13 Desemba 2014

NEC wataka JWTZ, Ukawa wapinga

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetaka uboreshwaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura usimamiwe na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Imesema kila wilaya nchini itakuwa na askari sita wa JWTZ ambao watashirikiana na wataalamu wanne wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka Nec na kampuni inayotengeneza vifaa vya uandikishaji.
Akizungumza katika mkutano baina ya tume hiyo na wadau wake juu ya hatua iliyofikiwa katika kuboresha daftari hilo, Mkurugenzi wa Nec, Julius Malaba alisema timu hiyo itasimamia uandikishaji na kufanya matengenezo madogomadogo ya vifaa wakati wa uandikishaji iwapo yatahitajika.”
Hata hivyo, mpango huo wa kutumia JWTZ umepingwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wakisema unaweza kuliingiza Taifa kwenye machafuko.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema kwa mpango huo, Nec inaweza kuiingiza nchi kwenye machafuko kama yaliyotokea katika nchi nyingine.
Alisema kulitumia jeshi ni sawa na kuondoa demokrasia ambayo imezoeleka kwa Watanzania na kusisitiza kuwa tangu nchi imepata uhuru, hakuna siku ambayo jeshi lilitumika kwenye masuala ya uchaguzi wala uandikishaji wa daftari la wapigakura.
“Hii mitambo ya BVR kwani ni ya kijeshi mpaka mnasema jeshi litumike kusimamia daftari hili? Tumieni busara ili demokrasia iendelee kuwapo nchini,” alisema Dk Slaa.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Chama cha Sauti ya Umma (Sau), Johnson Mwangosi alisema tangu mwaka 1995, vyama vya siasa vilikataa jeshi kuingizwa kwenye siasa, hivyo hakuna sababu kusimamia daftari hilo wala kujihusisha na uchaguzi.
Pia aliiomba Nec kutotumia Vitambulisho vya Taifa katika mchakato huo akisema ni Watanzania wachache wenye vitambulisho hivyo.
Mwenyekiti wa ADC, Said Miraji alisema: “Kutumia jeshi kwenye uandikishaji ni sawa na kutokomeza demokrasia iliyopo nchini.”
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Sheweji Mketo alisema: “Ni kosa kulihusisha jeshi katika hili. Haya ni matokeo ya Nec kutovishirikisha vyama vya siasa katika kuandaa taratibu za maboresho haya.”
Kaimu Katibu Mkuu wa NCCR - Mageuzi, Faustine Sungura alisema: “Kulitumia jeshi ni sawa na kuwaambia wananchi wasijitokeze kabisa kujiandikisha. Wakiwaona watashindwa kujiandikisha, watakaopiga kura watakuwa wachache.”
Kaimu Katibu Mkuu wa UDP, Isaack Cheyo alisema, “Kuruhusu jeshi kushiriki siasa ni kuipeleka nchi kubaya, hakuna sababu za msingi ambazo zimetolewa na Nec.”
Aliongeza: “Huko mbinguni tutaadhibiwa wote lakini nyinyi ( Nec) mtaanza kupigwa viboko kwanza kwa jambo hili ambalo mnataka kuwatendea wananchi kwa kuwanyima demokrasia yao.’’
Akijibu hoja za wadau hao, Kamishna wa Nec, Profesa Amon Chaligha alisema: “Tumesikia malalamiko yenu. Tutayafanyia kazi hasa kuhusu kutumia askari wa JWTZ.”
Mkuu wa kitengo cha Tehama cha Nec, Dk Sisti Karia alisema kila mwananchi ataandikishwa katika daftari hilo na hakutakuwa na makosa kama yaliyotokea miaka ya nyuma.
“Tunajua kuwa kuna maeneo umeme hakuna. Tunapenda kuwaeleza kuwa mashine hizi za BVR zinatumia umeme wa jua na hivyo kurahisisha kazi,” alisema.
Alisema hivi karibuni, walizijaribu mashine hizo katika shule mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa kuwaandikisha wanafunzi na kuanzia saa nane mchana hadi saa 12 jioni waliweza kuandikisha watu 140.
Pia, aliahidi Nec kushirikiana viongozi wa vyama vya siasa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mashine hizo mpya pamoja na mchakato mzima wa uandikishaji.
Majaribio ya uandikishaji Jumatatu
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Nec, Jaji Hamid Mahamoud Hamid alisema uandikishaji wa daftari hilo utatanguliwa na ule wa majaribio kuanzia Desemba 15 hadi 21 mwaka huu.
Majaribio hayo yatafanyika katika majimbo matatu ya uchaguzi ambayo ni Kawe (Dar es Salaam), Kilombero (Morogoro) na Mlele (Katavi).
“Vyama vya siasa vitaruhusiwa kuweka mawakala wao ili kushuhudia uandikishaji. Mpaka sasa Tume imepata vifaa 107 vya utambuzi wa mpigakura vya kielektroniki (BVR), vingine vilivyobaki vitapokewa wiki hii ili kufikia 250. Tukianza rasmi tutatumia BVR 8,000.”
Alisema baada ya uandikishaji kukamilika, daftari la awali la wapigakura litawekwa wazi ili kama kuna mapingamizi yatolewe na kushughulikiwa sambamba na kuboresha taarifa za wapigakura.
“Tume inatarajia kuwa Daftari la Kudumu la Wapigakura litakuwa tayari Aprili 28, 2015. Uandikishaji katika mikoa yote utafanyika kwa awamu nne katika kila halmashauri ili kutoa fursa ya kuhamisha vifaa vya uandikishaji kutoka eneo moja kwenda jingine,” alisema.
Alisema muda wa uandikishaji utakuwa siku saba katika kila kituo na kufanya siku za uandikishaji kuwa 28 kwa kuwa kila halmashauri itagawanywa mara nne.
“Mgawo huo utatokana na idadi ya vituo vya kujiandikisha vilivyopo pia idadi ya wapiga kura wanaolengwa kuandikishwa kwa mujibu wa takwimu za sensa zilizotolewa. Uboreshaji wa daftari utahusisha wapigakura wote, wapya na wa zamani,” alisema.
Alisema Vitambulisho vya Taifa na vya sasa vya kupigia kura vitatumika katika uandikishaji ili kurahisisha uchukuaji wa taarifa za wapigakura.
Wasomi wanena
Profesa wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (Duce), Kitila Mkumbo alisema ni jambo la kushangaza kwa JWTZ kusimamia uandikishaji huo kwa kuwa lina mambo mengi ya kufanya.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema si mara ya kwanza kutumia jeshi nchini kwenye masuala ya kisiasa kwani hata mwaka 1995, JWTZ lilitumika kusafirisha masanduku ya kura.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU
KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU

TANGAZO LA KAZI -Commited youth agricultural organisation CYAO is looking for a person who is specialised in agriculture

POSITION DESRIPTION;

Agricultural Technician

Qualifications

Diploma in agriculture

Mode of application applicant must send an updated Cv,birth cirtificate,one recent passport size, an accademic cirtificate, age limit 20 to 35

apply to Project cordinator,Commited youth agriculture organisation,P.O.Box 78438 Dar es salaam or you can call through +255657990920/+255754823728