Mazungumzo ya kujaribu kutafutia ufumbuzi mzozo wa kisiasa nchini Burundi yamefanyika nchini Uganda.
Hata hivyo washiriki wamekosa kuelewana kuhusu siku ya kuanza kwa mazungumzo kamili.Majadiliano hayo, yaliyoongozwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni, yalikuwa ya kuweka mikakati ya kufanyika kwa mazungumzo ya kina kuhusu mzozo nchini humo.
Machafuko yalianza Burundi baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kuwania uchaguzi kwa muhula wa tatu.
Alishinda uchaguzi huo uliofanyika Januari.
Mkutano huo uliafikia mazungumzo ya kina yaanze Januari 6 mjini Arusha, Tanzania lakini ujumbe wa serikali ya Burundi umesema hakukuwa na “makubaliano kuhusu tarehe hiyo”.
Msemaji wa afisi ya rais wa Burundi Willy Nyamitwe alitoa taarifa kwa vyombo vya habari baada ya mazungumzo ya leo akipinga tarehe hiyo.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika ikulu ya rais wa Uganda mjini Entebbe.
Rais Museveni, aliyeteuliwa na viongozi wa kanda kuongoza mazungumzo hayo, ametoa wito kwa upande wa serikali kutochukua msimamo mkali.
"Wanaweza kuwa wahalifu lakini kwa sababu za kuleta amani wacha watu hawa tuwape kinga ya muda. Hata nyinyi wakati ule mlikuwa mnavunja haki za binadamu (mlipokuwa waasi), kama vile kuua raia wa kawaida,” amesema.
“Huo ni uhalifu wa kivita hata mkiwa waasi. Mkiwa waasi kuweni waasi wazuri, msiwe waasi wabaya kwa kuwaua raia ambao si askari. Unaweza kutenda uhalifu wa kivita ukiwa serikalini au upande wa upinzani.”
Muungano wa Afrika umesema unapanga kutuma walinda amani 5,000 nchini humo, hatua ambayo imepingwa na serikali ya Burundi.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Burundi Alain-Aime Nyamitwe aliongoza ujumbe wa serikali kwenye mazungumzo hayo.
Awali naibu kwanza wa mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD FDD Victor Burikukiye alikuwa ametoa masharti kadhaa ikiwemo kutokubali kukaa katika meza moja na "wauaji waliopanga mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli”.
Kulikuwa pia na wawakilishi kutoka vyama vya upinzani na makundi ya kiraia.
Watu zaidi ya 300 wameuawa nchini Burundi tangu kuanza kwa machafuko nchini Burundi mwezi Aprili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni