Ukisoma vitabu vya historia utaona kuwa nyayo za mtu wa zamani
aliyeanza kutembea kwa miguu miwili zilipatikana katika Kijiji cha
Endeluni, wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Kijiji hiki kipo kilometa 34 kutoka Makao Makuu ya
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na eneo halisi lenye alama hizo za
historia ya binadamu linajulikana kama Laetoli.
Tukiwa katika jopo la waandishi wa habari,
tumewasili eneo la Laetoli ambalo kwa jamii ya Kimasai lina maana ya
eneo lenye vitu vizuri, kwa kuwa lina bonde, miti na uwanda wa kupendeza
wenye nyasi nzuri kwa ajili ya malisho ya mifugo ya nyumbani na wale wa
porini na maji mengi kutoka Mto Ngarusi.
Tunapokewa na Simel Odorop (29) anajitambulisha
kuwa yeye ni mlinzi mkazi wa Kijiji cha Enduleni. Anakiri kuwa pamoja na
umaarufu wa eneo hilo, jamii haijanufaika kiuchumi kwa kuwa wageni
hawafiki wengi, eneo hilo la kihistoria.
“Wageni hasa Wazungu wachache wanaokuja hapa
wanataka kuona nyayo halisi lakini wakifika wanaonyeshwa kaburi
zilimofikiwa. Wapo wanaotaka wafukue ili waone nyayo hizo, lakini
tunawakataza,” anasema.
Anasema Serikali iliamua kuzifukia nyayo hizo
ikisubiri ijengwe makumbusho ambayo itaweza kutunza vizuri nyayo hizo
ili watalii wawe wanafika kuziona.
Godfrey Olle Moita ni mhifadhi wa mambo ya kale,
anasema umaarufu wa eneo hilo utaongezeka mara mpango wa ujenzi wa
makumbusho hiyo utakapokamilika.
“Eneo hili lina historia ya kipekee maana nyayo za
Zamadamu Aferensis (Australopithecus Aferensis) watatu ziligundulika
zenye umri wa miaka 3.6 milioni. Walishabihiana na binadamu wa sasa.
Walitembea kwa miguu miwili wakiwa wima. Hii ni historia ya kipekee,”
anasema.
Tangu nyayo hizo zimefukiwa, anasema ni miaka
zaidi ya 20 imepita lakini baada ya ujenzi kukamilika zinaweza
kufukuliwa na kuonekana vizuri bila kuathirika.
Anasema ufukiaji ulitumia mbinu za kitaalamu
ambazo zinaweza kuzifanya zisiathirike kwa namna yeyote ile na
zikifukuliwa zitaonekana kama zilivyogundulika. Nyayo ambazo zina umri
wa miaka 20 tangu zimefukuliwa kisayansi ili mataifa mbalimbali
yashuhudie maajabu hayo kabla ya kuzifukia mwaka 1998 miaka 17
iliyopita.
Anasema maajabu hayo ni kivutio kikubwa cha utalii
ambacho kwa miaka zaidi ya 37 kilikuwa chini ya Mambo ya Kale,
kikitumika kama sehemu ya utafiti.
Kwa sasa, anasema kimehamishiwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kinapaswa kutangazwa kama kivutio cha utalii wa kipekee.
Ziligunduliwaje
Mwaka 1976, Andrew Hill na David Western, watafiti
washiriki kwenye timu ya Dk Mary Leakey wakiwa Laetoli baada ya
kumaliza kazi wakawa wanacheza huku wanatupiana kinyesi kikavu cha
tembo.
Dk Hill alipoangalia chini aligundua alama
zilizokuwa kwenye mwamba, ndipo mwaka 1978 Dk Paul Abell aligundua
zilikuwa nyayo za binadamu wa kale. Uchunguzi wa kihistoria ukabaini
kuwa ni nyayo za binadamu wa kale ajulikanaye kama Zamadamu ambaye
alitembea wima kwa miaka milioni 3.6.
Kabla ya hapo inaaminika kuwa binadamu alikuwa anatembea kwa miguu na mikono, kama ilivyo wanyama.
Changamoto zinazowakabili
Anasema kuwa mmomonyoko unaosababishwa na maji,
upepo na uzito wa udongo katika eneo hilo ni miongoni mwa mambo ambayo
wanahisi yanaweza kusababisha alama hizo za kale kuathirika. Mambo
mengine anasema ni wadududu wanaochimba ardhi kama vile panya wanaweza
kuathiri pamoja na mizizi ya mimea katika eneo hilo ambalo zilifukiwa
futi tano kwa udongo.
Hali ya hewa ya joto na baridi vinaweza kuathiri hali ya udongo hivyo alama kupotea au kupoteza uhalisia.
Wageni wachache kufika eneo hilo
“Tunapata wageni wachache sana wanaokuja hapa
licha ya umaarufu huu, hasa wanatoka Marekani ambako mgunduzi alitokea,
lakini kila anayefika, hurejea kwao akiwa hana furaha kwa sababu
hatekelezi kiu yake.
Kinachowaudhi ni kwamba licha ya kulipia, hawaoni
kitu halisi bali eneo ambalo alama hizo zimefukiwa na katika hali ya
kutoridhika huomba kama kuna uwezekano zifukuliwe ili baada ya kuziona,
zifukiwe.
Siyo wageni tu ambao hupata adha hiyo bali hata
wanafunzi hapa nchini ambao hufika eneo hilo ili wajifunze mambo ya
historia ambayo wameyasoma vitabuni.
Kutokana na hali hiyo, watalii wengi hukata tamaa
ya kufika maeneo hayo na hasa ikizingatiwa kuwa baada ya kutoka nchini
huwaeleza wenzao hali halisi.
Hii ni kusema watalii wengi ambao wangeweza kufika nchini ili
kuona maajabu hayo ya kihistoria, wanashindwa kuja kwa sababu tu
wamepata habari kuwa nyayo hizo kwa sasa zimezikwa ardhini.
Hivyo ni muhimu kwa Serikali kuhimiza ujenzi wa makumbusho hayo, ili kuongeza mapato ya Serikali yanayotokana na utalii.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni