia na amesema matukio aliyoyafanya wakati wa vita, yalikuwa na lengo la kuwalinda Waserbia.
Kesi ya Karadzic ni moja kati ya matukio ya mwisho ya Mahakama hiyo ya uhalifu wa kivita kwa ajili ya Yugoslavia, iliyoanzishwa mwaka 1993. Mahakama hiyo imewafungulia mashtaka watuhumiwa 161, miongoni mwao 80 wamepatikana na hatia na kuhukumiwa, 18 waliachiwa huru, 13 walirudishwa kwenye mahakama za ndani na 36 mashtaka dhidi yao yalifutwa au walikufa.
Mbali na Karadzic, watuhumiwa wengine watatu bado kesi zao zinaendelea kusikilizwa, akiwemo mkuu wa jeshi, Jenerali Ratko Mladic na mzalendo wa Serbia, Vojislav Seselj.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni