Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetangaza kumuunga mkono Rais wa
Yemen Abed Rabbo Mansour Hadi. Naye mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa
wa Yemen, ameonya nchi hiyo itatumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa
wenyewe.
Katika kikao chake cha dharura mjini New York hapo jana, Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa, pia lilielezea dhamira yake kubwa ya kuunga
mkono suala la kuwepo umoja, uhuru na mshikamano wa Yemen, na nia yake
thabiti ya kusimama pamoja na watu wa nchi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na wanachama 15 wa baraza hilo na wamefafanua
kwamba wanaunga mkono uhalali wa Rais Hadi na wametishia kuweka vikwazo
zaidi dhidi ya wanamgambo wa Kishia wanaojulikana kama Houthi, ambao
wanaudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Sanaa.
Kikao cha baraza hilo kimefanyika wakati ambapo Yemen inakumbwa
na mashambulizi, yakiwemo yale ya kujitoa muhanga wiki iliyopita katika
misikiti mjini Sanaa na kuwaua watu 142. Kundi lenye itikadi kali
linalojiita Dola la Kiislamu-IS limekiri kuhusika na mashambulizi hayo.
Uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, umefikiwa baada ya Rais
Hadi kuliomba baraza hilo kupitia barua kufanya kila liwezekanalo
kuingilia kati haraka. Akizungumza katika mji wa kusini wa Aden, ambao
ameutangaza kuwa mji mkuu wa muda, Rais Hadi amewataka waasi wa Houthi,
kuondoka kwenye mji mkuu, Sanaa pamoja na miji mingine.
Ama kwa upande mwingine, Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen,
Jamal Benomar ameonya kuwa nchi hiyo inaelekea kutumbukia katika vita
vya wenyewe kwa wenyewe. Akizungumza na baraza hilo kwa njia ya video
kutoka Doha, Qatar, Benomar amesema ghasia za Yemen zinafanana na mizozo
ya Iraq, Libya na Syria.
Hadi amlaumu mtangulizi wake
''Matukio ya wiki na siku za hivi karibuni yanaonekana kuitoa Yemen
katika amani na kuipeleka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tangu
Rais Hadi awasili Aden, ameanzisha kile kinachoitwa kamati inayomtii,
ambayo sasa inaidhibiti Aden na anamtuhumu kiongozi wa zamani, Rais Ali
Abdullah Saleh na waasi wa Houthi kwa kufanya mapinduzi dhidi yake,''
alisema Benomar.
Benomar amezitaka pande zinazohasimiana kujizuia na mapigano na kuacha
kutumia nguvu na amesema ili nchi hiyo iweze kusonga mbele, amani
itapatikana kwa njia ya mazungumzo pekee.
Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power amesema watu
wa Yemen wanazidi kujikuta katika hali mbaya, kwani wataendelea kukumbwa
na madhara iwapo pande zote hazitoacha mapigano mara moja na kuirejesha
Yemen katika kipindi cha mpito cha kisiasa.
Wakati huo huo, waasi wa Houthi wametangaza upya hatua yao ya kuitwaa
miji yote ya Yemen, kutokana na mashambulizi ya wiki iliyopita. Hapo
jana, waasi hao waliuteka mji wa Taiz, ambao ni wa tatu kwa ukubwa
nchini Yemen.
Kiongozi wa waasi, Abdulmalik al-Huthi amewasihi Wayemen kuhamasishana
na kujiunga na wapiganaji wake dhidi ya Dola la Kiislamu na Al-Qaeda
kusini mwa nchi hiyo. Huthi pia ametishia kujiondoa katika mazungumzo
kati ya makundi pinzani ya Yemen, yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa,
akikataa pendekezo la Saudi Arabia kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo.
23 Machi 2015
Umoja wa Mataifa kumuunga mkono
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni