01 Desemba 2014

Kafulila: Mambo manne yalinitia nguvu

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ametaja mambo manne yaliyompa ujasiri wa kulikomalia suala la ukwapuaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow hadi kufikia hatua aliyosema imempa faraja katika maisha yake.
Mbunge huyo kijana, ndiye aliyeibua sakata hilo wakati wa Bunge la Bajeti akituhumu kuwapo kwa wizi wa zaidi ya Sh200 bilioni zilizowekwa kwenye akaunti hiyo iliyofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania, kutunza fedha ambazo Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) lilitakiwa liilipe Kampuni ya ufuaji umeme ya IPTL kusubiri uamuzi wa mahakama kuhusu kesi iliyofunguliwa na Tanesco kupinga viwango vya tozo hiyo.
Hoja hiyo ilijadiliwa kwa siku tatu na Bunge na baada ya mjadala mkali, Jumamosi Bunge lilifikia maazimio ya kutaka waliohusika wote, ambao ni wanasiasa, wafanyabiashara, waajiriwa kwenye ofisi za umma na taasisi zilizohusika za fedha, kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Baada ya kuwasilisha hoja hiyo Mei 8, mwaka huu akihusisha mawaziri wawili, Kafulila alilalamika bungeni kuwa anatishiwa maisha, lakini alionekana kutotetereka hadi Bunge lilipofikia uamuzi Jumamosi.
“Mambo manne yaliyonipa ujasiri wa kulisimamia hili na kuona kuwa hatua zinachukuliwa ni pamoja na Mosi, utata wa kifo cha waziri wa zamani wa Fedha, Dk William Mgimwa,” alisema mbunge huyo kutoka NCCR-Mageuzi akiongeza kuwa kifo hicho kilimshtua na mazingira yake yalikuwa na utata kiasi cha kuona kuwa kuna haja ya kukomalia sakata la escrow.
“Baada ya kifo chake, kichwa kilini-click, nikajua tu hapa kuna kitu. Sikutaka kuishia hapa. Kuna kifo cha meneja biashara wa petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza ambaye alijiua baada ya kutoka Dodoma… kuna utata utata hapa,” aliongeza Kafulila.
Ofisa huyo wa Ewura alijiua kwa kujinyonga siku moja akiwa kwenye nyumba ya wageni jijini Dar e Salaam baada ya kutoka Dodoma ambako aliitwa kuhojiwa kuhusu kodi za mafuta na makusanyo yake.
“Pili, nilikomalia hili kwa kuwa nilikuwa nina nyaraka 604 za (transactions) za TRA kulalamikia kutolipwa fedha zake za kodi, barua za kutoka na kwenda Hazina, BoT, Benki za Stanbic, Mkombozi, kwenda kwa wahusika wote waliokumbwa na kashfa ya escrow na ndiyo maana sikuwa na hofu hata kidogo.
“Tatu, ushahidi wa mauziano ya hisa kwa Kampuni ya Mechmar (iliyokuwa inamiliki hisa za IPTL) kwenda kwa Kampuni ya Piperlink Limited ya British Virgin Island na mengine mengi na nne, nilikuwa ninajiamini kwa kuwa nilikuwa na barua ya TRA iliyokuwa ikilalamikia kutolipwa kwa kodi ya ongezeko la thamani baada ya kufanyika kwa miamala mbalimbali.”
Kafulila (32), ambaye alidokeza kuwa anataka kutunga kitabu kuzungumzia suala la escrow, alidai kuwa alipata vikwazo vingi kwani wabunge wengi walidhani anafanya mzaha na ndiyo maana wakampuuza, lakini anasema alisimamia alichokiamini.
“Nimejifunza mengi katika hili, mwanzoni nilipuuzwa niliambiwa tena na (Waziri wa Nishati na Madini,) Profesa (Sospeter) Muhongo kuwa ninataka kuichonganisha Serikali, nina nyaraka za uongo na hakuna uhakika wa ninachokisema na kwamba ninatumiwa,” alisema Kafulila.
“Waliniambia ninatumiwa na IPTL kuichafua Serikali. Niliambiwa ninatumiwa na (Mwenyekiti wa Kampuni za IPP,) Reginald Mengi- huyo Mengi sijawahi kukaa naye hivi- kummaliza Profesa Muhongo, na wapo waliosema ninatumiwa na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono kuchafua wengine. Yapo mengi yamesemwa, lakini sikutetereka.”
Akizungumzia kuyaweka maisha yake rehani, alisema kuwa kazi ya ubunge ina changamoto nyingi lakini anaamini amepunguza kasi ya wabaya wake kwa kuliweka bayana suala hilo.
“Unajua ninajiamini kwa kuwa nimelisema. Nisingesema maadui zangu wangetumia njia mbalimbali kunimaliza,” alisema Kafulila aliyedai pia kuwa amekuwa akitishiwa maisha mara kwa mara kutokana na kuliibua sakata hilo la escrow.
Alisema anaamini Rais Jakaya Kikwete atafanya kazi baada ya kupitia maazimio.
yote ya Bunge na kuwawajibisha wote waliohusika kwa kusababisha hata taifa ‘kukatiwa’ misaada.
na mataifa hisani pamoja na kuchafua taswira ya nchi kwa wahisani hao.
Kafulila alisema pia kuwa atahoji utekelezaji wa maazimio yote manane katika bunge lijalo la Januari 27, 2015 kuwa kwa kiasi gani yametekelezwa, kwani tayari Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameahidi kuyafanyia kazi kwa umakini zaidi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU
KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU

TANGAZO LA KAZI -Commited youth agricultural organisation CYAO is looking for a person who is specialised in agriculture

POSITION DESRIPTION;

Agricultural Technician

Qualifications

Diploma in agriculture

Mode of application applicant must send an updated Cv,birth cirtificate,one recent passport size, an accademic cirtificate, age limit 20 to 35

apply to Project cordinator,Commited youth agriculture organisation,P.O.Box 78438 Dar es salaam or you can call through +255657990920/+255754823728