Siku chache baada ya kulaza Manchester United, Stoke City wameandikisha ushindi muhimu Ligi ya Uingereza kwa kucharaza Everton.
Stoke walilaza United 2-0 Jumamosi, na leo hii wamepata ushindi wa 4-3 dhidi ya Everton uwanjani Goodison Park.
Walikuwa nyuma bao moja dakika ya 80 kabla ya Roselu kuwasawazishia na kisha Marko Arnautovic akawafungia la ushindi dakika za mwisho kupitia mkwaju wa penalti baada yake kuangushwa eneo la hatari.
Kwingineko, Tottenham Hotspur wameondoka Watford na ushindi wa 2-1, bao lao la ushindi wakilifunga dakika ya 89 kupitia Son Heung-min.
Watford walicheza zaidi ya dakika 35 wakiwa kumi uwanjani baada ya Nathan Ake kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea visivyo mchezaji wa Spurs Erik Lamela.
Norwich City nao wamepata ushindi wa 2-0 nyumbani dhidi ya Atson Villa, West Bromwich Albion wakashinda Newcastle United 1-0 nao Crystal Palace wakaridhika na sare na Swansea.
Kwenye mechi za baadaye, Arsenal watakuwa nyumbani dhidi ya Bournemouth, Manchester United wasakate gozi nyumbani dhidi ya Chelsea nao West Ham wakaribishe nyumbani watakatifu wa kutoka St Mary’s, Southampton.
Matokeo kamili:
- Crystal Palace 0 - 0 Swansea
- Everton 3 - 4 Stoke
- Norwich 2 - 0 Aston Villa
- Watford 1 - 2 Tottenham
- West Brom 1 - 0 Newcastle
- Arsenal v Bournemouth 20:30
- Man Utd v Chelsea 20:30
- West Ham v Southampton 20:30
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni