Siku mbili zimepita tangu kutoweka
kwa mwakilishi wa kituo cha redio cha Sauti ya Ujerumani (Deutsche
Welle) Salma Said visiwani Zanzibar na hadi sasa hajulikani alipo.
Taasisi
za kiraia, mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu na jumuiya
ya waandishi wa habari nchini Tanzania wamelaani kutekwa nyara kwa
mwandishi huyo.Mashirika mengine yameitaka serikali kuhakikisha kwamba Salma Said, mwenye umri wa miaka 45, anapatikana akiwa salama.
Sauti ya Ujerumani ilitangaza Ijumaa kwamba mwandishi huyo alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana.
“Taarifa zilizotufikia hivi punde ni kuwa mwakilishi wetu visiwani Zanzibar, Salma Said (pichani), amekamatwa na watu wasiofahamika kwa sababu ambazo bado DW haijazielewa. Tumezungumza naye akiwa sehemu anayosemekana kushikiliwa na sikiliza kwenye matangazo yetu ya jioni,” idhaa hiyo iliandika katika Facebook.
Mume wa Salma Said, Bw Ali Salim Khamis, amezungumza na mwandishi wa BBC Halima Nyanza kuhusu alivyoachana na mkewe uwanja wa ndege kabla ya kutoweka.
“Yeye alikuwa anaenda Dar es Salaam kwa ajili ya ‘check-in’ na mimi ndiye niliyempeleka uwanja wa ndege mpaka ‘amecheck-in’ pale ndani mi ndio nikaondoka uwanja wa ndege,” amesema Bw Khamis.
“Baada ya muda akaniambia ndege yao imechelewa, itachelewa kuondoka lakini haikupita muda mrefu akanijulisha kwamba kwa njia ya SMS kwamba saa hivi niko chini ya ulinzi nishakamatwa hapa.”
Bw Edwin Nsoko ambaye ni mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari wanaopinga matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu Tanzania amesema wamekuwa wakiwasiliana na vyombo vya usalama na wadau kuhakikisha Bi Salma “anarejeshwa na anakuwa salama na kuendelea na majukumu yake kama kawaida”.
Amesema kufikia sasa hawajaridhishwa na taarifa kutoka kwa vikosi vya usalama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni