Tanzania imesema inasubiri ripoti
ambayo imewataja wanajeshi wa Tanzania kuwa miongoni mwa wanajeshi wa
kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaotuhumiwa kuhusika katika visa vya
unyanyasaji wa kingono.
Jeshi la Tanzania linakabiliwa na tuhuma
tatu za unyanyasaji wa kingono kati ya tuhuma 69 zilizoorodheshwa kwenye
ripoti hiyo inayoangazia tuhuma zilizotolewa mwaka 2015.Visa hivyo viliongezeka kutoka kwa visa 52 mwaka 2014 na 66 mwaka uliotangulia.
Waziri wa Ulinzi wa Tanzania Dkt Hussein Mwinyi, amenukuliwa na gazeti la Daily News mjini Dar es Salaam akisema nchi hiyo bado haijapokea ripoti hiyo.
“Tutakuwa katika nafasi nzuri ya kutangaza msimamo wa taifa letu tukipokea ripoti hiyo na kuitathmini,” waziri huyo alinukuliwa na gazeti hilo.
Tanzania ilikuwa na wanajeshi 2,158 na polisi 74 katika vikosi vya Umoja wa Mataifa mwaka jana.
Tanzania imeorodheshwa miongoni mwa nchi ambazo zinaongoza kwa visa vya unyanyasaji, ikiwa na visa vitatu.
Visa viwili vinahusu kushiriki ngono na watoto na kingine kinahusu uhusiano wa kimapenzi wa kumtumia vibaya mhusika.
Nchi hizo nyingine ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (inayoongoza ikiwa na visa saba), Morocco, Afrika Kusini, Cameroon, Congo na Gabon. Rwanda inaoongoza kwa tuhuma dhidi ya polisi wake wanaohusika katika vikosi vya Umoja wa Mataifa ikiwa na maafisa watatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni