Maafisa wa Ulinzi
wa Kenya wamenasa shehena kubwa ya silaha, kufuatia operesheni ya
kuwasaka wapiganaji wa Al Shabaab Kaskazini mwa Kenya.
Idara ya polisi imesema kuwa maafisa wake walinasa risasi, vilipuzi, bunduki na vifaa vinavyotumika kutengeneza mabomu ambazo zinaaminika kuwa ya wapiganaji wa Harakat walio na uhusiano na kundi la Al Shabaab nchini Somalia.
Wapiganaji kadhaa wa kundi hilo ambao walikuwa wakisafirisha silaha hizo, walikamatwa na wanazuiliwa na maafisa wa polisi.
Kundi hilo linasemekana kuwa na majukumu ya kuwasilisha na kutoa mafunzo kwa wapiganaji wapya na hatya kujiunga na mapigano na mashambulio dhidi ya vituo vya umma.
Kukamatwa kwa shehena hiyo ya silaha ni pigo kubwa kwa kundi hilo la al-Shabaab. Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita wapiganaji wa al shabaab wamejaribu kuingiza silaha na kufanya mashambulio nchini Kenya.
Maafisa wa ulinzi na upelelezi nchini Kenya wameimarisha juhudi zao ya kupambana na kundi hilo kwa kuwakamata washukiwa wa kundi hilo na hata kushambulia kambi zao.
Wapiganaji kadhaa wa kundi hilo kwa sasa wanazuiliwa na polisi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni