22 Desemba 2014

Kitendawili cha Escrow: Chadema yaongeza orodha

Dar es Salaam. Masikio ya Watanzania leo yameelekezwa kwa Rais Jakaya Kikwete watakapokuwa wakisikiliza hotuba yake kwa Taifa inayotarajiwa kujibu maswali yapatayo 10 ambayo yanatarajiwa kutegua kitendawili cha kashfa ya uchotaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Maswali hayo yanatokana na maazimio ya Bunge ambayo yalionekana kuvuta hisia za wananchi katika kona mbalimbali za nchi ambako walikuwa wanafuatilia moja kwa moja mjadala wa Bunge hadi kupitishwa maazimio hayo.
Hotuba hiyo inayotarajiwa kutolewa wakati Rais atakapozungumza na wazee wa Dar es Salaam, ikiwa ni siku nne baada ya Kampuni za IPTL na Pan Africa Power Solutions (PAP) kukimbilia mahakamani kuzuia utekelezwaji wa maazimio ya Bunge.
Baadhi ya wasomi nchini wamesema hatua ya kuzuia utekelezaji wa maazimio hayo pamoja na kauli ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kuwa akijiuzulu Rais atamshangaa, ni mambo yanayofanya hotuba ya Rais kusubiriwa kwa hamu.
Swali la kwanza ambalo wananchi wanasubiri jibu lake ni iwapo Rais Kikwete atatuliza kiu yao kuhusu kashfa hiyo ambayo imekuwa gumzo nchi nzima na hivyo kulegeza msimamo wa wahisani wa kuinyima nchi misaada.
Pili, wananchi wanasubiri kusikia iwapo Rais Kikwete ataagiza uchunguzi zaidi wa Takukuru, Polisi na vyombo vingine kama ambavyo azimio la kwanza la Bunge linavyotaka wahusika wachukuliwe hatua za kisheria kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Tatu, wanasubiri kwa hamu kuona hatua ambayo Rais Kikwete atachukua dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi pamoja na Profesa Tibaijuka kutokana na kutajwa katika maazimio hayo ya Bunge.
Kwa nyakati tofauti, viongozi hao wamekaririwa wakisema kuwa hawahusiki na kashfa hiyo. Mbali ya Profesa Tibaijuka kujitokeza kujitetea mwenyewe, baadhi ya wananchi wamejitokeza kuwatetea na kuwasafisha viongozi hao katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Nne, Je, atatengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme (Tanesco) ambayo pia ilitakiwa kuwajibishwa ikiwa chini ya Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Robert Mboma.
Tano, ili kuwachukulia hatua majaji waliotajwa, Aloysius Mujulizi na Profesa Eudes Ruhangisa, Rais Kikwete anatakiwa aunde Tume ya Kijaji ya kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili zinazowakabili, kinachosubiriwa kwa hamu ni kuona endapo ataunda tume hiyo.
Swali la sita linalohitaji jibu linahusu kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi. Kinachosubiriwa ni jibu la Rais Kikwete iwapo Serikali itaandaa na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia masuala hayo.
Vilevile, wananchi wanatazamia kupata suluhisho la gharama kubwa za umeme katika jibu la Rais Kikwete iwapo Serikali iko tayari kuinunua mitambo ya Kampuni ya IPTL kama ilivyopendekezwa na Bunge kwa lengo la kuokoa fedha za Tanesco zinazotumika kununua umeme kwa bei ya juu.
Pia huenda katika hotuba hiyo, litapatikana jawabu iwapo Serikali itakuwa tayari kuwasilisha mikataba ya umeme bungeni au kwenye kamati zake kwa lengo la kuliwezesha Bunge kutekeleza vyema wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri.
Mbali na mawaziri waliotajwa, pia Rais Kikwete akiwa Mkuu wa nchi na kiongozi wa Serikali, kauli yake juu ya watendaji wengine wa Serikali na watu wengine waliotajwa katika kashfa hiyo inasubiriwa kwa hamu.
Pengine swali jingine zito linalosubiri majibu ni Rais atachukuliaje kitendo cha IPTL na PAP kufungua kesi kupinga maazimio ya Bunge na hoja kuwa liliingilia mihimili mingine ya dola.
Matarajio ya wasomi, wanasiasa
Pamoja na maswali hayo, wasomi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wana maoni tofauti kuhusu matarajio hayo. Mhadhiri wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jesse James alisema: “Kesho (leo) Watanzania wanaweza kufurahi au kukasirishwa. Nasema hivyo kwa sababu hatujui Rais Kikwete ameshauriwa nini kuhusu suala hili la escrow.”
Alisema ni vigumu kujua kama atatekeleza maazimio ya Bunge kwa kuwa kimya chake kililenga kupata ushauri wa chama chake cha CCM na Serikali.
“Kwanza kuna hii kesi iliyofunguliwa mahakamani kuzuia utekelezaji wa maazimio ya Bunge na hii kauli ya Profesa Tibaijuka kuwa hajiuzulu. Mambo hayo mawili bado yanatuweka njiapanda,” alisema Jesse.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema: “Nina wasiwasi kama Rais atatekeleza maazimio ya Bunge. Kwanza, tangu aliporejea kutoka katika matibabu amekuwa kimya, hajazungumza kuhusu suala hili, ni kama wiki tatu sasa zimepita. Pili, ni Ikulu kusema kuwa inafanya uchunguzi kuhusu wahusika, wakati tayari uchunguzi umefanyika na Bunge limetoa maazimio.
Sasa huu uchunguzi mwingine wa kazi gani. Pia Profesa Tibaijuka ametamka wazi kuwa hawezi kujiuzulu. Kwa mambo hayo machache sidhani kama Rais atamwajibisha mtu hapo.”
Kuhusu kesi iliyofunguliwa mahakamani, Profesa Mpangala alisema: “Kwa nini kesi ifunguliwe sasa wakati maazimio ya Bunge yametolewa wiki zaidi ya tatu zilizopita?”
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Professa Tolly Mbwete alisema: “Sikuona sababu ya wahusika kuzungumza kabla ya aliyewateua kuzungumza kuhusu escrow na tuhuma zinazowakabili aliowateua.”
Alihoji sababu ya waliokwenda mahakamani kufanya hivyo na kusema hatua hiyo inazidisha maswali mengi kwa wananchi na kuwa mtihani kwa Rais.”
Hata hivyo, Profesa Mbwete alisema mahali suala la escrow lilipofikia, ni wakati mwafaka kwa Rais Kikwete kulimaliza kabisa: “Anatakiwa kuchukua hatua bila kuogopa jambo lolote. Si vyema kuendelea na jambo hili katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.”
Chadema yataka Waziri wa Fedha, Gavana waingizwe
Mbali na wale waliotajwa katika maazimio ya Bunge, Chadema kimemtaka Rais Kikwete kuwawajibisha Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu kwa kuhusika katika suala la escrow.
Kauli hiyo inafanana na ile iliyotolewa na Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba aliyesema Bunge limefanya makosa ya kutozijumuisha Wizara ya Fedha na ile ya Viwanda na Biashara katika uchunguzi huo kwa kuwa nazo zinahusika.
Viongozi wengine waliotajwa na Chadema kuwa wanastahili kuwajibishwa na Rais Kikwete leo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba.
Desemba 4, mwaka huu, Jaji Warioba alisema uamuzi wa Bunge uliilenga Wizara ya Nishati na Madini lakini utoaji wa fedha hizo uliihusu zaidi Wizara ya Fedha na usajili wa Kampuni uliihusu Brela ambayo iko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Arcado Ntagazwa alisema Watanzania wanasubiri Rais Kikwete kumchukulia hatua Mkuya kwa sababu wakati fedha za escrow zinatolewa BoT kati ya Septemba na Desemba mwaka jana, alikuwa kaimu waziri wa fedha.
Kuhusu, Gavana Ndulu, Ntagazwa alisema anatakiwa kuwajibishwa kwa sababu hakuna benki inayoweza kufanya miamala ya mabilioni ya fedha bila BoT kuidhinisha.
“Kupitia Benki ya Stanbic, Sh160 bilioni zilibebwa kwa magunia, malumbesa na sandarusi ndani ya siku moja, BoT hawawezi kukwepa kuwajibishwa kwa kuwa walifahamu kutolewa kwa fedha hizo,” alisema Ntagazwa.
Alisema Dk Likwelile akiwa mtendaji mkuu wa wizara alitakiwa kuzuia uchotwaji wa fedha hizo huku Mkurugenzi wa Tanesco, Mramba ambaye ndiye Katibu wa Bodi ya Tanesco anatakiwa kuwajibishwa kwa sababu licha ya kufahamu uchotwaji wa fedha hizo hakuchukua hatua zozote.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chadema, Benson Kigaila alisema chama hicho kimepata taarifa za kiintelijensia kwamba Rais Kikwete ana mpango wa kuwalinda Profesa Muhongo na Maswi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU
KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU

TANGAZO LA KAZI -Commited youth agricultural organisation CYAO is looking for a person who is specialised in agriculture

POSITION DESRIPTION;

Agricultural Technician

Qualifications

Diploma in agriculture

Mode of application applicant must send an updated Cv,birth cirtificate,one recent passport size, an accademic cirtificate, age limit 20 to 35

apply to Project cordinator,Commited youth agriculture organisation,P.O.Box 78438 Dar es salaam or you can call through +255657990920/+255754823728