BONGE la soo! Katika hali ya kushangaza, msanii wa filamu Vicent
Kigosi ‘Ray’ hivi karibuni alijikuta akiangua kilio ukumbini baada ya
mshindi wa shindano la kusaka vipaji vya kuigiza kufananishwa na
marehemu Steven Kanumba.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita katika Ukumbi wa
Makumbusho ya Taifa, Posta, jijini Dar kulipokuwa na fainali za Shindano
la Tanzania Movie Talents (TMT) ambapo washiriki 10 ndiyo walikuwa
wakiwania kitita cha shilingi milioni 50.
Mara baada ya mshindi wa shindano hilo kutangazwa, ukumbi mzima
ulizizima kwa kelele za furaha na kwenda kumpongeza Dennis Laswai
aliyeibuka kidedea na wengi walikubaliana kuwa ni haki yake kutokana na
kufanya vizuri.
Wakati mshindi na mashabiki wake wakiendelea kufurahia ushindi, kundi
la vijana lilipanda jukwaani wakiwa wameshika fulana yenye picha ya
marehemu Kanumba huku wakisema mrithi wake amepatikana.
Ndipo ghafla, Ray ambaye alikuwa na upinzani wa kisanii na muigizaji
huyo, alipoanza kumwaga machozi hadharani na kujikuta amezungukwa na
watu wakimshangaa.
“Jamani mrithi wa Kanumba amepatikana rasmi baada ya miaka mitatu
kuishi bila yeye, sasa jembe limerejea tena, mama yetu hapaswi kuwa na
simanzi kila siku,” kijana mmoja alisikika akisema huku akienda kumshika
mkono mama Kanumba.
Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa Ray baada ya mmoja wa vijana hao
kumfuata na kumuonesha fulana hiyo ambapo alizidisha kilio kiasi cha
wenzake kumfuata na kumtuliza ili awe katika hali ya kawaida.
Mtu mmoja ukumbini hapo alibeza kilio hicho, akisema hiyo yote
ilitokana na kuzidisha ‘kiburudisho’ na wala haikuwa kwa sababu ya
kummiss sana marehemu kwani hawakuwahi kuwa na ukaribu wa kiwango hicho.
“Ray hana lolote, pale amezidisha kiburudisho tu, hakuwa na mapenzi
na Kanumba kiasi hicho mpaka leo hii alie vile, ni usanii tu hakuna
lolote. Wapo watu wa kulizwa na kitu kama kile na si yeye, halafu Ray
huwa hana ushirikiano mzuri na wasanii wenzie hasa wa kiume,” alisema
mtu huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Kwa upande wake Ray alisema kilichomtoa machozi ni ukweli kwamba
mshindi ana kipaji cha hali ya juu na yeye binafsi alipenda ushindi wake
kiasi kwamba mawazo yake yalimfikisha mbali.
Imeandaliwa na Shani Ramadhani, Mayasa Mariwata na Musa Mateja.
27 Agosti 2015
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni