Sakata la wafanyabiashara kufunga maduka kwa siku kadhaa katika
baadhi ya miji nchini wakipinga matumizi ya Mashine za Risiti za
Kieletroniki (EFD) limeelezwa kukumbwa na vikwazo kutoka kwa baadhi ya
vigogo kunufaika na mashine hizo.
Hatua hiyo ya wafanyabiashara kufunga maduka huwa
inawaathiri wananchi wengi kwa kukosa huduma. Tatizo hilo limekuwa
likitokea hasa katika Jiji la Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inasema mashine
za EFD zinazotumia nchini ni za kipekee, kwa kuwa zinatumia mfumo ambao
hautumiki sehemu nyingine yoyote ulimwenguni. Mashine hizo hutuma
taarifa za mauzo moja kwa moja TRA.
Pamoja na ufafanuzi ambao umekuwa ukitolewa mara
kwa mara na TRA na serikali kwa ujumla, bado wafanyabiashara
wanalalamikia namna mfumo huo unavyofanya kazi, pamoja na bei ya kununua
mashine hizo kuwa kubwa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania,
Johnson Minja, siku chache baada ya kuachiwa kwa dhamana kutoka Gereza
la Isanga Dodoma, ana mengi ya kusimulia baada ya kukumbwa na misukosuko
mingi, ikiwemo ya kushikiliwa kwa kukiuka masharti ya dhamana aliyokuwa
amepewa.
Minja anasema wafanyabiashara nchini wanakumbana
na changamoto nyingi, ambazo zimekuwa zikiwapa hasara wao na Serikali
kwa upande mwingine. Anasema changamoto, namba moja, ni ujio wa mashine
za EFD.
Minja anasema mashine za EFD hazikuingizwa nchini kwa lengo la kuongeza kodi ama mapato ya Serikali.
Anafafanua akisema pamoja na udhaifu uliopo kwenye
mashine hizo, kuweza kutafutiwa ufumbuzi kirahisi, kikwazo kikubwa ni
baadhi ya vigogo serikalini kutaka kutumia nguvu kuhakikisha kuwa
mashine zote zilizopo stoo, zinauzwa kwa wafanyabiashara.
Akionyesha mashine ya EFD, Minja anasema: “Hii
mashine ni biashara ya mtu. Sisi China tunaiona inauzwa Sh30,000 lakini
tunauziwa Sh800, 000. Wanasema inapatikana Tanzania pekee yake, yaani
Tanzania ambayo ya mwisho kwa teknolojia leo imegeuka kuwa ya kwanza kwa
teknolojia ulimwenguni!”
Akionyesha kushangazwa na bei hiyo, anahoji:
“Tofauti ya kuuza mashine kutoka 30,000 hadi Sh800,000 ni nini? Sasa
simu yangu ya Nokia inauzwa Sh30,000 ina tochi na vitu vingine, kununua
laini ya simu itaongezeka Sh1,000. Sasa kwa sababu ni biashara ya mtu
mkubwa anataka kuhalalisha kuwakandamiza Watanzania.”
Mwenyekiti huyo anasema kuwa misingi ya kisheria
ya kitaalamu ya namna ya kutoza kodi imekiukwa na kwamba njia pekee ya
kurejesha hali ya kibiashara mahali pake ni kwa Serikali kufuata
mtiririko wa kulipa kodi.
Anasema ingekuwa vyema kama mashine za EFD
zingekuwa zinaonyesha taarifa na mlolongo wote wa ununuzi. Hivi sasa
mashine hizo hunakili taarifa za mauzo pekee, bila kutambua
mfanyabiashara alinunua bidhaa kwa shilingi ngapi, aliisafirisha kwa
gharama gani au ameilipia kodi shilingi ngapi bandarini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni