14 Desemba 2014

Serikali ya awamu ya nne kumaliza vibaya’

Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Awamu ya Nne imebakiza takriban mwaka mmoja kuondoka madarakani, sifa ya Tanzania kwenye jumuiya ya kimataifa imeendelea kutiwa doa kutokana na kuhusishwa na ongezeko la ufisadi wa mabilioni ya fedha za umma na ujangili.
Kutokana na hali hiyo, huenda uongozi wa awamu hiyo iliyo chini ya Rais Jakaya Kikwete ikaiacha nchi vibaya na historia ya pekee ya kuwapo kwa ‘mikwaruzano’ kati yake na wafadhili mbalimbali wanaoelezwa kutoridhishwa na namna fedha za umma zinavyochotwa na wajanja wachache wakiwamo viongozi wa umma.
Alipotafutwa kuzungumzia hali hiyo na hatua ya wafadhili kusitisha misaada yake kwa Serikali inayoisimamia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Kwanza sina taarifa za kutosha kuhusu msimamo wa Marekani na suala zima la MCC na escrow zaidi ya kuziona kwenye magazeti yenu.”
Aliongeza: “Kwa kuwa sina taarifa rasmi, siwezi kusema chochote kuhusu hilo.”
Juzi, Balozi wa Marekani nchini, Mark Childressi alieleza kuwa nchi yake haitatoa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Milenia (MMC) kwa Serikali ya Tanzania, hadi itekeleze maagizo ya Bunge kuhusu uchotwaji wa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow. Kauli ya kiongozi huyo imedhihirisha ukubwa wa tatizo hilo, ingawa Ikulu imeshasema haitekelezi maagizo kwa shinikizo la misaada.
Katika tamko lake kwa umma, balozi Childress alisema: “Kupigwa hatua katika mapambano dhidi ya rushwa ni muhimu sana kwa mkataba mpya kati ya MCC na Tanzania na katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara Tanzania.”
Aliongeza: “Tunatoa wito kwa Serikali kuchukua hatua za haraka kuhusu suala hili hasa kutokana na uzito wake katika masuala muhimu kadhaa ya maendeleo.”
Uamuzi huo umekuja wiki kadhaa baada ya wafadhili katika nchi mbalimbali nao kuzuia kiasi kikubwa cha fedha kutokana na sakata la uchotaji wa fedha za escrow Sh306 bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Hata hivyo, Waziri wa Fedha Saada Mkuya akizungumzia taarifa hizo hivi karibuni, alisema hakuna mfadhili aliyekataa kutoa fedha, bali mazungumzo yalikuwa yakiendelea vizuri.
“Nataka kuwahakikishia kwamba washirika wetu wa maendeleo ambao wanatoa fedha kwa mfumo kusaidia bajeti kuu ya Serikali, hawajasitisha msaada.
Kulikuwa kuna majadiliano baada ya kuonyesha wasiwasi...Walikuwa wakisubiri Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili waweze kutoa. Fedha hizo ni Sh922 bilioni na hapa tunapozungumza Finland na Idara ya Maendeleo ya Kitaifa (DFID) wameshatoa kiasi chao,” alisisitiza.
Hata hivyo, wakati Serikali ikisema hayo, Wakala wa Uchunguzi wa Mazingira (EIA) wameitaka MCC kutokubali kuidhinisha mkabata huo na Tanzania wa Dola 450 milioni za Marekani (Sh700 bilioni), hadi Rais Kikwete atakapochukua hatua stahiki dhidi ya rushwa iliyotawala na sakata la ujangili na usafirishwaji wa pembe za ndovu kwenda nje hasa China.
Taasisi hiyo inayojihusisha na masuala ya mazingira, ilitoa wito huo jana kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry na Mwenyekiti ambaye pia ni Mkurugenzi wa MCC, Diana Hyde kwamba wasitishe hatua hiyo kwa Tanzania.
Novemba mwaka huu, EIA ilitoa ripoti ya utafiti wa ujangili uliyoanika madudu dhidi ya mauaji ya tembo na namna meno yanavyotoroshwa nchini.
Hali hiyo inaelezwa huenda ikapunguza nguvu na jitihada za Rais Jakaya Kikwete ambaye amekuwa akisisitiza kuwa anakwenda nje mara kwa mara kwa ajili ya kuonana na wafadhili ili waisaidie nchi kiuchumi. Jitihada za kumtafuta Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na naibu wake, Mwigulu Nchemba kwa siku mbili mfululizo hazikufanikiwa kutokana na simu zao kutopokelewa na hata walipotumiwa ujumbe mfupi haukujibiwa.
Hata hivyo, Msemaji wa wizara hiyo, Ingiahedi Mduma alisema kuwa Balozi wa Marekani nchini, Childress alitoa taarifa hiyo kwa nafasi yake.
“Anaweza akawa amesema yeye kwa nafasi yake na waziri pia alizungumza kwa nafasi yake. Lakini kama waziri alisema hizo fedha zitatolewa mwezi Desemba, tusubiri huu mwezi uishe ndipo tujue,” alisema Mduma.
“Kinachohitajika sasa ni kuwa na subira, kama kutakuwa na mabadiliko yoyote tutawajulisha kwa sababu Desemba haijaisha na kauli aliyotoa ya waziri ni nzito,” alisisitiza Mduma.
Mduma alibainisha kuwa MCC walisema wanatoa fedha hizo, hivyo lazima kusubiri kwani wanaweza kuamua kutoa sasa au hata mwakani.
Mkuu wa Kitivo cha Biashara Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Deogratius Massawe alisema iwapo MMC itazuia fedha hizo, Serikali italazimika kukopa fedha kwenye mabenki ya ndani.
Aliongeza kuwa pia baadhi ya miradi iliyokuwa ikisubiri fedha hizo itakwama kukamilika, huku sekta binafsi nayo ikiathirika. “Kutokana na kukosekana kwa fedha za kigeni thamani ya fedha itashuka, sekta binafsi zitaathirika kwa sababu benki zitakimbilia kuikopesha Serikali,” alisema Massawe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat), Dk Didas Massaburi akizungumza jana, alisema kuwa wafadhili wameamini maneno ya upotoshaji yanayosemwa na baadhi ya wabunge kuwa fedha za escrow ni za Serikali. Alisema siyo kweli kwamba fedha zilizochotwa ni za umma badala yake Serikali inadai kodi ambayo haiwezi hata kufika Sh26 bilioni.
Mkazi wa Kijitonyama wilayani Kinondoni, Leonard Gingo alisema uamuzi wowote utakaochukuliwa na serikali kukabiliana na suala hilo, utakuwa umechelewa.
“Wananchi tumesubiri nani anawajibishwa kwa kufukuzwa au kusimamishwa kazi wakati hatua zinachukuliwa, kitu cha ajabu watuhumiwa bado wapo ofisini, wengine tumewaona wakitia saini mikataba,” alisema Gingo.
Alisema haki nzuri ni ile inayotolewa kwa wakati na kwa mtu sahihi na kwamba kuendelea kusita kuchukua hatua ni kuendelea kuwapa watuhumiwa nafasi ya kuficha ushahidi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU
KUWEKA TANGAZO LAKO HAPA NI BEI NAFUU

TANGAZO LA KAZI -Commited youth agricultural organisation CYAO is looking for a person who is specialised in agriculture

POSITION DESRIPTION;

Agricultural Technician

Qualifications

Diploma in agriculture

Mode of application applicant must send an updated Cv,birth cirtificate,one recent passport size, an accademic cirtificate, age limit 20 to 35

apply to Project cordinator,Commited youth agriculture organisation,P.O.Box 78438 Dar es salaam or you can call through +255657990920/+255754823728